in

Usajili wa Yanga unafanywa na kocha yupi?

Dar young africans

Naikumbuka sana ile siku ya mechi kati ya Yanga na Namungo FC kwenye uwanja wa Taifa.ย  Naikumbuka kwa vingi sana. Naikumbuka kwa sababu ndiyo mechi ambayo niliona beki wa Namungo FC akifunga magoli mawili peke yake dhidi ya Yanga.

Suala kubwa hapa siyo kwa beki huyo kufunga, suala kubwa lilikuwa ni namna gani ambavyo safu ya ulinzi ya klabu ya Yanga ilivyokuwa mbovu, ilikuwa inawakaribisha Namungo FC kwa kuwatengenezea uwazi ambao ulikuwa rahisi kwa Namungo FC kuwaadhibu Yanga.

Naikumbuka sana hii mechi kwa sababu ndiyo mechi ambayo Yanga iliwabidi watoke nyuma ya magoli mawili na kuyarudisha kisha mechi ikaisha kwa sare ya magoli 2-2. Kilikuwa kitu kinachoumiza kuona timu kubwa kama Yanga ikiwa kwenye uwanja wa Mkapa ikihangaika dhidi ya Namungo FC.

Inauma kwa sababu Yanga ni moja ya timu kubwa hapa nchini na ilikuwa inacheza na moja ya timu ndogo hapa nchini, timu ambayo ndiyo ni mara ya kwanza kupanda ligi kuu kibaya zaidi Yanga ilikuwa ikihangaika kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Naikumbuka hii mechi kwa sababu mtakatifu Lucas Kikoti aliwafunika kina Haruna Niyonzima , Faisal Salum “Fei Toto” pale katikati ya uwanja. Ilikuwa ngumu kwao wao kutengeneza nafasi za kufunga kwa kina Ditram Nchimbi. 

Tanzania Sports
Yanga Vs Simba

Kitendo cha viungo wa Yanga kutotengeneza nafasi za kutosha kwa washambuliaji wao kilikuwa siyo kitendo cha kwanza kwenye mechi hii dhidi ya Namungo FC. Kwenye ligi hii iliyoisha hakuna kiungo wa kati wa Yanga aliyetoa pasi hata tatu za magoli. Hakuna kiungo wa Yanga ambaye alifunga hata goli tano msimu huu.

Wakati nikitazama viungo wa Yanga wakiwa wanahangaika kutengeneza nafasi za kufunga macho yangu yalikuwa yanamtazama mtakatifu Lucas Kikoti ambaye alikuwa mpishi mkuu kwenye mechi hii na aliwazidi sana viungo wa klabu ya Yanga.

Naikumbuka hii mechi kwa sababu ndiyo mechi ambayo ilitoa picha namna ambavyo Yanga wanatakiwa kusajili kiungo ambaye anauwezo wa kufunga akitokea katikati ya uwanja huku akitengeneza nafasi za kufunga kwa washambuliaji wake. 

Naikumbuka hii mechi kwa sababu ya kiwango kikubwa cha Hashim Manyanya. Kiungo wa pembeni wa Namungo FC. Kiungo ambaye aliwatesa sana Yanga kutokana na kasi yake , kujituma kwake pamoja na ufanisi mkubwa wakati akiwa na mpira mguuni. Alikuwa anatengeneza nafasi nyingi siku hii.

Wakati namtazama Hashim Manyanya nikakumbuka kwenye ligi kuu ana goli zaidi ya tano. Mawazo yangu yakarudi kwenye kikosi cha Yanga kutazama ni kiungo yupi anayetokea pembeni ambaye anafunga sana na kutengeneza nafasi nyingi za magoli akitokea pembeni.

Ilikuwa ngumu kwangu mimi kumpata huyo kiungo. Lakini wakati natafakari jibu sahihi nikamuona Mrisho Khalfan Ngassa. Mchezaji nyota ambaye enzi za ubora wake alikuwa na uwezo wa kumaliza ligi kuu akiwa mfungaji bora. 

Kumbuka huyu hakuwa mshambuliaji wa kati ila alikuwa kiungo anayetokea pembeni mwa uwanja. Alikuwa na uwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi za mwisho akitokea pembeni mwa uwanja. Lakini kwa wakati huo nguvu za miguu yake zilikuwa zimemwiishia.

Kwa hiyo Yanga haikuwa na kiungo wa pembeni ambaye alikuwa na uwezo wa kufunga magoli mengi akitokea pembeni. Mechi dhidi ya Namungo FC iliwaonesha Yanga kuwa wanahitaji aina hii mchezaji kwenye msimu unaokuja.

Namungo FC iliwakumbusha Yanga pia hata wachezaji ambao walikuwa wanacheza kama washambuliaji wa kati katika kikosi cha Yanga walikuwa siyo washambuliaji ambao walikuwa na uwezo mkubwa ukilinganisha na jina la Yanga.

Kuna wakati Yanga ilikuwa inahangaika kupata magoli, nyakati hizi ndizo nyakati ambazo timu unahitaji mtu ambaye husimama kama kiongozi katika safu ya ushambuliaji. Mtu ambaye anauwezo wa kuikoa timu katika nyakati ngumu lakini kwa bahati mbaya mtu huyu hakuwepo katika kikosi cha Yanga.

Naikumbuka mechi hii kwa sababu ya makosa mengi ya ulinzi kwa walinzi wa kati hasa Said Juma Makapu. Kiungo ambaye kwa asilimia kubwa alikuwa anatengeneza uwazi mkubwa katika eneo lake la nyuma uwazi ambao Namungo FC walikuwa wanautumia kuwaadhibu Yanga.

Kwa kifupi Namungo FC waliwaonesha Yanga maeneo sahihi ya wao kusajili wachezaji ambao watawasaidia kwenye ligi kuu msimu ujao. Hata baada ya mechi naikumbuka kauli ya aliyewahi kuwa kocha mkuu wa Yanga, Luc Eymael.

Luc Eymael alisema kuwa yeye anafundisha wachezaji ambao hakuwasajili yeye. Anafundisha watu ambao hakupata nafasi ya kuwaleta kwenye kikosi cha Yanga. Kauli hii ilinipa nguvu kuamini kuwa usajili mzuri ni ule ambao unafanywa na kocha na siyo viongozi.

Tayari dirisha kubwa la usajili lishaanza, Yanga imeshaanza kusajili na kwa bahati mbaya hakuna kocha ambaye anahusika na usajili huu kwa sababu Yanga haina kocha mkuu na kocha msaidizi kwa sasa hivi. Swali kubwa hawa viongozi wana taaluma ya ukocha na wanayajua mapungufu ya kikosi cha Yanga?

Nilifikiri usajili wa kwanza wa Yanga ungekuwa ni kuleta benchi la ufundi, benchi ambalo lingependekeza aina ya wachezaji ambao wanastahili kuwepo kwenye kikosi cha Yanga. Ni kitu cha kushangaza kuona usajili unafanyika bila kuwepo kwa benchi la ufundi.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Arsenal Chelsea

Giroud yuko tayari kwa shangwe za ubingwa FA

Gianni Infantino

Pingu zamnyemeleaโ€™ Rais wa FIFA