in

Ushindi umebadili kila kitu kwa Newcastle

Newcastle United

Unaposhuhudia timu yako inashinda mara nyingi inaleta hisia nzuri hasa ukizingatia ushindi wenyewe ulistahili kutokana na kiwango na uwezo. Hilo ndilo linalotokea na hakika ushindi hakikuwa kitu kilichozoeleka kwa mashabiki wa Newcastle United. Sasa wanaweza kushangilia zaidi.

Newcastle United imepata ushindi wa kwanza baada ya kucheza mechi 11 mfululizo ikiandamwa na ukame. Mara ya mwisho kupata ushindi ilikuwa Desemba 12 mwaka 2020 dhidi ya West Bromwich Albion. Lakini unaweza kurudi nyuma zaidi kuona ushindi wao wa mabao 3-1 dhidi ya  Burnley waliopata Oktoba 3 mwaka huo huo na kusema walistahili kupata pointi tatu.

Kocha mkuu Steve Bruce alihitaji ushindi kupunguza presha ya kutimuliwa. Muhimu zaidi, Newcastle United walihitaji ushindi huo ili kushusha presha ya mashabiki, angalau kuwaonesha kuondoka katika hatari ya timu zinazoweza kushuka daraja msimu huu.

Kuondoa kivuli cha kushuka daraja walitakiwa kucheza kwa kiwango cha juu na kuibuka na ushindi, ndicho kilichotokea Newcastle walionesha uwezo wa hali ya juu katika mchezo wote kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Wakati mwingine katika mechi zao, Newcastle wamewahi kuonesha kiwango kibovu cha uchezaji, lakini angalau walimaliza mchezo wakiwa wamepata pointi tatu muhimu kwao na kwa mashabiki wao.

Kwenye mchezo dhidi ya Everton walicheza mchezo mzuri na kupata ushindi usio na mashaka yoyote. Hakikuwa kiwango kilichoonekana kwa muda mrefu lakini bila shaka mashabiki wamekaribisha kwa furaha.

Changamoto iliyopo sasa kwa kocha Steve Bruce na timu yake ni kurudia kucheza kwa kiwango kizuri katika mechi zingine na kuibuka na pointi tatu siku zijazo. Pengine mchezo wao dhidi ya Everton ndio ambao wamecheza kwa kiwango bora kabisa kuliko mechi zote msimu huu.

Graeme Jones jinsi alivyotoa mchango kwenye mchezo huo ni jambo linaloleta mjadala mkubwa. Kocha huyo msaidizi amewafanya Newcastle United wacheze kwa utulivu na wameonesha mambo mapya waliyonolewa mazoezini. Ameonesha kuwa thabiti na mwelekeo wa kusaidia Newcastle United na ushindi wao kwenye dimba la Goodison Park unajieleza bayana.

Hata hivyo kumsifia Graeme Jones isichukuliwe kama kupora sifa za kocha mkuu Steve Bruce. Naye apewe sifa zake kutokana na mabadiliko ya Newcastle United.

Kwa muda mrefu Steve Bruce amekosolewa kwa kushindwa kuipa ushindi Newcastle na kushuhudia vipigo mbalimbali. Kipigo cha kukumbukwa ni hivi karibuni ni cha bao 1-0 kutoka kwa Sheffield United. Baada ya kipigo hicho, kocha huyo aliamua kubadili mambo kuelekea mchezo wao dhidi ya Everton, na ambayo yalimpa ushindi.

Wachezaji waliokosa kasi na uimara wa miili sasa walionekana kuwa thabiti zaidi. Kabla ya mchezo huo kupitia kikao walichofanya na baadhi ya wachezaji waandamizi wa Newcastle waliamua kwa kauli moja kuwa wanatakiwa kubadili hali ya mambo klabuni hapo na kuleta utulivu. Wachezaji walitakiwa kuonesha uthubutu na moyo wa kupambana ili kutengeneza mwelekeo wa Newcastle United.

Mfumo wa 4-3-3 ulichangia uwiano mzuri katika timu. Kupanga washambuliaji watatu ulihakikisha Callum Wilson ana wasaidizi zaidi kwenye mashambulizi.

Ryan Fraser alicheza upande wa kushoto na Miguel Almiron alicheza nyuma ya mshambuliaji wao Callum Wilson na kumruhusu Mparaguay huyo kucheza kuanzia nyuma zaidi na kuunganisha kazi za viungo  washambuliaji. Matokeo yake Callum Wilson alipata uhuru na kuwezesha Newcastle kumiliki mpira na kudhibiti presha kutoka kwa wapinzani wao.

Takwimu zinaonesha asilimia 55.5 ya mashambulizi ya Newcastle United yalianzia upande wao wa kulia ambako Wilson alikuwa anapata usaidizi wa Almiron.

Mbali ya mabao mawili ya Wilson, ambapo moja alifunga kwa kichwa na lingine akimalizia kazi nzuri ya wachezaji wenzake, kabla ya mchezo wa Everton alionekana kama hana msaada katika mechi kadhaa zilizopita.

Kwenye mchezo dhidi ya Everton aligusa mpira mata 56 ikiwa ni wastani wa 30.3 na 28 akiwa Villa. Pia alipiga mashuti 6 lango la adui, ambapo matatu yalilenga langoni, wakati kwa Aston Villa alikuwa na wastani wa 0.8. Mashuti mengine 8 alikuwa kwenye boksi ambayo ni sawa na wastani wa 4.1 akiwa Villa.

Takwimu zote hizo zinaonesha namna Wilson alivyobadilika katika mechi moja msimu huu na zinaweza kuelezea namna anavyofurahia kila mechi anayocheza Newcastle, ingawa alisikitika kutofunga mabao matatu kwenye mchezo huo.

Wilson amekabidhiwa jukumu la kuhakikisha Newcastle hawashuki daraja msimu huu, amefunga asilimia 47.6 ya mabao ya timu hiyo. Ametengeneza asilimia 67 ya mabao 21 yaliyofungwa na Newcastle United, lakini kwa mara ya kwanza alicheza kwa ushirikiano wa karibu kimbinu kwenye mchezo wao na Everton baada ya kupangwa washambuliaji watatu mbele.

Akiwa na Almiron inamsaidia kuwa na uhakika wa kupokea pasi za kufunga mabao mara kwa mara, huku Jeff Hendrick na Jonjo Shelvey wakiongoza jahazi la kudhibiti eneo la kiungo.

Kwa mfano Jonjo alihusika kutengeneza bao la kuongoza la kwanza la Newcastle msimu huu ambalo lililofungwa na Wilson. Katika msimu wa 2019/2020 Jonjo alifunga mabao 6 na kutengeneza mawili.

Kutumia wachezaji watano kudhibiti kiungo na kuungana na safu ya  ushambuliaji kwenye kipindi cha kwanza dhidi ya Everton kiliwapoteza kabisa vijana wa Carlo Ancelotti na kusababisha wafanye makosa mengi yaliyoruhusu Newcastle kupata mabao. Walifanya hivyo baada ya Isaac Hayden kurudi katika nafasi yake ya asili mchezoni kuliko kutumika nafasi ya beki wa kati au beki wa pembeni. Hayden alionesha vitu adimu kwenye kiungo na kuwadhibiti Everton, kuvuruga mipango yao mara mbili, kuondoa hatari mara tano na kuipa uhai Newcastle kwenye umiliki wa mpira mara nne.  

Bruce amekuwa akikosolewa mara kwa mara lakini mlipuko wa ugonjwa wa corona na majeraha ya mara kwa mara kwa wachezaji wake yamekwamisha juhudi za kupaisha Newcastle. Kuwakosa wachezaji wake wazuri kunamgharimu lakini hakuna anayeangalia hilo zaidi ya matokeo mabovu aliyokuwa anayapata.

Sasa ameleta mabadiliko na timu imeonesha kiwango kizuri dhidi Everton, ikiwa na maana anafanikiwa kurekebisha mambo klabuni hapo. Lakini mwisho wa msimu matokeo yatazungumza zaidi. 

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
SSC

Simba hawajapata hasara kwenye Simba Super Cup

Luis Suarez

Atletico Madrid timu ya ‘wazee’