in , ,

UJERUMANI WATAFANIKIWA KUTETEA KOMBE LAO?

Kuna kitu kimoja ambacho mpaka sasa hivi Ujerumani wanakitafuta, nacho ni kufikia rekodi ya Brazil ya mwaka 1962 ya kutetea kombe la dunia. Hakuna timu nyingine ambayo imefanikiwa kutetea kombe hili la dunia.

Joachim Low anaenda Russia kama bingwa mtetezi baada ya kufanikiwa kuchukua kombe la dunia la mwaka 2014 huko Brazil, Je atafanikiwa kutetea kombe hili?. Ipi nguvu ya Ujerumani katika michuano hii ya kombe la dunia ?

Nguvu ya kwanza ambayo naiona kwenye timu ya taifa ya Ujerumani ni  uwepo wa Joachim Low. Tangu Jurgen Klinsman aondoke mwaka 2008, kocha Joachim Low ameshiriki katika mashindano makubwa sita ya kimataifa. Alienda na timu ya Taifa ya ujerumani katika mashindano ya Euro ya mwaka 2008, akaenda nayo katika michuano ya kombe la dunia la mwaka 2010, akaenda nayo katika michuano ya Euro ya mwaka  2012, akaenda pia na  timu ya taifa ya Ujerumani katika michuano ya kombe la dunia la mwaka la 2014.

Mwaka 2016 akaenda na timu ya taifa katika michuano ya Euro na kombe la mabara. Katika michuano hii sita amefanikiwa kuingia katika fainali tatu (fainali ya Euro ya mwaka 2008 akafungwa na Hispania , 2014 akaifunga Argentina katika michuano ya kombe la dunia  na mwaka 2016 akaifunga Chile katika michuano ya kombe la mabara).

Na katika michuano yote ambayo Joachim Low amekuwa na timu ya taifa ya Ujerumani ana wastani wa kufika nusu fainali katika kila michuano.Hii inaonesha Joachim Low ni mshindani mkubwa katika kila michuano ambayo anaenda na timu ya taifa.

Kuna faida yoyote ambayo Ujerumani wataipata kutokana na kutokuwa na mtu ambaye anaonekana timu imejengwa kupitia yeye?

Bila shaka kuna faida kubwa, na hii ni moja ya silaha waliyonayo Ujerumani. Ujerumani imejengwa kitimu, tafasri halisi ya neno “timu” iko katika kikosi cha Ujerumani. Kikosi cha ujerumani hakijajengwa kumtegemea/kumwegemea mtu mmoja, hii ni tofauti na wapinzani wao. Mfano, Brazil inaonekana imejengwa kupitia Neymar, Argentina imejengwa kupitia Messi, Ureno imejemgwa kupitia Cristiano Ronaldo kwa mfano katika mechi za kufuzu kombe la dunia nchini Russia, Cristiano Ronaldo alifunga magoli 15 ambayo ni sawa na 47% ya magoli ya ureno.

Kuachwa kwa Leory Sane kutakuwa na madhara makubwa ndani ya kikosi cha Ujerumani ?

Sidhani kama kutakuwa na madhara makubwa hasi katika kikosi cha Ujerumani kwa sababu ya ukubwa wa kikosi walicho nacho. Joachim Low amefanikiwa kutengeneza idadi kubwa ya wachezaji wengi wenye vipaji. Mfano katika Euro ya mwaka 2016 aliwaacha wachezaji nyota kama Marcus Reus, Julian Brandt, Sebastian Rude lakini walifanikiwa kufika hatua ya nusu fainali na hii ni kwa sababu ya utajiri wa kikosi walicho nacho. Kitu kizuri wana wachezaji wengi ambao wanacheza katika eneo la kiungo, wachezaji ambao wanaleta nafasi kubwa ndani ya kikosi kuwa na mbadiliko wa kimfumo na kimbinu ndani ya kikosi.

Mfumo wa 4-1-4-1 una nafasi ya kuibeba Ujerumani ?

Mfumo huu umekuwa na nafasi nzuri kwa Ujerumani kuleta uwiano wakati wa kushambulia na kuzuia. Mfano wanapokuwa wanashambulia wanakuwa katika umbo la 4-2–3-1, lakini wanapokuwa wanapoteza mpira hurudi katika umbo  la 4-1-4-1.

Kimbinu, Joachim Low amekuwa akiifanya Ujerumani icheze katika eneo la juu. Timu huwa inaanza kujipanga katika robo ya uwanja wao, hii huifanya timu iwe juu muda mrefu na kuifanya timu iilazimishe timu pinzani iwe katika eneo lake tu muda mwingi mwa uwanja.

Kuna faida yoyote ya mchanganyiko wa umri uliopo katika kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani?

Mchanganyiko wa vijana wapya na wazoefu unatakuwa na faida kubwa sana kwa ujerumani, kikosi cha Ujerumani cha mwaka  2014 kilichochukua kombe la dunia kilikuwa na wachezaji kama Philipe Lahm, Per Mertersacker, Bastian Schweinsteiger, Miroslav Klose, lakini mwaka huu Ujerumani wanaenda na wachezaji vijana wenye vipaji kama Joshua Kimmich, Timo Werner , Niklas sule. Wachezaji hawa wapya wako chini ya wachezaji wazoefu kama kina Mesut Ozil, Mats Hummel’s, Thomas Muller na wengine ambao wanaleta mseto mzuri ndani ya kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MATUMAINI YA SAFARI YA ENGLAND KOMBE LA DUNIA YAPO HAPA!

Tanzania Sports

Morocco: Uenyeji Kombe la Dunia ngoma inanoga