in , ,

TUSIISHIE TU KUJIVUNIA MAFANIKIO YA SAMATTA NA ULIMWENGU

*Sasa nini kifanyike kuwapata hao ‘Samatta na Ulimwengu’ wengi zaidi?*

 

Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wameleta shangwe zisizoelezeka nchini Tanzania baada ya kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika wakiwa na TP Mazembe siku ya Jumapili walipoifunga USM Alger mabao mawili kwa sifuri.

Samatta aliyeifungia Mazembe mabao saba kwenye mashindano hayo ndiye aliyetufanya watanzania wengi kujivunia zaidi. Hata rais mstaafu JK jana alieleza namna alivyofurahishwa na kiwango cha mchezaji huyo aliyetwaa tuzo ya mfungaji bora.

Niwapongeze mno Samatta na Ulimwengu ambao wamekuwa watanzania wa kwanza kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika. Natumaini watatufanya tujivunie zaidi ya hapa kwenye safari zao za soka ambazo ndio kwanza zimeanza.

Lakii najaribu kujiuliza, nini kinafuata? Tubaki tu kujivunia kupitia watanzania wawili kati ya milioni arobaini tuliopo? Haiwezi kuwa hivi. Nchi inahitaji kuwa na ‘Samatta na Ulimwengu’ wengi zaidi. Hapa ndipo tutaweza kuwa na shangwe endelevu kwenye mchezo wa soka.

Sasa nini kifanyike kuwapata hao ‘Samatta na Ulimwengu’ wengi zaidi? Hapa ndipo jitihada za makusudi zinapohitajika. Wachezaji wanaoweza kufikia mafanikio ya Samatta na Ulimwengu wapo wengi sana kwenye miji na vijiji mbalimbali nchini Tanzania lakini hawajapata nafasi ya kuonekana.

TFF inatakiwa kuwa mstari wa mbele na kuwekeza zaidi kwenye kuimarisha mifumo ya kuvitafuta na kuviendeleza vipaji kupitia ‘Football Academies’. Hatuwezi kufika popote tukiendelea kusubiri vipaji vionekane kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ama Ligi Daraja la Kwanza baada ya kuibuliwa na klabu shiriki.

Advertisement
Advertisement

Klabu zetu ni masikini hivyo hazina uwezo wa kuanzisha mradi mipana na endelevu ya kuibulia vipaji. Kazi hii inaweza kufanywa na TFF ambao taarifa fulani ya BBC ya mwaka 2013 iliwahi kudai kuwa shirikisho hilo ndilo tajiri kuliko shirikisho lolote la soka Afrika Mashariki.

Mpango wa kutafuta na kuendeleza vipaji vya soka ulioanzishwa na TFF mwaka 2008 ndio ulioibua kipaji cha Thomas Ulimwengu. Pengine usingekuwepo mradi huo uliofahamika kama ‘Tanzania Soccer Academy’ kipaji cha Ulimwengu kisingekuja kuonekana mbaka hii leo.

Ukiacha TFF pia makampuni na mashirika mbalimbali yenye uwezo wa kifedha ni vizuri yakawekeza kwenye miradi ya kutafuta na kukuza vipaji vya soka. Niwapongeze NSSF ambao Januari mwaka huu waliingia makubaliano na Real Madrid ya Hispania katika kujenga kituo cha kukuzia vipaji vya soka.

Kwa upande mwingine pia klabu zetu ziwezeshwe kwa kupewa udhamini mnono ili nazo ziweze kuwa na nguvu ya kuweza kuwaibua akina ‘Samatta na Ulimwengu’ wengine kupitia shule zao za kuendeleza vipaji.

African Lyon waliokitambulisha kipaji cha Samatta nchini Tanzania kupelekea mchezaji huyo kunyakuliwa na Simba wangeweza kuwaibua akina Samatta wengi kama wangekuwa na uwezo wa kifedha kuwawezesha kuvisaka na kuviendeleza vipaji hivyo kutoka kwenye maeneo mbali mbali ya nchi yetu.

Shule ya kukuzia vipaji ya Azam FC ‘Azam Academy’ ni mfano wa kuigwa ila haitaweza kuigwa na klabu nyingi kutokana na umasikini. Nisisitize tena umuhimu wa mashirika na makampuni yenye uwezo wa kifedha kujitolea kuzipa udhamini mnono klabu zetu.

Jambo lingine la kufanyika ni kupigana ili kuhakikisha timu yetu ya taifa inapiga hatua ili kuzivutia klabu kubwa za nje na mawakala wa soka kutoka huko kuanzisha miradi ya kutafuta na kuendeleza vipaji. Tukiendelea kuwa nyuma kwenye viwango vya FIFA hatutavutia uwekezaji wa namna hii.

Kwa ufupi tusiishie tu kujivunia mafanikio ya Samatta na Ulimwengu. Akina ‘Samatta na Ulimwengu’ wapo wengi mno kwenye miji na vijiji mbalimbali nchini. Mifumo endelevu na imara ya kutafuta na kuendeleza vipaji itawaibua wengi zaidi na tutajivunia zaidi.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

STARS YALAZIMISHWA SARE

Tanzania Sports

ULAYA YATIKISIKA: