in

Yanga, Azam, Simba kwenye ‘vita ya vigogo wa soka’ Afrika?

Azamfc

SASA ni rasmi Julai 16 mwaka huu wa 2021 Kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka barani Afrika(CAF) itakutana nchini Morocco kujadili mfumo wa mashindano mapya ya CAF Super League au maarufu kwa jina lingine la African Super League.  Mashindano hayo yamepewa baraka na rais wa FIFA Giani Infatino ambaye kwa nyakati tofauti alionesha matamanio makubwa ya kuanzishwa kwake, lakini alikuwa kwenye mtihani wa kupata ushirikiano kutoka rais wa CAF. 

Hata hivyo baada ya CAF kupata rais mpya Dkt. Patrice Motsepe ikawa rahisi mno kwa ajenda ya Infatino kupitishwa kwa vile wote wawili wana mitazamo sawa. Katika makala haya ninaleta masuala muhimu yanayopaswa kufahamishwa kwa mashabiki.

Je CAF Super League ni mashindano ya namna gani?

Michuano hiyo itashirikisha timu 20 za Bara la Afrika. Tayari timu 15 zimepatikana, ambapo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba ni miongoni mwa timu zitakazoshiriki mashindano ya Ligi hiyo maalumu ya vigogo wa soka barani Aftika. Timu zingine ni Wydad Casablanca (Morocco), Raja Casablanca (Morocco), Burkane (Bukina Fasso), Al Ahly (Misri),Zamalek(Misri),Pyramids(Misri),Mamelodi Sundowns(Afrika kusini),Orlando Pirates(Afrika kusini),Kaizer Chiefs (Afrika kusini),TP Mazembe (DRC),AS Vita(DRC), Al Hilal (Sudan), Al Merreikh (Sudan) na Horoya (Guinea). Bado timu 5 kukamilisha idadi ya 20 ya kushiriki mashindano hayo.

Ni sababu zipi za kuanzisha CAF Super League?

Tangu mwaka  2020 rais wa FIFA Giani Infantino alipodokeza mipango ya kuanzisha African Super League  alikosa mtu sahihi wa kuunga mkono mkakati huo kwa manufaa ya soka la Afrika. Baada ya kuchaguliwa rais mpya wa CAF, Dkt Patrice Motsepe ndipo nguvuya kuanzishwa mashindano hayo imeongezeka huku wadau wa soka wakisema kiongozi huyo mpya ni kama kiranja tu wa michuano hiyo kwani mwenye wazo ni Giani Infatino na FIFA yake. 

Kwa mtazamo wa FIFA inaamini mashindano haya mapya ya African Super League yatatengeneza kiasi cha dola milioni 200 kwa bara la Afrika. Kwamba timu zinazopaswa kushiriki lazima ziwe 20 na kuifanya kuwa Ligi kubwa duniani. Vilevile ni kuhakikisha African Super League inazalisha vipaji vikubwa kama George Weah, Samuel Eto’o, Mohammed Salah, Nwakwo Kanu, Sunda Oliseh, El Hadji Diouf, Didier Drogba, Rigobert Song, Lucas Radebe, Michael Essien, Salif Diao,Khalilou Fadiga,Moustapha Haji, Geremi Njitap,Hossam Hassan, Mohamed Mido, na wengineo.

Msingi wa mashindano hayo unatokana na mafanikio hafifu yaliyopo katika timu za bara la Afrika kwenye mashindano ya kimataifa yakiwemo Klabu Bingwa dunia. Msimu uliopita klabu ya Al Ahly ilitolewa katika hatua ya nusu fainali ya Klabu Bingwa  dunia na Bayern Munich baada ya kuzabwa mabao 2-0, lakini bado safari ya mafanikio ya klabu za Afrika ni hafifu mbele ya tiu za Ulaya. 

Pia Ligi za Afrika ziko nyuma kimafanikio na maendeleo mara 10 nyuma ya timu za Ulaya. Hivyo kuwa chanzo cha timu na ligi kuwa dhaifu. Inaelezwa kuwa michuano ya African Super League itakuwa chachu ya ongezeko la uwekezaji na mapato kwa klabu na mchezo wenyewe.

Je mashindano hayo yanaweza kuleta mabadiliko Afrika?

Mpango huo unafanana na ule wa Bodi ya Mchezo wa Kikapu na Chama cha Mchezo wa Kikapu nchini Marekani (NBA) ambapo wameanzisha Ligi maalumu ya mpira wa Kikapu barani Afrika, “Baskeball Africa League” inayoshirikisha timu 12 kutoka kaskazini hadi kusini mwa Afrika. Mpango wa kuanzisha “Basketball Africa League” ulipaswa kutimu vumbi mwaka 2020 lakini kutokana na mlipuko wa ugonjwa corona umesimamishwa kwa muda. Aidha, mpango wa kuanzisha Ligi ya Afrika inatarajiwa kuondoa vikwazo vya maendeleo kwa vilabu,timu za taifa,vipaji vya soka na uongozi pamoja na kuongeza tija ya miundombinu.

Je muundo gani utatumika katika mashindano hayo?

Hili ni swali ambalo Kamati yaUtendaji na rais wa CAF Patrice Motsepe wanatakiwa kuleta majibu mbele ya wadau wa soka. Kimahesabu bado timu tano ili kukamilisha idadi kamili za timu zktakazoshiriki mashindano hayo. Zipo kanda tano; kanda ya Afrika Magharibi (Horoya ya Guinea na Burkane ya Burkinafasso); kanda ya Afrika kaskazini (Raja Casablanca na Wydad Casablanca za Morocco, Pyramids,Al Ahly na Zamalek za Misri); kanda ya Kusini mwa Afrika (Orlando Pirates,Kaizer Chiefs na Mamelodi Sundowns za Afrika kusini); kanda ya Afrika mashariki (Simba ya Tanzania); kanda ya Afrika ya Kati (TP Mazembe na AS Vita za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Al Hilal na Al Merreikh za Sudan).

Kuna timu zingine vigogo kama Etoile Du Sahel,Esperance, Club Africain za Tunisia nazo zina hadhi sawa na zingine hapo juu, je zitaachwaje au vigezo gani vitatumika kuziingiza? Na kama timu yoyote ya Tunisia itaingai maana yake ukanda wa Afrika kaskazini zitakuwa na jumla ya timu 6.

Je mgawanyo wa kanda utakuwa jibu?

Vilabu vinavyotoka chama cha soka cha kusini mwa Afrika, COSAFA ni vitatu; Mamelodi Sundwons,Kaizer Chiefs na Orlando Pirates ambazo zinatoka nchi moja; Afrika kusini. Wanachama wengine wa COSAFA wameambulia patupu. 

Wanachama wa Afrika mashariki CECAFA wanawakilishwa na klabu za Al Hilal na Al Merreikh za Sudan na Simba ya Tanzania. Wanachama wa Afrika magharibi (WAFU) wanawakilishwa na klabu za Burkane ya Burkina fasso na Horoya ya Guinea. Pale Afrika ya kati timu zote zinatoka DR Congo yaani TP Mazembe na AS Vita.

Bara la Afrika lina jumla ya nchi 56, ambazo ndizo wanachama wa shirikisho la soka CAF.  Hii ina maana ukitazama timu zinazofanya vizuri utaona zinatoka katika mataifa ya Morocco,Tunisia,Misri,Afrika kusini na DR Congo, pamoja na baadhi ya mataifa ya Nigeria,Ghana na Ivory Coast. Katika muktadha huu naona ugumu utakavyokuwa kwenye suala la kuchagua vilabu vyitano vilivyobaki kuingia kwenye African Super League.

Je gharama za mashindano mapya kwa klabu zitakuwaje?

Ifahamike gharama za Ligi ya Mabingwa Afrika zinasababisha kuonekana mashindano hayo kutokuwa na faida kwa timu. Gharama za usafiri wa ndege ni eneo ambalo linasumbua timu nyingi za Afrika. Hivi karibuni imeshuhudiwa timu ya taifa ya Gabon ikilala uwanja wa ndege kwa sababu ya gharama.

Wakati CAF ikitarajiwa kuongeza mapato kwa timu bado hali ya mashabiki na timu gharama ni kubwa. Suala la usafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine limekuwa tatizo kubwa linaloambatana na gharama. Hata kama wataendesha mashindano hayo kwenye nchi moja maana yake kutakuwa na gharama za uendeshaji pia.

Nini hatima ya Ligi ya Mabingwa Afrika?

Mvuto unaotengenezwa kwenye Ligi ya Mabingwa ukiletewa mashindano ya African Super League bila shaka kutakuwa na hasara kwa upande mmoja. Ligi ya Mabingwa inaweza kuathirika kutokana na kupoteza mvuto kwa watazamaji na wawekezaji. Pamoja na nia nzuri ya kuboresha soka barani Afrika ni wazi nafasi ya Ligi ya Mabingwa inatishiwa na mashindano mapya ikiwa yataanza. Na hilo litakwenda sambamba na ushindani kutoka ligi zingine za nje  hasa lina;ofika suala la muda wa mchezo.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
England

Ni jaribio la pili kwa Southgate na England

Patrik Schick, Gianluigi Donnarumma, Pedri na Kalvin Phillips

EURO na kuzimwa kwa ndoto ya England