in , ,

UWEPO WA OLUNGA GIRONA NI MATUSI KWA KINA AJIB

Mida ya usiku jana, usiku uliokuwa tulivu baada ya idadi nyingi za
mechi kuchezwa kuanzia mchana,ikawa imebaki mechi moja tu.

Mechi ambayo ilitupa uhuru wa kuiiangalia bughudha kwa sababu ilikuwa peke yake.

Hivo tulikuwa na uhuru wa kuiangalia vizuri mechi hiyo, mechi ambayo
ilikuwa inamjumuisha mchezaji bora na mwenye kipaji cha juu duniani
Messi.

Mchezaji ambaye macho yangu hayajuti kumshuhudia katika maisha yangu
ya soka, na ni moja ya hadithi nzuri nitakazokuwa nawasimulia wajukuu
zangu.

Kwangu mimi jana Messi hakuwa habari kubwa kwa sababu ni mtu ambaye
nishazoea kumuona kila mwisho wa juma.

Habari kubwa kwangu na yenye faraja ni kumuona Olunga akiwa anapambana
na kina Messi.

Olunga akiwa anakabwa na kina Mascherano, Olunga ambaye ni mwana
Afrika Mashariki mwenzangu.

Mtu ambaye aliwahi kukanyaga ardhi ya Tanzania katika mashindano ya
mapinduzi Zanzibar mwaka 2013, katika fainali ya kombe hilo dhidi ya
Azam FC ambapo timu yake ya Tusker FC ilifungwa goli 2-1.

Toka mwaka 2013 mpaka sasa ni miaka minne (4), miaka minne (4) yenye
maendeleo makubwa kwake na maendeleo hafifu kwa wachezaji wetu wa
Tanzania.

Hakuna Mtanzania hata mmoja aliyecheza ile fainali ya mapinduzi ya
Zanzibar ya mwaka 2013 aliyedhubutu kwenda nje kucheza.

Lakini leo hii Olunga , ambaye tena aliingia kipindi cha pili akitokea
benchi , leo yupo katika ligi kubwa barani ulaya.

Ligi ambayo ina wachezaji wenye vipaji vikubwa na soka safi.

Leo hii anakabana na Messi, mtu ambaye kila mtu anatamani siku moja
angalau apige naye picha.

Lakini kwetu sisi hakuna hata aliyeweza kwenda hata kupiga picha naye.
Na haya ndiyo matokeo ya kila unachokipigania katika maisha.

Unachokipigani ndicho utakachopata, yeye alipanga na alipigania kwenda
kucheza mbali ndiyo maana hata alipotaka kuchukuliwa na vilabu vyetu
vya Tanzania alikataa.

Alikuwa na watu waliokuwa wasimamizi wazuri wa vipaji, watu ambao
walitaka kuona kipaji chake kinafika mbali kwa manufaa yake binafsi.

Yeye pia hakuwaangusha wasimamizi wake, alipigania kipaji chake vizuri
mpaka pale alipoamua kwenda kudhubutu kucheza Sweden, njia ambayo
ilimpa nafasi kwenda China, sehemu pekee ambayo ilimpa upenyo wa yeye
kupelekwa kwa mkopo Ginora .

Ni hatua kubwa sana katika mafanikio yake binafsi na nchi yake kwa
ujumla. Tunazidi kuona idadi wengi ya Wakenya wakidhubutu na kwenda
kucheza nje ya nchi.

Tena katika ligi ambazo zina ushindani. Wanyama yupo ligi kuu ya
England, Olunga yupo katika ligi kuu ya Hispania.

Hii yote inaonesha ongezeko la wachezaji wa timu ya taifa ya Kenya
kwenye ligi kubwa inaongezeka.

Na hii ni kutokana na wachezaji wenyewe kujituma, kuikana nafsi yao na
kudhubutu kwenda sehemu kujaribu bahati zao.

Hawakuona umuhimu wa wao kuendelea kucheza katika ligi ya kwao au ya
nchi jirani kwa sababu hakuna kitu kikubwa ambacho wangenufaika nacho.

Waliyakana na kuyakataa magari waliyopewa na timu zao za nyumbani kwa
kuamini kuwa ipo sehemu ambayo kwao wao itawanufaisha zaidi ya hivo
vitu vidogo.

Walividhamini vipaji vyao na kuamini kuwa wanaweza kucheza ligi kubwa
duniani na kuacha kuhangaika na ligi ambazo zimejaa zengwe.

Leo hii ni Watanzania wangapi ambao wanaudhubutu wa kwenda kucheza nje
na kuzikana nafsi zao?

Nchi hii inawachezaji wenye vipaji vya hali ya juu lakini vipaji
ambavyo havijielewi na havina wasimamizi pamoja na washauri wazuri.

Ndiyo maana unakuta mchezaji anacheza bila malengo makubwa, maono yake
yanakuwa mafupi

Muda wa kutazama mbali hana, yeye anachoangalia ni mahali alipo
akiamini ndipo mahali panapomfaa na patakapo mfanya awe mkubwa.

Hafikirii taifa lake linatakiwa kujivunia kuhusu yeye, hafikiri timu
ya taifa inatakiwa iwe na wachezaji wakubwa kutoka ligi kubwa ambao
watasaidia kuamua matokeo ya timu ya taifa.

Kuendeleza kukidumaza kipaji chako nchini ni mwanzo wa kudumaza
maendeleo ya mpira nchini.

Hili tusi la Olunga kwetu tunatakiwa tulitumie kama silaha ya sisi
kudhubutu kuingia vitani kupigania mafanikio.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

NEYMAR UFALME HAUJENGWI SIKU MOJA

Tanzania Sports

NIMEIKUMBUKA MBEYA CITY KAMA NILIVYOMKUMBUKA DR.SLAA