in

Ubovu Yanga, kwenye uongozi mpaka kwenye timu..

Dar young africans

Yanga imekuwa timu ya kawaida, ukawaida ambao siyo wa kawaida . Ukawaida ambao umekuwa wa kuhuzunisha sana. Yanga imekuwa ikiingia uwanjani huku haina uhakika wa kupata ushindi ndani ya uwanja hata dhidi ya timu ambazo zinaonekana za kawaida kwa Yanga.

Tumeshashuhudia Yanga mbovu nyingi sana lakini hatujawahi kushuhudia Yanga inayohaingaika kupata ushindi dhidi ya Mwadui FC, Kagera Sugar, Polisi Tanzania au JKT Tanzania. Imekuwa kawaida sana kwa Yanga kucheza kawaida na kutokuwa na uhakika wa kupata ushindi hata dhidi ya timu za kawaida.

Moja ya sababu ambayo inaifanya Yanga kuwa timu ya kawaida ni Yanga kugawanyika katika makundi manne ambayo hayana ushirikiano katika ujenzi wa klabu na timu. Yanga kwa sasa iko katika makundi manne. Kundi la kwanza ni Yanga ya Mshindo Msolla, kundi la pili ni Yanga ya GSM, kundi la tatu ni kundi la Yanga ya Luc Eymael na kundi la nne ni kundi la Yanga ya Boniface Mkwasa.

Tuanze taratibu kutazama kila kundi, tuanzie hapa , kundi la Yanga ya Mshindo Msolla, kimsingi hili kundi ndilo lilitakiwa kuwa na msimamo mkubwa kuhusiana na masuala ya utawala wa klabu pamoja na usimamizi wa timu ya Yanga kwa sababu ndilo kundi ambalo lilikabidhiwa mamlaka ya kuongoza.

Lakini kundi hili limekuwa halina sauti kuanzia masuala ya utawala mpaka usimamizi wa timu. Masuala mengi ya utawala ndani ya klabu yamekuwa yakisemewa na kundi la pili la GSM ambalo tutakuja kulitazama baadaye. Kundi hili la Yanga ya Mshindo Msola limekuwa likishindwa hata kutoa ufafanuzi mzuri kuhusiana na masuala mbalimbali.

Kumetokea suala la Bernard Morrison kuonesha utovu wa nidhamu lakini kundi hili halikuwa na nguvu sana kuanzia kwenye kulitatua mpaka kulisemea. Suala la kocha msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa kutofautiana na mshambuliaji wa Yanga  David Molinga lilitatuliwa na kundi la pili la Yanga ya GSM, Yanga ya Mshindo Msolla imekuwa Yanga ambayo ni kibogoyo.

Kundi la pili ni kundi la Yanga ya GSM, hili kundi ndilo kundi ambalo linaonekana na nguvu pamoja na ushawahi mkubwa kutokana na kuwa na fedha.  Hili ndilo kundi ambalo linajihusisha kwa kiasi kikubwa na kusajili wachezaji ambao wanaonekana nyota katika kikosi cha Yanga, ndilo kundi ambalo linalipa mshahara kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi.

Ndilo kundi ambalo linatoa motisha kwa wachezaji na benchi la ufundi, unakumbuka kipindi ambacho Yanga ya GSM ilivyokuwa inatoa milioni 10 kwenye kila ushindi ambao Yanga ilikuwa inapata kwenye mechi za ligi kuu ya Tanzania bara, ndilo kundi pendwa ndani ya Yanga kwa sababu linatoa umate mate.

Kundi la tatu ni kundi la Yanga ya Luc Eymael . Hili ni kundi ambalo linaongozwa na kocha mkuu wa Yanga, Luc Eymael. Ni kundi ambalo lina kiburi haswa kwa sababu lilisajiliwa na kundi la Yanga ya GSM. Kumbuka Yanga ya GSM ndiyo inayolipa mishahara, pesa za usajili pamoja na posho za mechi mbalimbali.

Kundi hili la Yanga ya Luc Eymael lina makocha pamoja na wachezaji ambao walisajiliwa na kundi la Yanga ya GSM. Ni ngumu kwa kundi hili la Yanga ya Luc Eymael kulitambua kundi la Yanga ya Mshindo Msolla. Wao wanaamini waajiri wao ni kundi la Yanga ya GSM na siyo kundi la Yanga ya Mshindo Msola.

Kundi la nne na la mwisho ni kundi la Yanga ya Charlses Boniface Mkwasa. Hili ni kundi la wanyoge sana. Kundi hili halikusajiliwa na kundi la Yanga ya GSM. Kundi hili la Yanga ya Charles Boniface Mkwasa ni kundi ambalo linajumuisha baadhi ya makocha na baadhi ya wachezaji wa Yanga.

Hili ndilo kundi ambalo halina sauti kwa kiasi kikubwa ndani ya klabu ya Yanga. Ni kundi la watoto yatima kwa sababu halina mahusiano makubwa na kundi la Yanga ya GSM. Ugawanyiko wa makundi haya manne ndani ya Yanga imeifanya Yanga iwe na matokeo ambayo siyo mazuri ndani ya ligi kuu Tanzania bara na kombe la shirikisho.

Yanga imekuwa dhaifu kubwa sana, tangu Luc Eymael awe kocha wa Yanga, ameiongoza Yanga katika mechi 26, huku akipata sare kwenye mechi 12 na kushinda mechi 11 huku akifungwa katika mechi 3. Yanga ya Luc Eymael imekuwa timu ambayo ikipata sare nyingi hata dhidi ya timu ambazo siyo timu za kupata na Yanga.

Udhaifu huu wa Yanga ni kwa sababu ya kutokuwa na ushirikiano kwenye haya makundi manne. Kundi ambalo lilikuwa muhimu kuunganisha makundi yote manne na kuleta umoja ni kundi la Yanga ya Mshindo Msolla. Hili ndilo kundi ambalo lilichaguliwa kwa ajili ya kufanya kazi za utawala ndani ya Yanga na kuendesha timu. Lakini kundi hili limekuwa dhaifu, udhaifu ambao umeifanya Yanga iwe dhaifu ndani ya uwanja.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Coastal Union

Simba kuzikosa alama tisini

Leeds United

Ninavyokumbuka watemi wa Leeds United