in , , ,

TUNASHINDWA KUUFANYA UWANJA WA TAIFA KAMA SEHEMU YA UTALII?

Mkapa Stadium

Kutengeneza hela ni sanaa, kufanya kazi ni sanaa ila kufanya biashara
ni sanaa kubwa zaidi

Kuna biashara nyingi sana kwenye tasnia ya michezo lakini hatujawahi
kuzifanya katika kiwango kikubwa cha ubora.

Ukawaida usio wa kawaida umetawala sana kwenye eneo hili la biashara
za michezo, ndiyo maana mafanikio yetu ya kawaida ndani na nje ya
uwanja.

Hatujawahi kuumizwa na utajiri wanaopata wenzetu kutokana na kufanya
biashara ndani ya tasnia ya michezo.

Tasnia ambayo ina idadi kubwa ya watu wanaoipenda na kuifuatilia,
idadi ambayo inatoa taswira halisi ya soko kubwa la biashara hili.

Soko ambalo tunalichukulia kawaida na kuliangalia tu siku ya mechi.

Tunategemea siku ya mechi ndiyo iwe siku ambayo tutatengeneza pesa
nyingi na kusahau kuwa hata kabla ya mechi tunaweza kutengeneza pesa
kupitia michezo.

Siku ya mechi ya Simba na Al Masry kuna mengi yalitokea, lakini moja
ya jambo ambalo lilinishtua binafsi na kunifanya niliangalie katika
upande tofauti na wengine walivyokuwa wanalitazama ni suala la
mashabiki kuingia kwenye eneo la kuchezea (pitch) na kuanza kuteleza
wakati mvua inaendelea kunyesha.

Inawezekana wengi wetu tulikemea tabia ile, hata mimi nilikemea kwa
sababu ni tabia mbaya ambayo inahatarisha afya ya uwanja wetu.

Tujiulize kitu kimoja, kukemea peke yake na kunyamaza kunatosha? ,
sawa tunaweza tukawa tumekemea na kuwafanya mashabiki wasirudie tena
tabia ile.

Je tunatakiwa kuishia kwenye kukemea tu ? Hivi hatukuona furaha
iliyokuwa imetanda kwenye nyuso za mashabiki wakati wanateleza kwenye
ule uwanja? tunafanya nini ili kuweka furaha ya kudumu kwenye nyuso za
mashabiki wale?

Kama watu wanapenda kitu watakusikiliza, lakini kama watu wanakuamini
watafanya biashara na wewe, kuna umuhimu mkubwa sana ya kujenga imani
kwa hawa watu ili waweze kufanya biashara na nyie.

Hapa kuna vitu viwili vya kufanya ili kuweka imani kubwa ndani ya watu
ili kutengeneza mazingira rafiki ya kibiashara

Cha kwanza, ni kuwakemea hao watu walioenda kwenye sehemu ya kuchezea
(pitch) na kuanza kucheza wakati mvua inanyesha

Eneo hilo la kuchezea (pitch) sportpesa wametumia bilioni 2
kutengeneza eneo la kuchezea (pitch) lenye hadhi ya kimataifa

Bila utunzaji mzuri wa hii pitch tutabaki kusema tuliwahi kuwa na
pitch ya hadhi ya juu ya kimataifa

Wasimamiza wa uwanja wanatakiwa waweke ulinzi ambao utalinda miundo
mbinu ya huu uwanja.

Jambo la pili, ni kuuendesha kibiashara huu uwanja. Ni wakati ambao
wasimamizi wa uwanja wasisubiri viingilio vya mechi kwa ajili ya
kupata pesa za utunzaji wa huu uwanja.

Kama ilivyojionesha kwenye mechi ya Simba na Al-Masry kuna watu wana
ndoto ya kukanyaga kwenye hiyo pitch. Kuna watu kutoka mikoani ndani
ndani huko ambao wanatamani kutoa tongotongo zao kwa kukanyaga hiyo
pitch , inabidi watengenezewe mazingira ya kibiashara, mazingira
ambayo yatawawezesha wao kuja kufanya utalii kwenye uwanja huo na
kukanyaga pitch kwa gharama elekezi.

Pia kunaweza kujengwa maktaba ya iliyo na machapisho ya wachezaji wetu
wa sasa na wazamani kuelezea historia yao. Mtu akija awe na uwezo wa
kupata historia ya Sunday Manara na wachezaji nyota wa zamani na sasa
akimaliza hapo aende kupiga picha kwenye pitch , ateleze apendavyo,
kuwepo na mipira ambayo ataitumia kupiga penalti akimaliza hapo aende
na kwenye majukwaa.

Kwenye makumbusho ya Taifa kuna vitabu na picha zinazohusu timu ya
taifa na wachezaji wa zamani pamoja na makombe ambayo Taifa Stars
iliwahi kushinda

Vitu kama hivi vinatakiwa vipelekwe pale Uwanja wa Taifa. Iwe chachu
ya utalii wa uwanja kuwepo na maktaba maalumu ya vitu hivyo.

Maktaba ambayo itakuwa mpaka na CD ambazo zitakuwa na mahojiano ya
wachezaji nyota wa zamani. Vijana wengi hawajui historia za wachezaji
wao wa sasa na zamani, tunatakiwa tuwatengenezee mazingira ya
kibiashara ili na wao wanufaike.

Kuna nyota wengi sana ambao walileta sifa kwenye taifa hili kwenye
michezo mbalimbali kama soka, riadha, ngumi na michezo mingine.

Watu wengi wanahamu ya kuwajua kiundani hawa watu waliofanya vizuri,
hivo kutengeneza mazingira mazuri ya watu mbalimbali kupata historia
zao itaongeza chachu ya watu kwenda kutalii kwenye uwanja wa taifa.

Pia hata kuwajengea sanamu za heshima na kuziweka kwenye maktaba
maalumu au nje ya uwanja itaongeza chachu ya watu kujivunia mashujaa
wao.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MOURINHO ANAMTAZAMA SANCHEZ SISI TUNAMWANGALIA

Tanzania Sports

Carragher na kashfa ya kutema mate