in

Usajili wa Simba na Yanga uzingatie michuano ya CAF

Baada ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kumalizika hivi karibuni, klabu za Yanga na Simba zilimaliza katika nafasi za juu na hivyo kupata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya klabu ya Afrika inayoandaliwa na shirikisho la soka barani, CAF.

Yanga waliotwaa ubingwa wa ligi hiyo, watashiriki michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa huku Simba wakitarajiwa kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho.

Baada ya ligi kumalizika, klabu nyingi zilianza harakati za kusajili wachezaji wapya watakaoimarisha vikosi vyao kwa ajili ya msimu ujao utakaoanza Agosti 20 na jana, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na shirikisho la soka nchini (TFF), ilikuwa ndio siku ya mwisho ya kukamilisha uhamisho wa wachezaji, kutoka klabu moja kwenda nyingine.

Klabu za Simba na Yanga ni miongoni mwa zile zilizoripotiwa kila uchao kuhusiana na usajili. Tangu harakati rasmi za usajili zilipoanza mwezi uliopita, wachezaji kadhaa nyota walidaiwa kuwa katika mazungumzo na viongozi wa klabu hizo na wengine wakithibitishwa hadharani kuwa tayari wameshakubaliana na timu hizo na kusaini mikataba yao.

Kwakuwa bado kuna siku kadhaa kabla ya kufikia Julai 20 ambayo ni siku ya mwisho iliyotangazwa awali katika kukamilisha zoezi la usajili , sisi tunaona kuna haja ya kuwakumbusha viongozi wa klabu za Simba na Yanga kuwa sasa zishirikiane vyema na maafisa wao wa benchi la ufundi katika kuunda vikosi imara vitakavyowapa nafasi ya kufanya vizuri katika michuano ya Afrika.

Tunawakumbusha kuangalia zaidi ushiriki wao katika michuano ya CAF na sio ligi kuu pekee kwa sababu haitakuwa jambo zuri kuziona timu hizi zikifanya vizuri katika ligi ya Bara, lakini zikiendelea kuliaibisha taifa kila mwaka kwa kuwa wasindikizaji wa michuano ya klabu bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Si jambo zuri pia kuona wenzetu wakifika mbali katika michuano ya klabu na hata kutwaa mataji mfululizo kama walivyofanya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika miaka miwili iliyopita huku sisi tunaowakilishwa na timu mbili za Bara na nyingine mbili za Zanzibar tukitumika kama ngazi ya mafanikio ya klabu za nchi nyingine.

Tunadhani itakuwa vizuri kama makocha wa Yanga, Simba na klabu za Zanzibar zitakazotuwakilisha kwenye michuano ya CAF wakapewa nafasi ya kuimarisha vikosi vyao kwa mtazamo wa kiufundi zaidi, na sio kuingiliwa na viongozi wa klabu ambao timu ikivurunda hujiweka kando na kuwatupia lawama makocha.

Uwakilishi wa klabu zetu katika miaka ya hivi karibuni hauvutii sana. Kwa mfano, Yanga walitolewa katika raundi ya kwanza ya michuano ya ligi ya klabu bingwa mwaka juzi na FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kufungwa nyumbani na ugenini kwa jumla ya magoli 4-2 na mahasimu wao Simba wakitolewa na Harass Al Hadoud ya Misri kwa magoli 7-3.

Wawakilishi wa Zanzibar katika ligi ya klabu bingwa Afrika mwaka juzi, timu ya Mafunzo ilitolewa pia na The Gunners ya Zimbawe huku Miembeni ikitolewa kwa idadi kubwa ya mabao na Petrojet ya Misri katika michuano ya Kombe la Shirikisho.

Hata katika michuano iliyopita, Yanga waliokuwa wakishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho walitolewa mapema baada ya kufungwa kwa jumla ya mabao 6-2 katika raundi ya kwanza na klabu changa ya Dedebit ya Ethiopia; Simba ikatolewa katika ligi ya klabu bingwa na Raja Casablanca na baadaye ikaangukia pua katika kombe la Shirikisho kwa kutolewa na DC Motema Pembe.

Hata wawakilishi wa Zanzibar, klabu za KMKM na Zanzibar Ocean View, pia hazikufika mbali baada ya kung’olewa na haohao DC Motema Pembe na AS Vita, pia ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Matokeo hayo mabaya ndiyo yanayotulazimu kuwapa rai viongozi wa Yanga na Simba kuwa makini katika usajili wao, kwani wakiendelea kusajili kwa kufuata utashi wao binafsi na kupuuza mapendekezo ya wataalam wa benchi la ufundi, kwa mara nyingine watakuwa wasindikizaji na kuwasononesha Watanzania.

Tunawasihi Yanga na Simba kuzingatia ushauri huu kwa kufanya usajili makini ili kusitisha aibu ya kuwa na vikosi dhaifu katika michuano ya CAF ya kila mwaka.

CHANZO: NIPASHE

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published.

Loading…

0

City rivals opt for National Stadium

Give National Stadium committed management