in

Tuwekeze zaidi kwenye kutambua vipaji vya wanamichezo wapya, kisha matuzo yafuate baadaye……

Na:Israel Saria
————-
Moja ya vitu vinavyoitambulisha nchi mbele ya jumuiya ya kimataifa ni michezo.
Michezo hutumiwa kama jukwaa muhimu, kwa mashujaa wa nchi husika kupeperusha bendera kwa kufanya vizuri michezoni.
Hakuna anayevutiwa na kilicho kibaya, kwa hiyo wachezaji wanaposhiriki mashindano ya kimataifa na kufanya vibaya huwa aibu ya nchi na watu wake.
Kwa asili, michezo ilikuwa na malengo ya kujenga afya, ukakamavu, kuwa kiungo katika jamii, kuonyesha uwezo na vipaji vya watu kwa wenzao na kuendeleza uhusiano na urafiki kati ya jamii moja na nyingine.

Leo hii, pamoja na baadhi ya haya kuenziwa kimaandishi au nyuma ya pazia, michezo imegeuzwa soko la ‘kuuza’ nchi, ni eneo muhimu la mataifa kujitanua, kutamba na hata kujikuza kiuchumi.
Chochote unachowekeza kwa mipango na kufuatilia hulipa sana, na ndivyo wanavyovuna wenzetu wa baadhi ya nchi za Ulaya na za mabara mengine, hata baadhi za Afrika.
Lakini kuwekeza katika soka si jambo la siku, mwezi wala mwaka mmoja, yahitaji moyo na kama ni watu au taasisi zinazotaka kuibuka na ushindi wa haraka, hilo litabaki kuwa ndoto ya mchana.
Tanzania imekuwa na mipango mizuri vitabuni, viongozi wake tangu awamu ya kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wameeleza na kusisitiza kila wakati umuhimu wa michezo hadi leo hii.
Hata hivyo, tukubali tusikubali, kuna mahali ambapo bado kuna kasoro, na isiporekebishwa, Januari hadi Desemba, wadau wa michezo watabaki kulaumiana.
Ilivyo ni kwamba, kutokana na hamasa inayowekwa wakati wa mashindano, hasa ya kimataifa yanayoshirikisha klabu au timu za taifa, timu zetu huweza kuanza vizuri kwa ushindi, lakini hukosa uendelevu na kuishia hatua za awali kabisa.
Kwenye ligi kuu ya soka Tanzania, imekuwa kawaida kila mwaka kufurahia ratiba zinapopangwa, na kupamba vichwa vya habari kwenye magazeti na kutangazwa redioni na hata kwenye televisheni tarehe za michezo ya watani wa jadi – Simba na Yanga.
Je, nini kinatokea baada ya hapo? Hupatikana bingwa wa Tanzania na mshindi wa pili hadi wale wanaoshuka daraja. Kisha uwakilishi wa nchi, ambapo kumbukumbu za karibuni ni za kutolewa mapema kwenye michuano.
Julai hii Uingereza inaandaa Michuano ya Olimpiki, kila baada ya miaka minne imekuwa ikiandaliwa na Tanzania ipo, lakini tangu mwaka 1980 Filbert Bayi na Suleiman Nyambui walipoipatia nchi medali za fedha, hakuna aliyeleta nyingine hadi leo.
Hakuna mafanikio ya kuridhisha wala ya kujivunia kimataifa nchini Tanzania katika michezo ya soka, hoki, ndoni, netiboli, riadha, kikapu, wavu, tenisi, meza, mikono, kriketi, golfu na mingineyo.

Ukiacha vikombe vidogo vidogo vya kikanda, kama Yanga ambayo ni bingwa wa Afrika Mashariki na kwenye netiboli ambapo hapa na pale wamekuwa wakitwaa vikombe, katika mashindano ya bara zima au ya dunia imekuwa ngumu.
Mfano mmoja mzuri ni mchezo wa kuogelea. Huu mchezo ambao pamoja na kwamba baadhi ya wenzetu wajuao ‘kuogelea’ wanaweza kuchomoza uzuri, unahitaji ufundi tofauti.
Pamoja na kuwa na chama cha mchezo huo, hadi leo miaka 50 baada ya Uhuru, Tanzania haina bwawa la kiwango cha kimataifa – ukubwa wa mita 50 kwa 25. Hakuna, yapo mabwawa ya aina ambayo watu au taasisi wanaamua tu kuchimba wapendavyo, pengine kuvutia wateja kwenye maeneo yao ya burudani au kwa kutojua kanuni na viwango vilivyowekwa.
Lazima tufike mahali, na ni sasa, tujiulize; Watanzania kipi kinatukwamisha?
Kujua ugonjwa ni sawa na kuupatia nusu ya tiba. Kadhalika kujua kiini cha Watanzania kukwama kwenye michezo tutakuwa tumepiga hatua muhimu ya kupata ufumbuzi wake. Mficha maradhi kifo humuumbua, wamesema wahenga.
Kama ilivyoelezwa awali, mfumo wa michezo umesukwa vizuri tu, kama kuna kasoro ni kidogo wala si sababu ya kutetereka kisoka.
Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 iliyoanza kuandaliwa tangu 1985 ni nzuri, kwani imesheheni karibu kila silaha ya kupambana vita hii ya kuipatia Tanzania heshima duniani kupitia michezo.
Lipo Baraza la Michezo la Taifa (BMT), chombo cha juu cha kuratibu michezo nchini Tanzania, ambalo kwa hakika limekuwa likifanya kazi zake vizuri kusimamia michezo kwa kuunda kanuni na kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.
Vipo vyama vinavyofurahisha kwa jinsi vilivyoweza kuunda kamati mbalimbali muhimu za kusimamia michezo siku hadi siku, vikiwa na watu mahiri wenye ujuzi tofauti katika kuamua ubishani wa kisheria na usio wa kisheria unaotokea, na baadhi ya vyama vya aina hiyo ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Lakini wapo wengine ambao ni wanyonge, na baadhi ni kana kwamba hawapo kabisa, kwa sababu hata ofisi hawana.
Katika mlolongo wa michezo iliyotajwa mwanzoni mwa makala hii, kuna isiyojulikana si tu ofisi za vyama vyake ziko wapo, bali pia viongozi wake ni akina nani.
Lakini wakati uchovu wa aina hii ukiachwa kutamalaki, kuna mamilioni ya shilingi humwagwa kila mwaka na wenye pesa kwenye michezo hiyo hiyo.
Kupanga ni kuchagua, kwa hiyo hata wanaomwaga mamilioni hayo, wanatakiwa kutafakari kabla ya kuamua mahali pa kuyamwaga.
Lakini pia wanaowashawishi kuyamwaga pengine wanakosea, na wangetumia nguvu ya ushawishi wao au ukaribu wao na matajiri husika kuelekeza fedha hizo sehemu mwafaka zaidi.
Pamekuwa pakitolewa zawadi kwa wanamichezo mbalimbali bora nchini Tanzania kila mwaka, ambapo Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TASWA) kimekuwa ndicho mwandaaji mkubwa.
Lakini kando yake kuna kampuni ambazo hujitokeza kudhamini, kwa sababu pasipo udhamini wa wenye fedha hao, ni vigumu kwa vyama kama vyama kutekeleza wajibu huo ipasavyo.
Kila mwezi pia pamekuwapo mchezaji bora anayepata kitita chake pia, na yote hayo si mambo mabaya katika yenyewe, lakini yangeweza kuboreshwa zaidi, ikiwa tunataka uendelevu wa mafanikio na maendeleo ya soka.
Tumeshuhudia Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi akikabidhi zawadi washindi wa tuzo za TASWA, baada ya kutoa nasaha zake kuhusu umuhimu wa michezo mbalimbali kupewa umuhimu.
Hoja ya msingi inabaki kuwa ile ile, bila maandalizi ya muda mrefu itakuwa tuzo za ndani hazitakuwa na maana kubwa, kwa sababu Tanzania itaishia kupeleka timu dhaifu kwenye mashindano na kuchafua jina la taifa.
Kwa vile sasa imedhadhihirika kwamba kuna watu na taasisi waliodhamiria na waliokwishaanza kuwekeza fedha kwenye michezo, na kwa kuwa upo udhaifu mkubwa katika maandalizi ya wanamichezo mbalimbali, ni wakati mwafaka sasa kuelekeza fedha hizo kwenye maandalizi.
Tumeshapata uzoefu wa kutosha kuhusu maandalizi duni, hata sasa Olimpiki inayokuja mataifa mengine yanapeleka wachezaji wengi, lakini Tanzania imekuwa ya kukusanya kusanya wachezaji kiaina, na wengine wakitoka ng’ambo kueleza wamefuzu bila hata vyama vyao kujua kama walikuwapo.
Inatambulika kwamba waandishi wa habari wapo kwenye mhimili wa nne wa dola (hata kama si rasmi), na ukali wa kalamu una athari nyingi – chanya na hasi kwa jamii.
Hawa ni watu wanaofukua habari kutoka vyanzo vya aina nyingi, ndio wanaochunguza na kuibua mambo makubwa yanayokuja kushangaza jamii, nchi na hata jumuiya ya kimataifa.
Kwa uwezo wao huo huo, kwa akili yao hiyo hiyo na sasa wawe na dhamira kama hayo yaliyotangulia, kujielekeza si tu kuibua mambo hasi, bali katika kuijenga Tanzania kwa kutumia michezo.
Katika muktadha unaojadiliwa hapa, ni muhimu kwa waandishi kutumia nyenzo zao kwa marefu na mapana yake kuibua na kutambulisha vipaji vya wanamichezo mbalimbali.
Sahau soka kidogo, tafakari michezo mingine na vipaji vilivyojificha pembezoni mwa Tanzania yetu kubwa isiyofikika kirahisi, lakini pia ambayo wenye vipaji hao si rahisi wakavionyesha kwa umma nje ya vijiji, kata, tarafa au wilaya zao.

Ni aibu kwamba tangu hiyo 1980 hadi leo medali za fedha na kubwa kuliko hizo hazijaletwa tena kutoka Olimpiki katika michezo tofauti, lakini kwa namna ya pekee riadha.
Kuna mikoa inayojulikana kwa kuwa na wanariadha wa asili wengi; hawa wala hawaundwi, wanajianzisha wenyewe, kwa sababu ya mazingira ya vijijini mwao, ni juu ya waandishi na wadau wengine sasa kwenda kuwaibua na kuwaweka juu kwenye ramani.
Ndiyo fursa iliyo mbele yetu kwa wenye moyo wa kuchangia michezo ambao wanamwaga mamilioni katika usajili, tuzo kwa makundi mengi kupindukia na hata kufadhili makundi kwenye klabu tofauti, kujielekeza huko.
Mtoto gani aliye ndani ya vizuizi vya mtaa au kijiji chake maporini mwenye kipaji anayeweza kukianika kwa umma unaoamini kwamba Dar es Salaam ndiyo kila kitu?
TASWA na wadau wengine wanatakiwa kuwa na zile ‘pua za kunusa vipaji’ na kuvifuata huko vilipo, hata kwa kuvuka madaraja ya kamba za miti kwenye mito iliyofurika, mwisho wa siku kinachotakiwa kuonekana ni kile kipaji kilicho ndani kabisa kijijini kikinuliwa hadi taifani na kwenda kung’ara kimataifa.
Jinsi ya kufanya kazi hiyo kitaaluma waandishi wanajua, uwezeshaji na ufanikishaji wake wadau wengine waliokwishajitokeza na wenye moyo huo wanajua pia, ni kuweka nia tu na kuanza.
Haya ni mawazo mbadala – kwamba badala ya kukusanya kitita kikubwa cha fedha na kumpa mtu mmoja kwa vile amekuwa bora kuliko wengine wengi (ambao kwa ujumla wao pengine wapo chini ya kiwango sana), kitita kisambazwe kuibua vipaji vya kweli.
Kutokana na maendeleo ya ulimwengu siku hizi, lazima vipaji hivyo vikishang’amuliwa vikusanywe na kuwekwa pamoja, ndiyo kusema tuwe na kambi, darasa au academy kama wenzetu wanavyopenda kuita.
Wote watakaokuwa wamekusanywa kutoka kusini, kati, kaskazini, mashariki na magharibi, watatakiwa kuanza mafunzo kwenye kituo au vituo maalumu, ambapo pamoja na kuendeleza michezo hiyo, watafunguliwa zaidi akili zao, ili kwenda na wakati.
Bado hapa ndani hatujakuwa na wachezaji maarufu wa kuwamwagia mamilioni kiasi hiki, ingekuwa hivyo wangekuwa kwenye ligi kubwa nje wakijiwinda kama wenzao wa Afrika Magharibi wanavotamba.
Tunao wengi wenye nia ya kushiriki michezo, wenye mwamko wa kushindana kwa malengo mbalimbali, lakini hawafanikiwi kwa sababu ya mazingira, kwa sababu ya miundombinu isiyoruhusu na hali halisi ya uchumi inayoelezwa kuwa mbaya.
Nguvu ya kalamu na ya wadau wengine ambao ni watu binafsi na taasisi, kampuni tofauti na hata shindani, ndiyo itakuza michezo ya Tanzania na bendera yake itapeperushwa vyema kama wengine wanaotamba kwenye Olimpiki, Jumuiya ya Madola, Kombe la Dunia na kwingineko.
Kwa kutumia Sera ya Maendeleo ya Michezo, Serikali kwa njia mbalimbali inaweza kuratibu mchakato huu wote, ili hatimaye baada ya muongo mmoja hivi, Tanzania iweze kuwa tishio mbele ya nchi nyingine.
Michezo ni chanzo kikubwa cha fedha, zipo nchi zilizo radhi kutumia mabilioni ya Dola au Pauni kwa ajili ya kuweka msingi wa michezo, lakini wakianza kuvuna, kwao ni kicheko siku zote.
Michezo inaweza kutumia katika kukuza uchumi, kwa sababu ikishajengewa miundombinu mizuri, nchi ikawa na wachezaji wengi katika michezo tofauti, huwa chanzo kikubwa cha ajira, na hivyo kipato.
Mapato hayo ya mchezaji mmoja mmoja hukatwa kodi na kuiingizia serikali mapato, lakini pia miundombinu ya soka inayojengwa huja kuingiza fedha nyingi za ndani na za kigeni kadhalika.
Viongozi waliokabidhiwa dhamana ya michezo wakiwa na dhamira ya dhati, haitachukua muda Tanzania itakuwa mbali, kwa sababu vipaji vipo, watambuzi wa vipaji wapo na mazingira ya kuvikuza na kuviweka sokoni yanaweza kutengenezwa bila tatizo.
Huu ni wakati wa wadau wote wa michezo kukusanyana, wakiwamo waandishi, na kujipanga kutimiza ndoto ya maendeleo ya kweli ya michezo Tanzania.
Serikali, kama baba ianze hatua ya kwanza ya kuviweka vyama vya michezo katika mazingira mazuri – mguu wa kuanzia safari hii muhimu na ya haraka kuanza.
Kigingi kimojawapo cha viongozi wa michezo na vyama vyao ni kutokuwa na ukwasi; hawana senti za kutimiza majukumu yao.
Inafika mahali unakuta chama hakina ofisi wala majadala, na kama yapo basi kiongozi wa chama husika anayahifadhi nyumbani au kwenye ofisi nyingine isiyohusiana na michezo.
Hii ndiyo kusema wengine wana ofisi za mifukoni au za kwenye mikoba (briefcase), na mtu akiugua, akisafiri, akiwa na udhuru, akijiuzulu au kukosana na wenzake ndio kusambaratika kwa kila kitu.
Maana yake hapa ni kwamba hakuna mfumo; bila mfumo hakuna msingi bora wa michezo na mafanikio yatakuwa ndoto, yanaweza kuonekana kama anavyonyanyuliwa mchezaji mmoja kuelezwa ni mahiri kwa vile alifunga mabao, alilamba chenga au kudaka sana, lakini alidaka mashuti ya nani? Alimfunga nani? Alimpiga nani chenga? Je, hatujifunzi tu katika simulizi za kipofu mmoja kutoweza kumwongoza mwenzake – kwamba wote watatumbukia shimoni?
Labda tunashabikia ‘uafadhali’ miongoni mwa wagonjwa, halafu tunatoa tuzo za mamilioni, kupiga makofi, kula na kunywa kisha tunarudi majumbani, lakini baada ya hapo kimataifa hatuna tulichopata, wale bora wamefanya nini? Nchi haipati tuzo maana haijazishinda nchi nyingine. Tunafurahia tunavyocheza ndani kwa ndani, wala nje hawatujui na ikitokea wametujua inakuwa kama moto wa mabua, unababua mara moja na kuzimika, waliodhaniwa wameunguzwa nao wamebaki wazima na hata mabua hayakuacha majivu, achilia mbali mkaa!
Ukiwa na mfumo panakuwapo uendelevu, ndiyo maana serikali kama mdau kiongozi ingetarajiwa itoe moja ya majengo yake mengi kwa ajili ya ofisi za vyama na kiongozi mmoja awe mratibu au ofisa tawala mmoja kwa vyama hivyo vya michezo mbalimbali vinavyodhaniwa kutokuwa na nguvu.
Katika jengo hilo la ofisi, Serikali ya Tanzania ivipe laini moja ya simu kwa vyama hivyo pamoja na kuhakikisha panakuwapo aina fulani ya ruzuku kutoka kwenye fungu la bajeti ya michezo, maana huko ndiko kuendeleza michezo kwenyewe.
Mawasiliano ya uhakika yataanza kujengwa sasa kati ya ofisi husika na wanamichezo kote mikoani na hata waandishi wanapofanya upekuzi wao wa vipaji inakuwa rahisi kuwakutanisha mchezaji tarajali na kiongozi wake kabla ya kupelekwa kwenye kituo husika.
Kwa vile gharama za maandalizi ni kubwa, lazima serikali iweke mkono wake, maana ndiyo taasisi yenye uhakika wa kipato, na zaidi sana iliyopo kwa ajili ya watu.
Wafadhili wa hiari huja na kupotea, wanaotoa fedha kudhamini mashindano wapo leo lakini keshokutwa hujui walikotokea na wanaogharimia tuzo huwezi kuwa na uhakika na uswahiba wao kila mwaka.
Lakini mfumo ukishawekwa, ofisi zikawapo, kituo madhubuti cha michezo mbalimbali kikaanza na baadaye kujengwa vituo kila kanda kabla ya kuzama mikoani, wafadhili wa ndani na nje watavutiwa.
Kwa hiyo nguvu itawekwa katika kambi kwa michezo yote ambayo wadau wamekubaliana waiendeleze. Kambi zinakuwa za muda mrefu mfano wa shule, hata wanamichezo wanapokwenda kwenye mashindano wanakuwa wameiva na wanajua wanakwenda wapi, kufanya nini na kwa sababu gani.
Leo hii wapo wanaokwenda akilini wanawaza jinsi watakavyozamia. Wapo wa nchi ya kigeni walikuja Tanzania wakaomba ukimbizi na ukaazi wa kudumu na wengine wanafikiria kusafirisha mihadarati. Kituo cha michezo kitatoa elimu ya jumla kwa wote.
Huu ni wakati wa kurejesha hamasa ya michezo iliyokuwapo zamani; enzi za mashindano na makombe ya Masumin, Bonite, KLM, Nyerere, Muungano na hakika walimu na wanafunzi wote walikuwa lao moja. Hii ni pamoja na kuboresha Umitashumta na Umiseta.
Uzuri wa michezo ni kwamba katika kufanikiwa inakuwa furaha ya wote, tuzo zinatoka za kimataifa, jina la nchi linang’aa na ndiyo inakuwa njia ya moja kwa moja ya kujitangaza kwenye utalii.
Ama kwa upande wa soka ambayo kwa ndani ya nchi hatua imepigwa, bado wadau wanatakiwa kuibua vipaji zaidi na kuvikuza ili bingwa au mshindi wa pili wa ligi kuu akafanye mambo makubwa kwenye mashindano ya Afrika.
Tuzo tunazipenda, ni nzuri maana ni utambuzi wa jitihada, lakini kama wanaotunukiwa leo ndio wamefika kilele cha mafanikaio na kesho wameshaanguka na kusahaulika, hazina maana, bora wafunzwe zaidi ili wafaidi kwa kitambo kirefu maishani.
[email protected]

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Pasua kichwa ya teknolojia ya goli katika soka

Mabilioni yaboreshe michezo, kisha tuzo zifuate baadaye…….