in , , ,

VAN GAAL BADO ANATENGENEZA TIMU

 

Misimu miwili imepita tangu Manchester United walipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu England kwa mara ya mwisho. Walitwaa ubingwa kwa mara ya mwisho wakiwa chini ya Sir Alex kwenye msimu wa 2012/13. Misimu miwili iliyofuata wakawashuhudia Manchester City halafu Chelsea wakitwaa ubingwa wa ligi hiyo.

Washabiki wa timu hiyo hawapo tayari kuishuhudia timu yao ikikosa ubingwa wa EPL kwa mara ya tatu mfululizo msimu huu. Wana shaku ya hali ya juu ya kutwaa ubingwa wa EPL msimu huu.

Agosti mwaka jana kocha mkuu wa timu hiyo Louis Van Gaal alinukuliwa akisema kuwa alitarajia kutwaa ubingwa wa EPL kwenye msimu wake wa pili akiwa na timu hiyo na huu ndio huo msimu wa pili.

Kwa kiasi fulani amefanya maandalizi kwa ajili ya malengo yake hayo. Amefanikiwa kuwaleta wachezaji wapya kadhaa kwa ajili ya mapambano. Amewaleta Memphis Depay, Morgan Schneiderlin, Bastian Schweinsteiger na Matteo Darmian.

Hapo juzi pia, siku ya mwisho ya dirisha la usajili kocha huyo alitoa kitita cha paundi milioni 36 na kumtwaa Anthony Martial wa miaka 19 kutoka AS Monaco ya Ufaransa.

Lakini kwa upande wangu sidhani kama kikosi cha Van Gaal kimekamilika kwa ajili ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu. Sidhani kama ni kikosi kinachotosha kupambana na makali ya Manchester City ambao ndio nafikiri wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu kutokana na uimara wa kikosi chao.

Tatizo ninaloliona kwenye kikosi cha Manchester United ni lile lile ambalo niliwahi kulizungumza kwenye moja ya makala zangu za nyuma. Tatizo ni mpachika mabao. United inahitaji mshambuliaji mwenye kiwango cha kushindania tuzo ya mfungaji bora ili iweze kutwaa ubingwa. Sidhani kama Martial ameshafikia kiwango hicho kwa sasa.

Anthony Martial bado ana mengi ya kujifunza. Bado anahitaji muda wa kutosha ili awe mchezaji wa kiwango cha kutegemewa na timu kubwa kama United katika kuifungia mabao ya kutosha kwenye mechi ngumu na rahisi. Kwa sasa hawezi kuwa suluhisho la kiu ya mataji Old Trafford.

Martial anatarajiwa kupewa nafasi ya kusimama mbele ya Wayne Rooney kwenye mfumo wa Manchester United na kutengeneza safu tegemeo ya kupachika mabao. Cha ajabu nahodha huyo wa Manchester United hakuwa amewahi kumsikia Martial mbaka hapo juzi alipokuwa katika hatua za mwisho za kusajiliwa.

Hii inaonyesha ni kiasi gani mchezaji huyo bado yupo katika hatua za kujiendeleza kiuwezo. Ana safari ndefu kidogo kuwa mchezaji kamili na tegemeo wa timu kama Manchester United. Kwa sasa hawezi kukata kiu ya washabiki wa Manchester United.

Nafikiri hata Luis Van Gaal ana mawazo kama haya ya kwangu. Hapo juzi alinukuliwa akisema, “Anthony ni mshambuliaji kinda aliyejaliwa kipaji. Naamini United ndiyo klabu ambayo itaweza kumuendeleza.”

Van Gaal anakusudia kuendeleza kipaji cha mshambuliaji Martial ambaye amemsajili kwa dau lililovunja rekodi kwa wachezaji wa chini ya miaka 20 waliosajiliwa kwa madau makubwa zaidi.

Nadhani  kocha huyu anasahau kuwa msimu huu lengo lake ni kutwaa ubingwa wa EPL na kwamba kutwaa ubingwa huo kunahitaji mpachika mabao aliyekomaa na kuwa mchezaji kamili. Ingawa kipaji cha Martial si cha kubeza lakini bado hajawa mchezaji wa kutegemewa na United kwa sasa.

Nafikiri mwalimu Louis van Gaal bado anatengeneza timu yake. Anajiandaa kwa ajili ya kutwaa ubingwa wa EPL mbeleni ila si msimu huu.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Ni lawama tu

Arsenal walimkataa Cavani