in , ,

Viongozi wana kiburi, Zahera ana jeuri, Wachezaji hawajui cha kufanya

Miaka zaidi ya 80. Ndiyo umri halisi wa Yanga. Umri ambao ni mkubwa sana. Umri ambao wasingetakiwa kuwepo hapo walipo kwa sasa.

Hili tumeshaliongea sana, tumelipigia kelele sana na inawezekana lishaanza kuonekana la kawaida katika masikio ya walio wengi.

Hasa hasa wanaopewa dhamana kuiongoza klabu ya Yanga. Pamba ngumu zimezunguka ngoma za masikio yao.

Tongongo nzito zimeziba mboni za macho yao. Hawaoni vizuri na hawasikii vizuri, kinachofanyika ni wao kukanyaga bila kujua ni wapi wanapopakanyaga.

Na kuna wakati mwingine wanakimbia sana, tena kwa kasi kubwa bila mwelekeo wowote ule. Kwa kifupi malengo hayajawa kama nguzo ya kila anayepewa dhamana ndani ya Yanga.

Miaka 80 Yanga imeongozwa bila malengo ya kuifanya imara. Imeongozwa ili kuhakikisha ipo tu ndani ya ligi kuu na inashindana na Simba.

Hapa ndipo mwanzo na mwisho wa ujinga wa viongozi wa Yanga ulipo. Ndiyo maana kwa umri walionao ni tofauti kabisa na utajiri walionao.

Siyo umri tu, hata rasilimali walizonazo ni tofauti kabisa na utajiri walionao. Yanga ilitakiwa kubwa klabu kubwa sana.

Najua kwa sasa watu wengi wanadai Yanga ni klabu kubwa. Hapana shaka wanajifariji kwenye hili na huwa kama egemeo kwao kwa ajili ya kujipatia faraja.

Yanga haina ukubwa wowote ila ina umaarufu mkubwa. Umaarufu ambao unaweza kuisaidia kuwa klabu kubwa Afrika.

Lakini cha kusikitisha kila anayepewa dhamana ya kuiongoza Yanga hajawahi kufikiria namna ya kuufanya umaarufu wa Yanga kuwa wenye faida.

Namna ya kuitengeneza Yanga imara kupitia umaarufu wa Yanga. Hakuna aliyewahi kufikiria hivo.

Na siyo kwamba hawaelezwi namna ya kuifanya Yanga iwe kubwa, huwa wanaimbiwa sana. Na huwa tunaandika sana makala zetu kuwakumbusha tu namna ya kuifanya Yanga kuwa kubwa.

Lakini hakuna ambaye amewahi kulielewa hili somo. Hakuna kabisa. Na cha kusikitisha wengi wanaopita pale hunufaika zaidi kuliko Yanga inavyonufaika.

Ndipo hapo unaweza kujiuliza maswali mengi yasiyo kuwa na majibu sahihi. Kipi kinawasababisha wasisikie maoni yetu?

Kipi kinachosababisha wao kama viongozi kwa miaka zaidi ya 80 wasiwaze kuifanya Yanga kuwa kubwa pamoja na mtaji mkubwa wa watu ?

Kiburi?, bila shaka hili linaweza kuwa jibu sahihi. Wengi wa viongozi waliopita Yanga walikuwa na kiburi. Kiburi ambacho kiliwafanya wazibe masikio na macho yao.

Hawakutaka kusikiliza ushauri wowote wa kujenga au kutazama mifano bora ya uendeshwaji wa klabu kisasa. Wakabaki kuamini kupitia njia zao.

Njia ambazo hazina manufaa makubwa katika dunia ya sasa. Njia ambazo zimewafanya mpaka sasa hivi kuwa klabu masikini hapa nchini.

Tena masikini wa kutupwa kabisa, kapuku tena kapuku mkubwa. Masikini asiyeweza kusimama yeye kama yeye.

Ndiyo maana siyo jambo la kushangaza kusikia wachezaji wa Yanga wanaɗai mishahara ya miezi hata minne. Siyo jambo la kushangaza kabisa.

Hii yote ni kwa sababu wameshirikia kiburi ndani ya uongozi wao. Hawataki kufungua akili ndani ya miaka 80 ili kuifanya Yanga isimame yenyewe.

Leo hii wachezaji wa Yanga wanagomea mazoezi kisa mshahara. Na cha kusikitisha wamekutana na kocha mwenye jeuri.

Wakati wachezaji wa Yanga wakiwa wanapigania haki yao ya msingi, Mwinyi Zahera anaingiza kiburi ndani yao.

Hataki kusikia neno kugoma, hataki kuelewa kuwa wachezaji wana haki yao ƙubwa ya msingi. Hawa wachezaji wana familia ambazo huwategeme kupitia kuichezea Yanga.

Hivo ni haki yao ya msingi kabisa kudai kitu ambacho kinawafanya watokwe jasho ndani ya dakika 90 za mchezo wakiipigania Yanga.

Kitendo cha Mwinyi Zahera kudai kuwa ambaye hatofanya mazoezi hatocheza kwenye mechi za ligi kuu zilizobakia. Hii ni jeuri kubwa ya baba kwa mtoto.

Mwinyi Zahera anatakiwa asimame kama baba wa hawa watoto. Ahakikishe wanapata haki yao ya msingi.

Leo hii akiwalazimisha wacheze hivo hivo na njaa kesho kwenye mechi hawatofanya vizuri. Ndipo hapo unabaki kuwahurumia wachezaji wa Yanga wanavyokuwa katika njia panda.

Hawajui cha kufanya, viongozi wao wana kiburi, hawataki kuelewa , kusikia na kuona jinsi ya kuifanya Yanga kuwa bora na kocha wao ana jeuri haswaaa

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Wachezaji Sita ambao hawatakiwi kucheza Manchester United

Tanzania Sports

Katikati ya furaha ndiko kulikuwa mwisho wa Alexis Sánchez