in , , ,

USAJILI UPI UMEKUWA WA MAFANIKIO ZAIDI?

 

Takribani jumla ya paundi milioni 870 zilitumika na klabu za EPL kwa ajili ya usajili wa wachezaji kwenye dirisha la usajili lililoishia tarehe 1 Septemba. Manchester City ndio waliotumia pesa nyingi zaidi kuliko klabu yoyote ya EPL. Walitumia takribani paundi milioni 160 kuwavuta Etihad Kevin De Bruyne, Raheem Sterling, Nicolas Otamendi, Fabian Delph na Patrick Roberts.

Manchester United ndiyo klabu iliyotumia pesa nyingi zaidi kwenye siku ya mwisho ya dirisha la usajili ilipolipa paundi milioni 36 kumtwaa Anthony Martial kutoka Monaco. Usajili huo ulimfanya Martial kuweka rekodi ya mchezaji wa chini ya miaka 20 aliyesajiliwa kwa pesa nyingi zaidi kwenye historia.

Pesa zilitumika kila timu ikijaribu kujiimarisha kwa ajili ya msimu huu unaondelea. Je kati ya wachezaji waliosajiliwa na klabu za EPL msimu huu ni yupi aliyeonyesha kiwango cha kuridhisha zaidi. Yaani ni usajili upi unaweza kusemwa kuwa wa mafanikio zaidi kwenye Ligi Kuu ya England msimu huu?

Jamaa wakiwa kazini
Jamaa wakiwa kazini

Baadhi ya watu wanaamini kuwa Kevin De Bruyne aliyetua Manchester City kwa dau la paundi milioni 54 akitokea Wolfsburg ya Ujerumani ndiye aliyeonyesha mafanikio zaidi kati ya wachezaji waliosajiliwa msimu huu. De Bruyne amekuwa moto wa kuotea mbali tangu alipotua Etihad Agosti 30. Mbaka sasa ameifungia City mabao manne na kutoa pasi tatu za mabao.

Wapo wengine wanaodai kuwa usajili wa mafanikio zaidi ni ule wa mshambuliaji kinda Anthony Martial. Mshambuliaji huyu ameweza kuifungia Manchester United mabao matano kwenye michezo yake tisa ya kwanza aliyocheza mbaka sasa. Cristiano Ronaldo alihitaji michezo 39 kufunga idadi kama hiyo ya mabao baada ya kujiunga na Manchester United Agosti 2003.

Dimitri Payet wa West Ham pia hawezi kuwekwa kando inapotajwa orodha ya wachezaji waliosajiliwa msimu huu na kuonyesha uwezo. Kiungo huyu raia wa Ufaransa aliyesajiliwa kutoka Marseille amekuwa sehemu kubwa ya mafanikio ya West Ham wanaoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa EPL. Ameifungia timu hiyo mabao matano na kutengeneza mengine matatu kwenye michezo 10 aliyoichezea.

Wapo pia washabiki wanaodhani kuwa Raheem Sterling ndiye amekuwa na mafanikio zaidi tangu alipojiunga na Manchester City akitokea Liverpool kwa dau la paundi milioni 49. Pengine hat-trick aliyofunga dhidi ya AFC Bournemouth kwenye mchezo wa mwisho wa EPL aliocheza ndiyo imezidi kuwashawishi washabiki hawa kuamini hivi. Hat-trick hiyo imemfanya awe ameifungia City mabao manne tangu alipojiunga na timu hiyo mwezi Julai mwaka huu.

Virgil van Dijk pengine hana washabiki wengi wanaomsapoti lakini mlinzi huyo kisiki wa Southampton ni mmoja kati ya wachezaji walioonyesha kiwango cha juu kati ya waliosajiliwa na klabu za EPL msimu huu. Kiwango alichoonyesha kwenye michezo mitano ya EPL aliyocheza mbaka sasa kinatosha kuwaaminisha washabiki kuwa amelitendea haki dau la paundi milioni 11 lililotumika kumng’oa Celtic.

Mlinda mlango mahiri wa Arsenal Peter Cech aliyejiunga na timu hiyo akitokea Chelsea kwa dau la paundi milioni 10 pia amekuwa kwenye kiwango cha juu. Cech ameweza kucheza michezo mitano bila kuruhusu bao msimu huu sawa na Joe Hart wa Manchester City. Mchezo wa juzi dhidi ya Bayern Munich na ule uliochezwa wiki tatu zilizopita dhidi ya Manchester United ni baadhi ya michezo ambayo alionyesha kiwango cha kushangaza na kumaliza dakika tisini bila kuruhusu bao lolote.

Yupi ni mchezaji aliyeonyesha kiwango cha juu zaidi mbaka sasa kati ya hawa sita waliosajiliwa na klabu za EPL msimu huu? Kura yako inakwenda kwa nani? Hata hivyo pengine ni mapema mno kutoa uamuzi kwa kuwa imebaki mizunguko 29 kuumaliza msimu huu wa EPL.

Advertisement
Advertisement

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Man United, City doro

Tanzania Sports

MTOANO KOMBE LA LIGI: