in , ,

TUMKUMBUSHENI SALAMBA KUHUSU BAHANUZI

Kongole Adam Salamba! Hili ndilo neno kubwa ambalo mimi nimechagua kuanza nalo kwenye makala yangu.

Makala ambayo naiandika kwa mapenzi makubwa na wewe na hii ni kwa sababu mimi ni shabiki mkubwa wa kipaji chako ukiachana na kwamba tumetoka mkoa mmoja wa Shinyanga.

Mkoa ambao unafamilia nyingi zenye maisha duni. Najua ulipo nyuma yako kuna macho ya watu wengi yanakutazama kama msaada mkubwa wa uchumi kwao.

Kuna wengi ambao ni ndugu zako wanaamini kabisa kuwepo kwako Simba ndiyo mwisho wa maisha magumu katika familia zao.

Siwezi kuwalaumu kwa sababu ujamaa ndiyo sera ambayo imetulea na kutukuza toka enzi za zamani.

Hatuwezi kuukwepa kwa sababu bado tunaamini ujamaa ndiyo sera bora tunayotakiwa kuishi nayo katoka ulimwengu huu wa kipebari.

Ulimwengu wenye ushindani mkubwa wa kiuchumi. Ushindani ambao unaanzia kwenye akili zetu (Ubunifu) mpaka kwenye maeneo ya kazi zetu.

Wengi hawataona ugumu unaopitia watakachobaki wanawaza akilini mwao ni namna gani ambavyo utawasaidia kwenye matatizo yao.

Hakuna atakayefikiria upo sehemu ambayo ina ushindani mkubwa was kuwa na  wachezaji wengi bora wa eneo la ushambuliaji.

Hakuna atakayefikiria jinsi unavyopambana kwa ajili ya kupata nafasi katika kikosi cha Simba ili uwasaidie walio nyuma yako.

Inawezekana kuwepo na watu nyuma ya Adam Salamba wanaomtegemea kunaweza kukawa sababu ya yeye kupigana kila uchwao katika maisha yake ya mpira.

Hatutakiwi kutumia muda wetu kwa sasa kumsifia kwa hiki alichokifanya jana kwenye kombe la Kagame. Busara itumike kumwambia kwamba yuko katika ulimwengu wa kipebari, ulimwengu wenye ushindani mkubwa.

Ulimwengu ambao Emmanuel Okwi hatamani kuanzia benchi. Ndiyo ulimwengu huo huo ambao unamfanya John Bocco kuwa mshanbuliaji chaguo la kwanza katika kikosi cha Simba.

Ndiyo ulimwengu ambao umewaleta Marcel Kaheza na Mohammed Hussein pale Simba. Ndiyo ulimwengu ambao uliwafanya Simba waende Kenya kumsajili Kagere bila kujali wana wachezaji wengi wa eneo la ushambuliaji.

Huu ndiyo ulimwengu ambao hutakiwi kuushangaa kwa sababu bila juhudi huwezi kufanikiwa. Mafanikio hayaji kwa kuzubaa au kuridhika na hatua moja ya jana.

Hatua ya jana inatakiwa ikukumbushe kuwa una hatua mia zilizobaki kufikia kilele cha mafanikio. 

Ndiyo ulimwengu huu ambao watu wengi wanapenda kusema “makosa ni mwalimu mzuri” na walimwengu hupenda kusisitiza ni muhimu kujifunza kupitia makosa yetu au makosa ambayo wenzetu huyafanya katika hatua zao za kupanda ngazi za mafanikio.

Ndiyo maana jana kila wakati nilipokuwa namuona Adam Salamba nilikuwa namkumbuka Said Bahanuzi, mchezaji aliyewahi kuwa  mfungaji bora wa mashindano ya Kagame Cup.

Mashindano ambayo yalimfanya awe mfalme wa mashindano yale. Kila camera ilitamani picha yake, kila gazeti lilitazamani kuandika kwa sifa jina lake mbele ya gazeti kwa sababu kwa wakati huo macho mengi yalitamani kumsoma yeye tu.

Hata masikio yetu yalitamani kumsikia yeye, kitu kilichofanya waandaji wa vipindi vya redio kuandaa habari ya kwanza kuwa ya Said Bahanuzi.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa yeye kupotea njia. Alisahau ni wapi alitakiwa kwenda na hatua muda alipokumbuka muda ulikuwa umeenda na mwisho wa siku taifa likawa limepoteza kipaji kikubwa sana.

Leo hii tusishiriki katika hatua ya kumpoteza njia Adam Salamba. Tunatakiwa kumkumbusha huku mikono yetu ikiwa nyuma ili tujihadhari na kumpigia makofi yetu ambayo yatampoteza njia.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

RONALDO NA MESSI WATAISHI KWENYE VITABU VYA KINA PUSKAS

Tanzania Sports

Ubelgiji: Kizazi cha dhahabu