in , , ,

UWEZO WA BARCA WA KUMALIZIA NAFASI NDICHO KILICHOIUA ARSENAL

Asilimia kubwa ya washabiki wa soka walitarajia kuwa Arsenal wangepoteza mchezo wa jana Jumatano dhidi ya FC Barcelona kule Hispania. Hakuna aliyeshangazwa na ushindi wa 3-1 wa Barcelona.

Lakini pengine ni wachache mno waliotarajia kuwa Arsenal wangeweza kupiga mashuti mengi zaidi ya Barcelona kwenye mchezo ule. Ila ndivyo ilivyokuwa, Arsenal walipiga mashuti 21 dhidi ya 17 ya Barcelona.

Hii ni tofauti mno na mchezo wa kwanza uliopigwa kule Emirates ambapo Arsenal walipiga mashuti 8 pekee huku Barcelona wakiwa na mara mbili ya idadi hiyo.

Pia haikutarajiwa kuwa Arsenal wangeweza kupata angalau asilimia 40 za umiliki wa mpira kwenye mchezo huo wa Jumatano. Lakini waliweza kumiliki mpira kwa asilimia 43 dhidi ya 57 za wenyeji.

Kipengele hiki cha takwimu pia kinatofautiana na mchezo wa kwanza ambapo Arsenal wakiwa nyumbani walikuwa na asilimia 32 tu za umiliki wa mpira huku Barcelona wakitawala kwa asilimia 68.

Arsenal walipata pia kona 8 kwenye mchezo wa jana Jumatano huku Barcelona wakipata kona 7 pekee ndani ya Nou Camp.
Kwenye mchezo wa kwanza vijana wa Arsene Wenger walifanikiwa kupata kona 1 pekee kwenye dakika zote 90 za mchezo huku Barcelona wakipiga kona 7.

Takwimu hizi zinatulazimisha kukubali kuwa Arsenal hawakuachwa nyuma kimbinu na Barcelona kwenye mchezo wa Jumatano ndani ya Nou Camp.

Timu inapopiga mashuti 21 dhidi ya Barcelona ndani ya Nou Camp haiwezi kusemwa kuwa ilizidiwa mno kimchezo hata kama itafungwa zaidi ya mabao mawili.

Hata miongoni mwa timu zilizofanikiwa kuifunga Barcelona msimu huu, hakuna iliyoweza kupiga mashuti 21 kwenye michezo husika.

Athletic Bilbao waliowafunga Barcelona 4-0 Agosti mwaka jana kwenye mchezo wa “Spanish Super Cup’ ndani ya dimba la San Mames walisajili mashuti 11 pekee.

Celta Vigo waliowaadhibu Barcelona 4-1 Septemba mwaka jana ndani ya Balaidos kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Hispania walipata mashuti 18.

Sevilla ambao waliibuka na ushindi wa 2-1 Oktoba mwaka jana dhidi ya Barcelona kwenye dimba la Ramon Sanchez Pizjuan waliweza kupiga jumla ya mashuti 13 tu kwenye dakika zote za mchezo.

Lakini Arsenal walipiga idadi ya mashuti 21 ndani ya dimba la Nou Camp hapo jana Jumatano.

Pia asilimia 43 za umiliki wa mpira walizopata Arsenal kwenye mchezo wa jana ni nyingi zaidi ya zile walizopata Bilbao na Celta dhidi ya Barcelona zilipoifunga timu hiyo.

Bilbao walikuwa na asilimia 26 pekee za umiliki wa mpira kwenye ushindi wao wa 4-0 dhidi ya Barcelona huku Celta wakiwa na asilimia 40 kwenye ushindi wao wa 4-1 dhidi ya mabingwa hao wa Ulaya.

Sasa kama Washika Bunduki walifanikiwa kudhibiti makali ya kimbinu ya vijana wa Luis Enrique, nini kilichofanya wapoteze mchezo ule kwa kwa 3-1?

Jibu la swali hilo ni rahisi mno. Ni uwezo uliopitiliza wa Barcelona wa kumalizia nafasi za kufunga. Nafasi zilizotumiwa na Neymar, Suarez na Messi kufunga mabao matatu kwenye mchezo huo hazikuwa nafasi rahisi.

Ukilitazama bao la Neymar kwenye dakika ya 18, mshambuliaji huyo alikuwa na utulivu wa hali ya juu na kafanikiwa kufunga kiufundi licha ya Bellerin kumgasi kwa kasi akitokea nyuma na golikipa kuonekana kumbana vizuri.

Goli la Suarez alilofunga ndani ya dakika ya 65 ni la uwezo zaidi. Isingemshangaza yeyote iwapo mshambuliaji yeyote wa daraja la dunia angeshindwa kutumia nafasi ile kufunga.

Messi naye alionyesha maajabu yake tuliyoyazoea kwenye dakika za majeruhi. Aliuinua mpira kiufundi licha ya kukabiliwa kwa ukaribu na Ospina. Mpira ukainuka vyema kuelekea wavuni na kumuacha golikipa huyo akikosa la kufanya.

Hivyo ingawa Arsenal waliyazima makali ya kimbinu ya Barcelona kwenye mchezo wa jana, uwezo wa ajabu wa washambulizi wa Barca wa kumalizia nafasi za kufunga uliwaua Arsenal.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

HAYA YANAWEZA KUWAFANYA ARSENAL WAWASHANGAZE BARCA

Tanzania Sports

Pep Guardiola ni mbunifu au mvurugaji vipaji?