in , , ,

TUNATAKA KUMZAMISHA SALAMBA KWA KOSA MOJA

Mengi Jana yalitokea, siku ilikuwa nzuri na kikubwa ilikuwa siku kubwa ambayo ilikuwa na tukio kubwa Tanzania.

Inawezekana sherehe ya wakulima Tanzania ni sherehe inayojulikana sana lakini tunakoelekea sherehe ya Simba Day itakuwa kubwa na itakuwa sherehe maalumu hapa Tanzania.

Ni dhambi kubwa sana kwa vidole vyangu kutoandika chochote kuhusiana na siku ya Simba.

Wengi wataandika, watatumia maneno bora na mazuri ya kupamba lakini kuna kitu kimoja tu ambacho akili yangu inaniambia nikiandike kwa hali ya udogo.

“Hongereni Simba”, maneno haya mawili yanatosha sana kuweka hitimisho la maneno mengi yatakayoandikwa kuhusiana na tamasha la Simba Day.

Tamasha hili ni kitabu bora ambacho kila kiongozi wa timu hapa Tanzania anatakiwa kusoma kila kurasa ya kitabu hiki kwa makini neno baada ya neno.

Kitabu hiki kimebeba chakula kikubwa cha akili, chakula ambacho kitaweza kunenenpesha akili kwa kuleta ubunifu mkubwa ndani ya klabu.

Ubunifu ambao utaviwezesha vilabu vyetu kutokuwa na urafiki wa njaa. Kwao wao watakuwa marafiki wakubwa wa raha.

Raha ambayo itahakikisha nembo ya klabu inakuwa imara kutokana na tamasha la siku ya klabu husika.

Kiutani utani Simba inaenda kuwa timu yenye nembo/chapa kubwa (Brand) hapa Tanzania kwa sababu ya tamasha hili ambalo walilifanya jana.

Wameuza jezi nyingi ni kitu kikubwa kwao, wameingiza mashabiki wengi uwanjani ni jambo la faraja kwao lakini kwangu mimi natazama jinsi ambavyo walivyofanikiwa kuuza hisia.

Hisia ndiyo kitu cha muhimu katika biashara yako. Biashara yoyote duniani ili ufanikiwe lazima uuze hisia.

Hapa ndipo walipofanikiwa Simba, Jana waliuza hisia. Kila mtaa ulitawaliwa na hisia za Simba, rangi pekee iliyokuwa imefunika hisia za watu jana ni rangi nyekundu.

Kila shabiki alikuwa na furaha kumuona kila mchezaji wa Simba, kwao wao ilikuwa Simba mpya. Simba ilikuwa ni mwanamke mpya aliyekuwa anavutia.

Ndiyo maana kila shabiki wa Simba alitamani jana Simba ishinde mechi ya jana kwa sababu hisia zao zilinunuliwa na Simba.

Ukamilifu wa hisia wao ulihitaji ushindi katika mechi ya jana.Kwao wao ile ilikuwa mechi yao ilikuwa lazima washinde.

Uwanja wao, jezi zao, mashabiki wao, pesa zao kwanini wasishinde? Ilikuwa lazima wapate ushindi ili furaha yao ikamilike.

Ndiyo maana hata Adam Salamba alipokosa penati lawama zote zilikuwa juu yake.

Alionekana katili, alikatili furaha ya mashabiki wengi kwa kifupi ni kwamba alikuwa muuaji wa hisia za watu jana.

Mazuri yote ya Adam Salamba yalisahaulika jana, hakuna aliyekuwa anakumbuka tambo ambazo alikuwa anazitoa kipindi ambacho Adam Salamba walikuwa wamemsajili.

Wamesahau kuwa huyu ndiye walimwimbia nyimbo za kuwa Mfalme wao katika pori la msimbazi.

Waliamini yeye atakuja kutoa furaha kubwa kwenye pori hili la Msimbazi, kibaya walisahau kitu kimoja, mwanadamu siku zote hawezi kuwa mkamilifu.

Makosa kaumbiwa mwanadamu, ni ngumu kuukwepa huu ukweli hata kama ni mchungu.

Walisahau kuwa mpira ni mchezo wa makosa na hakuna mchezaji asiyefanya makosa kwenye mpira hata siku moja.

Cristiano Ronaldo mara nyingi hufanya makosa mara nyingi tu lakini heshima yake hubaki pale pale kwa sababu mpira ni mchezo wa makosa.

Tushasahau kuwa Adam Salamba ni kijana mdogo, kijana ambaye anahitaji kupewa moyo kwa ajili ya kuendelea kukuza kipaji chake.

Mashabiki wana nafasi kubwa sana kujenga na kubomoa kipaji cha mchezaji. Wachezaji wetu hawana watu wa Saikolojia, watu ambao watakuwa wanajenga kiakili kipindi wanapopitia nyakati ngumu.

Tunawalazimishia wachezaji wetu kuwapitisha katika nyakati ngumu ilihali tunajua hakuna watu ambao wataweza kuwajenga wakiwa katika nyakati zao ngumu.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Tunawekeza Ubora wa Paa la Taifa Stars na kusahau Msingi

Tanzania Sports

Pazia EPL linafunguliwa