in , ,

Vijana wa Madiba wafunika AFCON

*Morocco wazuia Cape Verde kuweka historia

 
Baada ya kuwaacha roho juu wananchi kwa kutoka suluhu na Cape Verde mechi ya kwanza, Afrika Kusini wamesafisha nyota kwa kuwafunga Angola mabao 2-0.
Hayo yalikuwa pia mabao ya kwanza kwa timu zote nne za kundi ‘A’ katika Michezo ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON.
Matokeo hayo yamewaacha wenyeji wakijawa furaha, na kuwa na matumaini makubwa kwamba sasa timu yao itaingia hatua inayofuata.
Katika uwanja wa Moses Mabhida jijini Durban, Bafana Bafana walipata bao la kwanza kutoka kwa asiyetarajiwa – beki wa kati, Siyabonga Sangweni dakika ya 30, na walitawala sehemu kubwa ya mchezo, lakini wakapoteza nafasi nyingi za wazi.
Angola wanaojulikana kwa soka ya nguvu siku hizi, walikosakosa pia nafasi za kufunga, kupitia kwa mchezaji wao mahiri, Alberto Manucho.
Alikuwa ni Lehlohonolo Majoro aliyeingia kipindi cha pili, aliyewainua vitini washabiki kwa mara ya pili katika dakika ya 62, na kuiweka Bafana Bafana nafasi ya kwanza katika kundi hilo.
Timu zote zilianza kwa kusomana mchezo, ikadhaniwa ingekuwa kama siku ya kwanza, ambapo hadi timu zote za kundi A zilikuwa zimeishia kwa suluhu, pointi moja, bila goli la kufunga wala kufungwa.
Pamoja na uzuri wa Angola, ni wazi kwamba shinikizo lilikuwa kwa wenyeji zaidi, kuwapa raha wananchi, ili watuzwe kwa kucheza kwao, isiwe kama kwenye kombe la dunia walipoandaa na kutoka hatua ya mwanzo kabisa.
Angola walishaanza kuonekana kujipanga vyema kurudisha bao la kwanza, lakini aina ya bao la pili liliwaanika Waangola kwamba hawakuwa makini vya kutosha.
Mfungaji alikokota mpira toka mbali, akawapiga chenga mabeki, akasogea karibu na upande wa kona na kurudi kujongea golini kabla ya kupiga mpira na kumpiga tobo golikipa Luís Mamona João ‘Lama’
Itabidi wachezaji wa Angola, Manucho, Guilherme Afonso na Jose Pirolito wajilaumu wenyewe kwa jinsi walivyotumia vibaya nafasi za kufunga walizopata.
Katika mechi ya pili, nusura wazoefu Morocco wazamishwe na chipukizi wa visiwa vya Cape Verde, kwani chipukizi Platini (Luís Carlos Almada Soares) alimtungua golikipa Nadir Lamyaghri kwa bao la dakika ya 35.
Morocco walihangaika kurejesha udhibiti wa mchezo, na ilifika mahali wakawa kama wamekata tamaa.
Hilo lilikuwa bao la kwanza katika historia kwenye mashindano ya AFCON, na kama kuna kitu walikiwaza zaidi pale Afrika Kusini na waliokuwa nyumbani ni ushindi.
Hiyo ni kwa sababu Cape Verde walifanikiwa kuwazuia Morocco kupata bao kwa muda mrefu, lakini waliponzwa na ama kuishiwa pumzi au kupendelea mchezo wa kujihami zaidi.
Ndiyo maana robo ya mwisho ya kipindi cha pili mipira ilikuwa zaidi langoni mwa Cape Verde, na haikuwa ajabu sana kwa wajuzi wa soka kuona Morocco wakipachika bao dakika 12 kabla ya mpira kumalizika.
Mfungaji alikuwa Youssef El-Arabi aliyeingia uwanjani dakika ya 46, ambapo alifunga kwa kusukumiza wavuni kwa nguvu mpira wa kuchonga wa Abdelaziz Barrada.
Simba wa Milima ya Atlas walipewa nafasi kubwa kufanya vyema, ikizingatiwa uzoefu wake wa muda mrefu kwenye mashindano haya na mengine.
Cape Verde au Papa wa Bluu wanaofundishwa na Lucio Antunes ndiyo nchi ndogo zaidi kijiografia kushiriki AFCON.
“Bado tungali hai, nimefurahishwa sana na matokeo haya, ni heshima kubwa kwa taifa letu,” akasema kocha Antunes.
Morocco walijikuta wakicheza ama kwa hasira au kwa kuchanganyikiwa baada ya kufungwa bao, wakaishia kuadhibiwa kwa mipira mingi ya adhabu katika eneo lao la hatari, watashukuru kutofungwa zaidi ya bao hilo.
Kocha wa Morocco, Rachid Taoussi anasema hawakuwabeza wapinzani wao kutokana na ugeni, bali walikuwa wakiwasoma na kujaribu kuendana na mchezo wao ili hatimaye waweze kuwapenya na kufunga.
Kwa matokeo ya Jumatano, Afrika Kusini wanaongoza kundi A kwa pointi nne, wakifuatiwa na Cape Verde na Morocco wenye pointi mbili kila moja na mkiani wameketi Angola wenye pointi moja tu.
Alhamisi hii ni mechi kati ya Nyota Nyeusi wa Ghana dhidi ya Tai wa Mali. Mechi ya pili ni kati ya Swala wa Niger na Chui wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Toure, Gervinho waibeba Ivory Coast

Kombe la ligi laiponyoka Chelsea