in

Tusisahau kukisifu kichwa cha Sven Vandenbroeck

Sven Vandenbroeck

Kuna vingi sana ambavyo vinaweza kuongelewa kuhusiana na mechi ya juzi ya ligi ya mabingwa barani Africa  kati ya Simba na FC Platnumz ya Zimbabwe.

Kuna midomo itamsifu Haji Manara kwa kufanikisha hamasa kubwa ndani na nje ya uwanja. Kuna midomo mingine itasifia kiwango cha Claoutus Chota Chama.

Na kuna midomo mingine itasifia pia kiwango cha Larry Bwalya na kuna marafiki zangu wengine wataendelea kumsifia Erasto Nyoni pamoja na umri wake kuwa mkubwa lakini kiwango chake kinazidi kuimarika.

Sifa zote hizi zitawafikia lakini kuna mtu mmoja anaweza kusahaulika kwa kiwango kikubwa. Mtu huyu kwenye mechi ya jana alikuwa amekaa suruali nyeusi na shati jeupe.

Muda mwingi aliutumia kusimama mbele ya benchi la Simba. Macho yake yalikuwa yanatazama uwanjani, akili yake ilikuwa tulivu kuusoma mchezo wa jana. Utulivu wa akili yake ndiyo ulikuwa silaha kubwa.

Utulivu wa akili yake ndiyo ulifanya hamasa ya Haji Manara iwe bora , utulivu wa akili yake ndiyo ulifanya viwango vya kina Larry Bwalya, Cloutus Chota Chama, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni kuonekana bora.

Ni kwa namna gani utulivu wa akili ya Sven Vandenbroeck ulikuwa silaha kubwa kwa Simba? Kwanza tunatakiwa kufahamu kuwa FC Platnumz wamefanikiwa kucheza ligi ya mabingwa barani Afrika ngazi ya makundi kwa miaka miwili mfululizo, kwa hiyo Sven Vandenbroeck alikuwa anakutana na timu yenye uzoefu.

Kitu cha pili tunachotakiwa kukifahamu ni kuwa kabla ya mechi ya jana Simba walikuwa nyuma ya goli moja. Kwa hiyo Simba walikutana na mazingira mawili magumu kwenye mechi ya juzi, walikutana na timu bora ambayo kwa miaka miwili mfululizo imefanikiwa kucheza hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika na walikuwa nyuma ya goli moja.

Sven Vandenbroeck alifanikiwa kutengeneza mazingira ambayo yaliweza kuendana na hizo changamoto mbili ambazo nimezitaja hapo juu. Mazingira yapi hayo aliyotengeneza Sven Vandenbroeck kwenye mechi ya jana?

Sven Vandenbroeck alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kubadilika kwenye mchezo wa jana kulingana na mahitaji ya mechi kwa muda husika. Kwa mfano, kwenye mechi ile alibadilisha uchezaji kulingana na matokeo.

Kipindi cha kwanza anamwanzisha Said Ndemla na Larry Bwalya wakicheza kama Pivot . Wakawa na mbadilishano wa kimajukumu. Wakati Larry Bwalya alipokuwa anapanda juu kushambulia, Said Ndemla alibaki nyuma. Wakati Said Ndemla alipokuwa anapanda juu, Larry Bwalya alibaki nyuma.

Nyuma yao kulikuwa na mabeki watatu ambao walikuwa wanawalinda, Erasto Nyoni Joash Onyango na Pascal Wawa. Hii ilisaidia kuleta uwiano kwenye kuzuia na kushambulia. Sven Vandenbroeck aliwafanya Simba watafute goli huku wakiwa na tahadhali nyuma.

Alipoingia kipindi cha pili, Sven Vandenbroeck alikuwa na goli moja. Goli ambalo lilikuwa halimhakikishii kufuzu, hivo alitakiwa apate goli la pili.

Sven Vandenbroeck alimtoa Said Ndemla na kumwingiza Ibrahim Ame. Tafasri yake ilikuwa moja Erasto Nyoni alikuwa kiungo mkabaji. Kwenda kwa Erasto Nyoni kuwa kiungo mkabaji kilimpa uhuru Larry Bwalya kusogea juu .

Ibrahim Ame alikuja kuimarisha beki. Pia eneo la kiungo cha kuzuia liliimarika kwa sababu Erasto Nyoni ni mzuri zaidi kwenye kuzuia kuzidi Said Ndemla.

Baada ya Simba kuwa mbele ya Magoli  2-0! Sven Vandenbroeck alirudisha wachezaji nane wakae nyuma ya mpira na kutegemea mashambulizi ya kushtukiza. Hapo ndipo ikawa nafasi nyingine ya Claoutus Chota Chama kung’aa. Kwa hiyo ukiangalia namna mpira ulivyokuwa unabadilika ndivo ambavyo Sven Vandenbroeck alivyokuwa anabadilika na kuwafanya baadhi ya wachezaji wang’ae. Ndiyo maana naona kabla ya kuwasifu kina Claoutus Chota Chama tunatakiwa kumsifu Sven Vandenbroeck.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
La Liga

La Liga bila nyota wakubwa hali itakuwaje, serikali itakwepa lawama?

Sergio Ramos

Je, klabu zinaweza kuvunja utaratibu kwa mchezaji pendwa?