in

Wachezaji wa Tanzania watafute ‘Connection’

Mbwana Samatta

Neno ‘Connection’ ni maarufu sana katika mitandao ya kijamii Tanzania. maelfu ya watumiaji  wanafahamu nini kinachojadiliwa mara baada ya neno hilo kutajwa kokote, iwe Facebook,  Instagram, WhatsApp, Snap Chart na kwingineko.  

‘Connection’ mara nyingi linahusisha skendo inayomhusu staa wa Bongofleva, Bongo movie au  raia wa kawaida kutoka taasisi tofauti. Hasa hasa ni skendo za kimapenzi. hata hivyo, neno hilo  linahusisha pia uwezo wa mtu kutengeneza mtandao wa watu ambao wanampa taarifa.  

Ni kwamba mtu anakuwa na watu ambao wanakuwa vyanzo vya kupatikana mfano hizo skendo,  fursa za ajira,biashara na uchumi na mengineyo yenye tija. Tunaweza kulitumia neno hilo kwa  wachezaji wa kitanzania watafute fursa. Mifano ni mingi. 

Kwenye kikosi cha mabingwa wa soka nchini klabu ya Simba msimu 2019-2020 kulikuwa na  wachezaji watatu raia wa Brazil. Kati yao amesalia kiungo Fraga. Ni wachezaji wanaotoka bara  la Amerika kusini. Haswa wanatoka nchi inayosifika kwa kandanda duniani na mabingwa mara  tano wa Kombe la Dunia. Nchi anayotoka Neymar Junior, Ronaldinho,Gilberto Silva,Romario  na mastaa wengine.  

Lakini vipaji vya Kibrazil vimeingia Ligi Kuu Tanzania Bara kuleta maarifa mapya. Pengine si  jambo la ajabu kwa wachezaji wenye ya asili ya Brazil kutua Ligi Kuu Tanzania bara kwa  sababu wamekuwa na utamaduni wa kuzurura nchi mbalimbali kusakata soka. Katika Ligi Kuu  Afrika kusini nyota wa Brazil ni wengi. Hali kadhalika kuna baadhi yao wanacheza Ligi Kuu  Angola maarufu kama Girabola. Rivaldo Ferreira nyota wa zamani wa Barcrlona na Brazil  bingwa wa kombe la dunia alitua Ligi ya Girabola. 

Aidha, nyota kutoka mataifa ya Malawi, Botswana, Angola, Namibia, Swaziland, Zimbabwe, Zambia wamekuwa wakipenya Ligi Kuu Afrika kusini kwa sababu ya ‘Connection’. Nchi hizo  zimekuwa na mastaa wao wanaosakata dimba PSL. Lakini je, wachezaji wa watanzania  hawawezi kutamba PSL? 

Seleman Matola alikuwa kiungo aloyenunuliwa moja kwa moja na Supersports United ya Afrika  kusini kutoka Simba. Ubora na uwezo vilimpeleka Matola bondeni. Lakini wachezaji wengi wa  zamani hapa Tanzania hakuwa na fursa kama zilizopo sasa. Nina uhakika wachezaji wa  kitanzania wanazo sifa za kucheza Mamelodi Sundowns, Orlado Pirates, Kaizer Chiefs, Bidvsest  na nyinginezo za PSL. 

‘Connection’ ya mchezaji wa Kibongo inaweza kumpeleka Ligi Kuu Kongo. Katika ligi hiyo  Tanzania imeweka alama kupitia Mbwana Samatta aliyecheza kwa mafanikio TP Mazembe.  Eliud Ambokile na Ramadhani Singano ni miongoni mwa nyota waliosajiliwa TP Mazembe hata 

kama hawajaonesha viwango vikubwa kama Samatta. Hii nayo ni ligi ambayo tuna ‘connection’  nayo. 

Himid Mao anachezea klabu ya ENNPI ya Misri. Tayari Himid Mao ametengeneza jina lake  vizuri katika Ligi Kuu Misri na bila shaka yoyote ndiye balozi wetu katika soka nchini humo.  Kwamba kampuni ya Siyavuma Sports inayomsimamia Himid Mao ina ‘conneticoon’ ambayo  wachezaji wa kitanzania wanaweza kuitumia kama daraja kupata mafanikio. Inawezekana kabisa  mastaa wetu wakasajiliwa Zamalek, Al Ahly, Pyramid na timu zingine za Misri iwapo  ‘Conneticon’ itatumika vizuri. 

Kwenye Ligi Kuu Moroco ndani ya El Jadida tunao mastaa wawili Simon Msuva na Nickson  Kibabage ambao wanawakilisaha kizazi cha sasa cha soka. kwa mastaa walioko Tanzania kwa  sasa wanaweza kutua Ligi Kuu Moroco kwa sababu Msuva na Kibabage wametengeneza  ‘Connection’ nzuri itakayowavutia makocha na wamiliki wa vilabu kusaka vipaji vya Tanzania. 

Hii ina maana wanasoka wetu kama wanataka kucheza soka la kulipwa maana yake njia  imefunguliwa na vilabu kama Raja Casablanca na Wydad Casablanca zitatoa nafasi kwa  wachezaji wetu. Tayari wameshaona vipaji vitatu; Simon Msuva, Nickson Kibabage na staa wetu  Mbwan Samatta aliyetamba Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutumkia Ublegiji. Ni kwamba  Tanzania ni kisima cha vipaji, lakini wenyewe tupo tayari kutumia ‘connetion’ hiyo kutamba  Morocco? 

Tanzania haijatamba katika Ligi Kuu Tunisia. Hata hivyo vilabu kama Etoile Du Sahel au Club  Africain ni sehemu nzuri ya kuonesha vipaji na kuwa daraja la kusonga mbele. Wachezaji wengi  wa Nigeria kama kama Julius Aghahowa, John Utaka na wengineo walianzia kwao kisha  wakaingia Ligi ya Tunisia kutamba na kusonga mbele hadi Ulaya. Ni ligi ambayo imekuwa  kama daraja kwa wanandinga wengi Afrik,a.  

Kwa maana hiyo ‘Connection’ ambayo tunaweza kuifanya ni pamoja na kuhakikisha fursa za nje  za vilabu vya Afrika mashariki, kati, kusini,magharibi au kokote tunazitumia kama njia ya  kupata maarifa na ‘connection ya kwenda Ulaya. 

‘Connection’ ni muhimu kwao, mawakala wenye viwango pia ni muhimu katika maendeleo ya  soka nchini pamoja na wachezaji wenyewe. Bila ‘Connection’ tutadunisha vipaji vyetu hapa  nchini tu.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Paulo Dybala

‘Ligi ya wahenga’ kupindua utawala Juventus?

Lomana Lualua

Samatta Alitakiwa Awe Mbinafsi