in

Vionjo vya Ufunguzi wa Olimpiki London

*Siri ya Dany Boyle na wasanii 15,000 yafichuka
Kitakachojumuishwa ndani ya sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya London 2012 ni siri, lakini tunaweza kubashiri kitakachojiri.
Je, tutarajie ngoma itanoga kama ya Beijing miaka minne iliyopita, ambapo tuliona utitiri wa wapiga ngoma 2,008 sawa na mwaka wenyewe?
Au labda labda itakuwa mfano wa ile ya Los Angeles mwaka 1984 tulipoona mtu akiruka kutoka angani kuingia eneo la tukio akijifunga kifaa kinachotumiwa na wanaoruka kutoka kwenye ndege?
Safari hii London tunaye Daniel ‘Danny’ Boyle na jopo lake, ambao kwa hakika wamefanikiwa kwa muda sasa kuficha siri ya kile kitakachojiri Ijumaa hii katika sherehe za ufunguzi.


Boyle aliyezaliwa 1956 ni mkurugenzi na mtayarishaji wa filamu. Amejipatia sifa kwa kazi yake kwenye filamu kama ‘Slumdog Millionaire’, ‘Shallow Grave’, ‘127 Hours’, ‘28 Days Later’, ‘Sunshine’ na ‘Trainspotting’.
Amejizolea tuzo nyingi, ikiwamo ya mkurugenzi bora zaidi na nyingine ya mchango wa kutukuka katika kutayarisha filamu. Juni 2010 ndipo alitangazwa kuwa mkurugenzi wa Sherehe za Ufunguzi wa Michezo hii ya Olimpiki ya London
Katika utaratibu waliojiwekea kwenye maandalizi ya mazoezi ya sherehe za ufunguzi, wanaojitolea wamekula yamini kulinda siri ya wanachojifunza dhidi ya wote walio nje.
Ama kwa wataalamu wa ufundi na wacheza dansi nao wamefungwa na mikataba yao kutoeleza chochote nje ya eneo lile kipi watafanya siku hiyo.
Boyle mwenyewe, akiwa mkurugenzi wa sanaa, ametuma ujumbe binafsi kwa kutumia mitandao jamii ya Facebook na Twitter kwa kila mshiriki na waandaaji binafsi, ili kila mmoja atunze siri ili waje kuwashangaza watu – iwe surprise!
Licha ya wenyewe kujipa majukumu ya kutunza siri ya sherehe za ufunguzi, walinzi kadhaa hufanya kazi ya kushika doria kuzunguka Uwanja wa Olimpiki, kuhakikisha wanahabari hawasogei karibu mno na uwanja – Olympic Park.
Humo ndimo mazoezi yanafanywa, ikiwa ni pamoja na kujaribisha na kurekebisha aina mbalimbali za mavazi yatakayotumika wiki hii.
Mapaparazi hawaruhusiwi hata kusogelea studio zilizo Dagenham au Stratford, ambako maandalizi yanaendelea kwa miezi kadhaa sasa.
Licha ya yote haya, wasaka habari hawakushindwa kudaka hiki na kile na kuviweka pamoja na kupata picha itakavyokuwa kwenye sherehe hizo za ufunguzi zitakazochukua saa tatu.
Boyle mwenyewe ameahidi kwamba kazi itakuwa kubwa, burudani isiyo kifani itakayoacha watu midomo wazi kwa mshangao.
Sherehe za Ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki 2012 zitatangazwa na kurushwa moja kwa moja kufikia watu wanaokadiriwa kuwa bilioni nne – kichocheo na kikolezo chake kikiwa ni mchezo wa kuigiza wa Shakespeare ulioandikwa mwaka 1610 uitwao ‘The Tempest’.
Kwa kuutumia huo, wataionesha dunia kwenye sherehe hizo jinsi visiwa vya maajabu vilivyovuka milima na mabonde, kupita kwenye ukombozi hadi kufanikiwa kuweka hai matumaini ya baadaye.

Mandhari ya Uingereza ya Kale Vijijini

Sehemu ya kwanza ya ufunguzi inatarajiwa kuanza saa tatu usiku wa Ijumaa. Itapambwa na rangi za kijani zenye uzuri wa kuvutia. Ilipangwa kufunikwa na aina ya giza kabla ya nyota wa James Bond, Daniel Craig kuingia uwanjani mithili ya mshuka milima, akitoka kwenye helikopta.
Hapo kengele yenye uzito wa tani 27 itagongwa kuashiria kuanza kwa sherehe zenyewe. Kengele hiyo itakuwa na nukuu kutoka kwenye mchezo wa ‘The Tempest’: “Msiogope, kisiwa kimejaa kelele.”
Ni baada ya hapo ataonekana Kenneth Branagh akisoma yaliyoandikwa kuuhusu mchezo huo.
Nyuma yataonekana mandhari ya maeneo ya vijijini ya Uingereza miaka iliyopita – vijumba vilivyoezekwa kwa makuti na wanyama hai.
Imepangwa wawepo punda 12, ng’ombe watatu, kondoo 70, mbwa watatu wenye sura za kondoo na plau.
Kadhalika wataonekana watumishi wakamua maziwa, familia zilizo kwenye pikniki, mfano wa timu ya kriketi ya kijiji ambayo wachezaji wake wamevalia nguo za vitambaa laini, kofia huku wengine wakicheza muziki.
Inasemwa kwamba Boyle amepata kufikiria hata kutengeneza mawingu bandia ya kuashiria mvua ili kutoa mandhari halisi anayotaka.

Sanaa Kukumbushia  Mapinduzi ya Viwanda

Tukio la pili katika sherehe hizo linatarajiwa kusheheni mambo ya enzi za mapinduzi ya viwanda. Pamoja na mambo mengine, wafanyakazi watavalia kama wafumaji, wachimba madini, wafanyakazi wa kwenye viwanda vya chuma na wahandisi. Wataonekana pia wakipumzika baada ya kazi ngumu. Hiyo itakumbushia enzi zile Uingereza ikichukuliwa kuwa karakana ya dunia – ikiongoza kwa uzalishaji na uchumi imara kadhalika.

Vionjo vya Uingereza ya Kisasa

Pamoja na siri kutunzwa, inajulikana kwamba mchezo wa tatu katika mfululizo wa sherehe za ufunguzi utahusisha matumaini kwa maisha ya baadaye Uingereza.
Wasanii watakuwa wameshaondoka zama za giza, mapinduzi ya viwanda na sasa wataiigiza Uingereza yenye vitu kama Big Ben na vivutio vingine vinavyoipa London sura yake ya sasa.
Hapa patakuwapo gwaride la wauguzi na wafanyakazi shirikishi kwenye sekta ya afya.
Hawa wataonesha jinsi Mpango wa Huduma za Afya (NHS) ulivyopiga hatua kuhudumia watu wa aina mbalimbali. Waigizaji wataonekana wakisukuma vitanda hispitalini kuashiria watu wenye afya waishio Uingereza.
Wasaniii watatumia aina tofauti za utamaduni wa Uingereza kufikisha ujumbe kwa mamilioni ya watu watakaokuwa wakifuatilia moja kwa moja ufunguzi huo.
Watakuwapo wasakata dansi watakaowaenzi wanamuziki maarufu kama wa The Beatles na wengineo.
Hao watajumuisha kundi la London Rockin’ Rollers, ambapo jumla ya waigizaji, wanamuziki, wacheza dansi, wapiga ngoma na wanaoteleza kwa vibao vyenye matairi watakuwa 15,000
Boyle anaandaa, na siku hiyo atasimamia wasanii watakaoonesha sura za utamaduni mbalimbali wa watu kutoka pande tofauti za dunia wanaoishi nchini Uingereza.
Hao watatumika pia kuonesha uwapo wa matukio mbalimbali kama ya kisiasa na maandamano kudai haki za wafanyakazi.
Sir Paul McCartney anatarajiwa kufunga pazia la sherehe za ufunguzi huo kwa kutoa burudani. Huyu ni mmoja wa wanamuziki wanaoheshimika zaidi nchini Uingereza, aliyetamba na The Beatles na bado anacheza muziki.

Kumpokea Mkuu wa Nchi

Malkia Elizabeth II, mkuu wa nchi mwenyeji atapokewa kwenye lango la Uwanja na Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), Jacques Rogge.

Maandamano ya Wanamichezo Washiriki

Timu kutoka mataifa shiriki zitaingia kwa kuzingatia mtiririko wa alfabeti. Hata hivyo Ugiriki itaingia ya kwanza, kwani ndio waasisi na wenyeji wa kwanza wa Olimpiki.
Aidha Uingereza (Team GB) ambayo ni mwenyeji wataingia wa mwisho. Timu zitafanya gwaride na kujipanga katika aina ya duara lililoumuka pande mbili, mfano wa track ‘M25’.
Kati ya watakaobeba bendera za mataifa yao ni mchezaji tenisi wa Urusi, Maria Sharapova, aliyepata kuwa bingwa wa Wimbledon.
Wengine ni mwanariadha wa Afrika Kusini, Caster Semenya na Laura Flessel-Colovic wa Ufaransa.
Baada ya hotuba za Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Olimpiki London (LOCOG), Lord Coe na ya Rais wa TOC, Rogge zitafunga hatua za awali.
Baada ya hapo ataalikwa Malkia Elizabeth II atakayetangaza kufunguliwa rasmi kwa michezo hii, ambapo Bendera ya Olimpiki itaingizwa uwanjani na kusimikwa wakati wimbo husika ukichezwa.
Mwanamichezo mshiriki, jaji na kocha kutka taifa mwenyeji watasimama kando ya mimbari, wakishika kona ya Bendera ya OIC kwa mkono wa kushoto na kuipandisha kwa ule wa kulia, kula kiapo cha Olimpiki, wakiahidi kushiriki na kutoa uamuzi kwa mujibu wa kanuni za michezo husika.

Mwenge wa Olimpiki

Moto wa Olimpiki utaingizwa uwanjani, ukipitishwa kwa wanamichezo washiriki hadi kwa mkimbiza mwenge wa mwisho – ambaye bado jina lake na anakotoka ni siri.
Huyo kazi yake itakuwa kwenda nao hadi kwenye Mwenge wa Olimpiki na kuuwasha, na itakuwa ishara wazi ya kuanza rasmi kwa michezo yenyewe. Ni baada ya hapo fataki na fashifashi zitapigwa angani na kengele itapigwa kwa mara ya mwisho kuashiria amani.

Wageni Maarufu Hafla ya Ufunguzi wa Olimpiki 2012

Wageni watakaohudhuria hafla ya uzinduzi wa Michezo ya Olimpiki 2012 wanajumuisha watu maarufu zaidi duniani.
Hao ni pamoja na wakuu zaidi ya 120 wa nchi na serikali, idadi itakayofanya kuwa kusanyiko kubwa zaidi la wakuu wa nchi kupata kufanyika nchini Uingereza.
Kamati ya Maandalizi ya Michezo ya Olimpiki London (LOGOC) wanafanya kila linalowezekana kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza na ofisi ya Jumuiya ya Madola, kuepusha viongozi wa nchi hasimu kujikuta wamekaa pamoja.
Rais Vladimir Putin wa Urusi ameeleza nia yake ya kutazama mchezo wa judo, licha ya tabia yake ya kihasama kwa Uingereza.
Mgeni anayetarajiwa kwamba uwapo wake utazua utata ni Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, ambaye kwa bahati mbaya hajawekewa vikwazo vya kusafiri na Umoja wa Ulaya (EU).
Hali yake inamwezesha kusafiri hadi London japokuwa wengi hawangependa, tofauti na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye amepigwa marufuku na umoja huo kusafiri katika nchi zake wanachama.
Ahmedinejad amedokeza kwamba atatua London siku moja kabla ya kuzinduliwa mashindano hayo kwa ajili ya kuwaunga mkono wanamichezo 50 wanaopeperusha bendera ya nchi yake.
Kiongozi huyo anakengeuka tishio lao la awali la nchi hiyo kususia mashindano haya, kwa madai nembo yake ni ya Kizayuni.
Mke wa Rais Barack Obama wa Marekani, Michelle Obama na binti zake Sasha na Malia ataongoza ujumbe wa Marekani. Haijulikani kama Obama mwenyewe atafika.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel atakuwa mmoja wa wageni maarufu kwenye uwanja wenye uwezo wa kuchukua watu 80,000. Wengine ni Waziri Mkuu wa Urusi, Dmitry Medvedev na Waziri Mkuu wa Japan, Yoshihiko Noda.
Mfalme Mswati III wa Swaziland anatarajia kuwapo, walau na mmoja kati ya wake zake 13. Mawaziri wakuu wote walio hai wa Uingereza ambao wamealikwa pia. Sir John Major na Tony Blair wamethibitisha kushiriki.
Wadau wa soka wa Australia wamechukizwa na uamuzi wa Waziri Mkuu wao, Julia Gillard wa kutohudhuria.
Wengine watakaopamba sherehe hiyo kama wageni rasmi ni wanafamilia ya kifalme ya Uingereza
Majina mengine makubwa ya walioalikwa ni akina Brad Pitt, Angelina Jolie na David Beckham mwaka 2005 alikuwa kati ya mabalozi wa Uingereza waliotoa ushawishi ili nchi iandae michuano hii.
Wengine ni Dames Helen Mirren na Judi Dench.
Kati ya viongozi wa nchi na serikali wanaotarajiwa kuhudhuria, ni marais, wafalme, malkia, masheikh 82 waliokwenda Beijing kwa michezo ya mwaka 2008 na 48 waliosafiri hadi Athens kwa mashindano kama hayo mwaka 2004.
Ulinzi kumzunguka kila mkuu wa nchi utakuwa mkali, ukijumuisha wapambe na polisi.
Askari wa kikosi maalumu cha Scotland Yard kinacholinda wanadiplomasia watatoa ulinzi wa jumla, wakiwa kwenye rangi zao nyekundu, wakiwasindikiza kwenda na kurudi uwanjani.
Sherehe hizo za ufunguzi zinatarajiwa kuanza saa tatu usiku na kumalizika usiku wa manane. Gharama yake ni Pauni milioni 27.
 [email protected]

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Usain Bolt aingia Olimpiki kwa unyonge

Siri ya Dany Boyle na wasanii 15,000 yafichuka- Ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki 2012 LONDON