in , , ,

YALIYOJIRI LIGI KUU YA ENGLAND

Wiki ya 37 ya Ligi Kuu ya England imehitimishwa wikiendi hii ambapo Stoke City wamekuwa timu ya kwanza kushuka daraja huku Chelsea wakiimarisha mbio zao za kugombania nafasi kwenye nne bora. Yafuatayo ni mambo kadhaa yaliyojiri kwenye Ligi Kuu ya England wiki hii.

STOKE YASHUKA DARAJA, WEST BROM YAENDELEA KUKOMAA

Stoke relegated from Premier League

Baada ya kudumu kwenye Ligi Kuu ya England kwa misimu 10, hatimaye Stoke City imeshuka daraja baada ya kufungwa kwa 2-1 na Crystal Palace ndani ya dimba la bet365 licha ya wenyeji hao kutangulia kuongoza kwa 1-0 kwenye kipindi cha kwanza cha mchezo huo uliopigwa Jumamosi.

Xherdan Shaqiri aliwaweka Stoke City mbele kwa bao safi la mpira wa adhabu aliouweka moja kwa moja wavuni muda mfupi kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika lakini mabao mawili ya James McArthur na Patrick van Aanholt yaliwapa Crystal Palace ushindi na kuzamisha jahazi la vijana wa mwalimu Paul Lambert.

Kwingineko West Bromwich Albion wameendelea kukomaa wakipambna kubaki kwenye Ligi Kuu ya England licha ya kuwa walikuwemo kwenye hatari ya kuwa timu ya kwanza kushuka daraja kwa wiki kadhaa. Ushindi wa 1-0 dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye mchezo wa Jumamosi umewafanya wabaki na nafasi ya kujaribu kujinusuru.

Jack Livermore aliwafungia West Brom bao hilo muhimu katika dakika za nyongeza na kuipandisha timu yake kwa nafasi moja hadi nafasi ya 19. Sasa kuna tofauti ya alama 2 kati ya West Brom na Southampton walio kwenye nafasi ya 17 na tofauti hiyo hiyo ya alama nyuma ya Swansea walio kwenye nafasi ya 18. Mchezo wa Jumatano kati ya Southampton na Swansea utawashusha daraja West Brom ikiwa hautaisha kwa sare.

CHELSEA YAJIIMARISHA VITA YA NNE BORA

‘Jürgen Klopp gets animated on the Stamford Bridge touchline’

Chelsea walipopoteza kwa 3-1 nyumbani dhidi ya Spurs mwezi mmoja uliopita, walijikuta wakiwa nyuma ya timu hiyo iliyokuwa kwenye nafasi ya nne kwa alama 8 huku zikiwa zimesalia mechi 7 pekee. Pia kulikuwa na alama 10 zilizowatenganisha vijana hao wa Antonio Conte na Liverpool waliokuwa kwenye nafasi ya tatu.

Lakini baada ya bao la kichwa la Oliver Giroud lililowapa Chelsea ushindi wa 1-0 dhidi ya Liverpool siku ya Jumapili, vita ya kuwania nafasi nne za juu sasa iko wazi. Vijana hao wa Stamford Bridge sasa wanahitaji kushinda michezo yao miwili wiki hii dhidi ya Huddersfield na Newcastle na kuomba Liverpool au Spurs wapoteze alama ili kuingia kwenye nne bora na kukata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa.

Vijana wa Klopp wao wanahitaji kushinda mchezo wao wa mwisho dhidi ya Brighton katika dimba la Anfield Jumapili ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Hata hivyo hata wakishindwa kuitumia nafasi hii wanabaki na fursa ya kutimiza lengo hilo kupitia kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa mbele ya mabingwa wa kihistoria, Real Madrid Mei 26.

MAN CITY WASHEREHEKEA UBINGWA, WENGER AAGWA KWA USHINDI MNONO

Baada ya mchezo ulioisha kwa sare ya bila mabao dhidi ya Huddersfield siku ya Jumapili, Manchester City walikabidhiwa rasmi kombe lao ndani ya dimba la Etihad. Hata hivyo City walikosa ushindi ambao ungewawezesha kuvunja rekodi ya alama nyingi zaidi kwenye msimu wa EPL na ile ya mabao mengi zaidi kwenye msimu mmoja.

Sare dhidi ya Huddersfield imewafanya kuwa na jumla ya alama 94. Wanahitaji alama 2 kwenye michezo miwili iliyosalia kuvunja rekodi ya alama 95 iliyowekwa na Chelsea kwenye msimu wa 2004/05. Pia wanahitaji mabao mawili kuvunja rekodi ya mabao 103 iliyowekwa na Chelsea kwenye msimu wa 2009/10. Ushindi mmoja zaidi pia utawafanya kuvunja rekodi ya kushinda michezo mingi zaidi ya EPL kwa msimu (31).

Kwaheri na Asante AW

Kwingineko Arsene Wenger aliiongoza Arsenal kwenye mchezo wake wa mwisho kabisa ndani ya dimba la Emirates kwa mtindo wa kupendeza kwa kuisambaratisha Burnley kwa kipigo cha 5-0. Pierre-Emerick Aubameyang aliweka mawili wavuni kwenye karamu hiyo ya kumuaga Wenger aliyedumu na klabu hiyo kwa zaidi ya miongo miwili. Mabao mengine yalifungwa na Iwobi, Kolasinac na Lacazette.

mail to:[email protected]

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Yanga ina kikosi chepesi katika michuano migumu

Tanzania Sports

TEKE LA AZAM KWA BOCCO, LILIMPA KASI CHURA