in , , ,

VIPIMO VITANO VYA JULIO NA MWADUI FC

 

Mwadui FC juzi ilitoa sare ya bila kufungana dhidi ya Simba SC kwenye mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam. Baada ya mchezo huo kocha mkuu wa Mwadui FC ya Shinyanga Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alitamba kuwa timu yake iko vizuri mno na imejiandaa vyema kupambana na timu tunazoziita timu kubwa.

 

Julio alisema kuwa timu yake inadharauliwa lakini atazionyesha timu zinazoitwa timu kubwa. Huenda ni kweli kocha huyu anayetambulika kuwa mwenye maneno mengi na kikosi chake kilichosheheni nyota kama Athumani Iddi ‘Chuji’, Uhuru Suleiman, Rashid Mandawa na wengine wanao ubavu wa kufanya maajabu anayoyasema Julio.

 

Kwenye makala hii tunaangalia vipimo vitano vya Julio na timu yake kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu bara itakayoanza kutimua vumbi tarehe 12 Septemba. Vipimo hivyo ni mechi tano ambazo natarajia Mwadui FC wanaocheza ligi kuu msimu huu kwa mara ya kwanza ndani ya kipindi cha miaka 27 watakuwa na wakati mgumu kupata matokeo mazuri.

advertisement
Advertisement

 

1) Toto Africans v Mwadui FC (Septemba 12, 2015)

Mchezo huu utakuwa mgumu na wa upinzani mkubwa kwa kuwa utakuwa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu bara kwa timu zote hizi zilizopanda daraja msimu huu. Nafikiri Julio na kikosi chake watakuwa na kibarua kigumu kwa kuwa watakuwa ugenini kwenye dimba la CCM Kirumba. Ni dimbani ambapo timu ya zamani ya Julio Simba SC iliwahi kupigwa 4-1 mwaka 2008.

 

2) Mwadui FC v Azam FC (Septemba 20, 2015)

Kwenye mchezo huu Mwadui watakuwa wenyeji wa Azam. Julio ameapa kuonyeshana na timu tunazoziita timu kubwa na Azam FC ni moja ya timu hizo. Mwadui watakuwa na wakati mgumu kuwazuia Azam FC wasipate ushindi kwenye mchezo huu ushindi ambao nafikiri ni matokeo pekee ambayo Azam watakuwa wanatarajia kuyapata kwenye dimba la Mwadui siku hiyo.

 

3) Mwadui FC Vs Yanga SC (Oktoba 28, 2015)

Kwenye mchezo huu mabingwa wa Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita watakutana na mabingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita. Ni kipimo kikali kwa kocha Julio ambaye nafikiri ataupania mno mchezo huu kwa kuwa Yanga ni timu hasimu ya Simba SC ambayo ipo moyoni mwa Julio. Yanga pia hawatataka kuruhusu maneno ya jeuri hivyo watakusudia kushusha kipigo kikali.

4) Stand United Vs Mwadui FC (Novemba 7, 2015)

 

Timu hizi zilikuwa kwenye kundi moja (Kundi C) la Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2013/14. Stand United wakawazidi ujanja Mwadui na kupanda daraja mwaka jana. Waliwaacha Mwadui kwenye Ligi hiyo ya Daraja la Kwanza na hatimaye mwaka huu na wao Mwadui wamepanda Ligi Kuu. Hivyo mchezo huu wa ‘Shinyanga Derby’ utakuwa ni mchezo wa visasi. Ni kipimo kikali pia kwa Julio.

5) Mwadui FC Vs Simba SC (Disemba 26, 2015)

 

Siku moja baada ya pilau la Christmas Julio atakutana na timu yake ya zamani Simba SC. Ingawa ana mapenzi binafsi na klabu hii nafikiri hilo halitaweza kubadili nia yake ya kuzionyesha timu tunazoziita timu kubwa. Ikumbukwe juzi timu yake ilitoa sare ya bila kufungana dhidi ya timu hii. Hata hivyo Simba nao hawatakuwa tayari kumruhusu kijana wao awatie aibu. Hivyo Julio atakuwa na kibarua kigumu.

Report

Written by Kassim

What do you think?

72 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Kombe la Ligi ni hivi

Rooney mabao