in ,

Ukurasa wa Mwisho wa kitabu cha John Bocco utakuwa wa Majonzi

Kuna hadithi nyingi sana ambazo huvutia na kusisimua kwa pamoja kipindi unazisoma. Na siku zote hadithi hubeba uzito mkubwa wenye mafundisho makubwa kwa jamii.

Ndiyo maana waandishi wa vitabu duniani wanabaki kuwa watu wanaoheshimika zaidi. Wanauwezo mkubwa wa kung’amua mambo na wanauwezo mkubwa wa kuandika vitu ambavyo vinaweza kubaki kuwa fundisho kubwa katika vizazi mbalimbali.

Kila kizazi hukaa na alama zake, kwenye mpira wetu kulikuwepo na kizazi cha kina Sunday Manara ambacho kilibaki na alama yake ambayo mpaka leo hii tunaikumbuka. Tunamkumbuka Sunday Manara kama mfungaji hatari kuwahi kutokea Tanzania.

Leo hii mtoto wa darasa la saba anajua kuwa Tanzania imewahi kufuzu mara moja tu katika michuano ya Afcon chini ya kizazi cha kina Leodigar Chilla Tenga, hii ndiyo alama ambayo iliwekwa na kizazi hiki cha kina Leodigar Chilla Tenga.

Alama inaoishi, itabaki katika mioyo yetu na itabaki katika kumbukumbu zetu kwa sababu ni moja ya kumbukumbu zisizofutika. Huwezi kuifuta kwa sababu wino wa jasho la damu ulitumika kuiandika alama hii.

Tunajivunia sana, tutaiimba sana na tutatamani siku moja tuifikie hata tujaribu kufika sehemu ambayo Marcio Maximo alipojaribu kutishika akiwa na kina Mrisho Khalfan Ngassa katika michuano ya CHAN.

Tutamkumbuka Marcio Maximo kama kocha ambaye aliturudishia hamasa iliyokuwa imepotea kwa muda katika tena chini ya wachezaji ambao wengi tulikuwa tunawachukulia kawaida.

Lakini ndiyo wachezaji ambao walishiriki kuweka alama ambazo tutakuja kuzikumbuka na kuzisumilia kwenye vizazi vinavyokuja.

Nitakuja kumsimulia mwanangu kuwa nilimshuhudia Mrisho Khalfan Ngassa akienda England kufanya majaribio kwenye ligi kuu ya England.

Wakati akiendelea kushangaa na habari hiyo ya Mrisho Khalfan Ngassa nitamgusia kuhusu Mbwana Ally Samatta , mshambuliaji ambaye nimemshuhudia akicheza katika mashindano ya ulaya.

Hizi zote ni alama ambazo zimewekwa na wachezaji wawili tofauti tena katika nyakati tofauti na zitasimuliwa katika uzito tofauti. Hadithi ya Mrisho Khalfan Ngassa itasimuliwa kama hadithi ambayo inafundisho la vijana kuhakikisha wanapata wasimamizi wazuri ili kufika mbali.

Kipaji pekee hakitoshi kumfikisha mchezaji mbali, kuna vingi amabvyo vinahitajika kwa mchezaji ili afike mbali na hivo vingi vipo kwenye kitabu cha Mbwana Ally Samatta.

Nidhamu, kujituma na kuwa na washauri bora na sahihi ndizo kurasa ambazo zitapamba kitabu cha Mbwana Ally Samatta.

Kitabu pekee ambacho nakisubiri kwa shauku kubwa ni kitabu cha John Bocco, mfalme wa Chamazi na hapana shaka ni mfalme wa ligi kuu Tanzania bara.

Magoli mia yakiwa yametoka katika miguu yake yamempa taji la Ufalme. Hakuna mchezaji aliyefanikisha kufikisha idadi hiyo ya magoli katika ligi kuu Tanzania bara.

Ni yeye pekee na anabaki kama mwamba ndani ya maji, atasimama katika kipindi chote cha masika na kiangazi na kudumu kwa muda mrefu huku akikumbukwa kwa alama hii.

Alama ambayo itaandikwa kwenye kitabu chake, kitabu ambacho sura ya kwanza kitajaa hadithi nyingi sana kuhusu yeye na ndoa yake na Azam FC.

Ndoa ambayo ilianzia tangu Azam FC ikiwa ligi daraja la kwanza, John Bocco alikuwa ni mmoja wa wachezaji ambao walitumia miguu yake kuipandisha Azam FC mpaka ligi kuu.

Ikapandana kwa imani kubwa sana ndani ya mioyo ya walio wengi. Wengi wakaamini kuwa Azam FC ndiyo mkombozi wa mpira wetu kutokana na uwekezaji mkubwa ambao walifanya.

John Bocco alitembea na Azam FC akakimbia nayo kwenye nyakati zote, walikuja washambuliaji wengi, walijaribu kupambana naye , wakaondoka na kumwacha akiihudumia klabu yake.

Alidumu miaka kumi (10 ) akiwa amevaa jezi ya Azam FC huku miguu yake ikifanikisha kufunga magoli 84. Hii ilitosha kumfanya kuwa mfungaji bora wa wakati wote wa Azam FC na mchezaji wa kuheshimika wa Azam FC.

Leo hii tunamuongelea kama mchezaji wa kuheshimika zaidi katika ligi kuu ya Tanzania bara. Amefanikisha kuwaliza magolikipa mara 100. Rekodi kubwa sana na yenye kuhitaji pongezi sana.

Pongezi ambazo zinaweza kukufanya utamani kuwa John Bocco angekuwa sehemu ambayo kina Mbwana Ally Samatta wapo. Lakini cha kuhuzunisha ni kuwa anaweza kumalizia maisha yake ya mpira sehemu ambayo alianzia.

Inauma, na inasikitisha sana kuona miguu ya mchezaji ambaye alitabiriwa kuwa ndiye Emmanuel Adebayor ajaye ikimaliza soka sehemu ambayo ilianzia.

Haikuweza kudhubutu kwenda nje kujaribu kucheza, haikuweza kuona umuhimu wa kuwa na washauri wazuri ambao wangemuongoza vizuri katika maisha yake ya soka.

Leo hii umri umeenda kwa kasi sana kwake. Hana muda mrefu sana wa kuendelea kupambana katika kiwango chake kikubwa kama zamani.

Yuko kwenye umri ambao vilabu vingi huogopa kumsajili kwa hofu ya kuporomoka kiwango kutokana na kupungua kwa kasi ya mchezaji ndani ya uwanja au kutokana na majeraha ya mara kwa mara.

Tumechelewa sana kumkumbusha John Bocco kuwa Tanzania ilikuwa siyo sehemu ambayo alitakiwa kucheza kwa muda mrefu. Tulitakiwa kumkumbusha mapema sana inawezekana leo hii angekuwepo hata sehemu ambayo alipo Abdi Banda.

Hii ingesaidia kusoma kitabu chake kwa katika mlinganyo ulio sahihi. Kwa sasa hakuna usahihi katika hatua zake za maisha ya soka kutokana na kipaji chake alicho nacho.

Tulitakiwa kumuongelea John Bocco kama mchezaji ambaye amefanikiwa kupiga hatua ya kucheza katika ligi za nje, lakini leo hii tunabakia kumsifia kwa kutumia muda mrefu kupambana na kina mwadui.

Kitu ambacho kinaumiza sana na kinakatisha tamaa sana lakini mwisho wa siku kinabaki kuwa funzo kubwa sana kwa wachezaji wengi wa ndani.

Kipi wanajifunza kwa John Bocco?, mazuri yake tu?, wanatazama sehemu ambayo John Bocco alianguka na wao kuchukua tahadhali ili wasianguke ?. Ndipo hapo ninapoamini kuwa pamoja na kwamba John Bocco anastahili pongezi kubwa kufikisha magoli 100 lakini hawezi kukwepa lawama kwa kuruhusu kurasa ya mwisho ya kitabu chake kuwa na sura ya majonzi.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

NANGWANDA IMENIFANYA NIONE KESHO YA SIMBA

Tanzania Sports

KATIKATI YA GIZA LA MARTIAL KUNA PENZI ZITO LA MASHABIKI