in , , ,

YA MONTELLA NA ALLEGRI YANA HUZUNISHA UKIYAKUMBUKA YA CAPELLO NA ANCELOTTI

Ni kawaida maji kujaa na kupwa kwenye bahari, na hii yote huonesha
dunia hupita kwenye majira tofauti yaliyoambatana na nyakati tofauti.

Ndiyo maana majira haya ya mpira pesa yanaambatana na nyakati ambazo
wachezaji wanafikiria zaidi pesa kuliko kutumikia timu zao kwa nguvu
zao zote.

Kujitoa na kupigana kwenye mpira kumepungua kwa kiasi kikubwa, ndiyo
maana huwezi shangaa majira ya mpira damu yaliambatana na nyakati za
wachezaji kulilia kucheza timu zao za taifa, na majira haya ya mpira
pesa yameambatana na nyakati za kina Matip kugoma kujiunga na timu za
Taifa.

Tuko nyakati za hatari sana, nyakati ambazo kwa kiasi kikubwa hatuna
wachezaji ambao wako tayari kujenga historia nzuri ambazo zitakuwa
kumbukumbu kwa siku za mbele.

Majira yaliyopo sasa yanaambatana na hali ya kushangaza sana. Majira
ya mpira damu yaliambatana na nyakati za msisimko katika soka, ndiyo
maana ilikuwa ngumu kwa shabiki yoyote duniani kwa wakati ule kuacha
kuangalia mechi kubwa sana kwa wakati huo ya Juventus na Ac Milan.

Kuukana usingizi kilikuwa kitu cha kawaida tu kipindi kile ilimradi tu
uende ukamwangalie Allessandro Del Piero anavyohangaika kupambana na
Paolo Maldini au Nesta.

Vita ya kina Nedved na Gattusso ilikuwa vita iliyovutia sana machoni
mwa watu. Wizi wa Inzaghi ulikuwa wizi wa kiufundi ambao hata
aliyekuwa anaibiwa ilikuwa lazima afurahi tu kwa kiasi kikubwa.

Buffon alikuwa akitumia muda mwingi kufikiria kujibu michomo mikali
iliyokuwa inatolewa na Dida ili kuoneshana umwamba kati yao.

Leo hii ni tofauti kabisa, badala ya Buffon kutumia muda mwingi
kujibu michomo ya Donnaruma, yeye hutumia muda mwingi kuangalia makosa
ya Donnarruma ili baada ya mechi apate cha kumfunza maana yeye ndiye
afuataye baada ya Buffon kutoka kwenye milingoti mitatu ya timu ya
Taifa.

Leo hii Suso ndiye mhimili mkubwa wa Ac Milan, wakati ukirudisha
nyuma macho yako eneo lile lilikuwa linamilikiwa na Seeedorf, mtu
ambaye hata kiumbo tu anakushawishi kabla hata hujamwangalia akishika
mpira.

Vitu vingi sana vimebadilika, Ushindani wa kimbinu kati ya Fabio
Capello na Carlo Ancelotti ulikuwa wa hali ya juu ukilinganisha na
ushindani wa kimbinu uliopo kwa sasa kati ya Allegri na Montella.

Vitu vingi vinatia huruma sana, vinahuzunisha sana, eti leo hii
Carlos Bacca ndiye mshambuliaji tegemeo la Ac Milan? Ukakasi mkubwa
machoni mwangu unanijia pale ninapofikiria hilo na kumkumbuka Crespo
na Shevchenko.

Sijapata mzani sahihi wa kunidhibitishia ukubwa wa uzito wa Paolo
Dyabala, Higuain dhidi ya uzito wa Trezeguet na Zlatan.

Hata kwa macho ya nyama uzito wa Dyabala ni mwepesi sana juu ya uzito
wa Zlatan. Leo hii M’baye Niang analiliwa wakati ukimrudisha enzi za
nyuma alikuwa hawezi kumweka kwenye mbao Gattusso.

Msisimko wa hii Mechi umepotea sana ndiyo maana nasema haya ya
Montella na Allegri yanahuzunisha sana kama ukijaribu kuyakumbuka ya
kina Capello na Ancelotti. Tokea mwaka 2004 mpaka sasa mambo mengi
sana mazuri yametoweka kwenye Kumbukumbu zetu.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

NILICHOKIONA KWENYE BAADHI YA MECHI ZA EPL.

Tanzania Sports

SINGANO, MAHUNDI KABEBA ‘JENEZA’ BEGANI MWAKE.