in

Tuisila Kisinda ‘TK Master’ zali la mawinga wa Yanga

Tuisila Kisinda

Maelfu ya mashabiki waliohudhuria uwanja wa Nakivubo nchini Uganda kushuhudia mashindano ya Klabu Bingwa Afrika mashariki mwaka 1999 wanalikumbuka jina la Edibily Lunyamila. Mashabiki wa Express na SC Villa za Uganda wanalifahamu jina la Yanga. Wanaukumbuka mguu wa kushoto wa Lunyamila ulivyowanyanyasa nchini humo.

Mamia ya mashabiki waliohuduhuria mechi za aina hiyo kwenye uwanja wa Nyayo nchini Kenya nako wanalifahamu jina la Lunyamila. Si kwenye mashindano ya Chalenji tu hata klabu bingwa Afrika mashariki na Kati nako ni habari ileile. Haikuwa Express au SC Villa pekee hadi Kenya Breweries walifahamu umahiri wa nyota huyo.

Mashabiki wa soka Sudan wanalifahamu jina la Mrisho Ngassa. Wanakumbuka namna winga huyo alivyowanyanyasa chini ya kocha Marcio Maximo. Wanakumbuka namna kasi yake ilivyowasumbua mabeki wao kwenye chalenji na mashindano ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika, AFCON. 

Mashabiki wa Angola wanafahamu kasi ya winga machachari Said Maulid. Mashabiki wa Rwanda, Burundi,Uganda na Kenya hadi Sudan wanafahamu namna Said Maulid alivyosumbua timu zao. 

Ukiangalia kikosi cha kocha Cedric Kaze wa Yanga utaona Tuisila Kisinda ni winga ambaye anachachafya ngome ya wapinzani. Kasi yake imekuwa habari nyingine. Mabeki wa Simba wanafahamu namna winga huyo alivyomsumbua kitasa wao Joash Onyango na kusababisha penalti kwenye mchezo wa Ligi Kuu baina ya watani hao wa jadi. 

Onyango alikumbana na kasi ambayo alishindwa kuimudu, ikabidi amfanyie madhambi Tuisila Kisinda hivyo mwamuzi kutoa adhabu ya penalti. Tukio hilo ni miongoni mwa yale ambayo TK Master amekuwa akiyafanya ndani ya kikosi cha Yanga. 

Hivi kaaribuni kwenye mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting, TK Master aliwaburuza mabeki wao na kusababisha kile mashabiki wa soka wanachokiita ‘mbilinge’. Yaani mchezaji anawachachafya na kuwakimbiza mabeki wa timu pinzani kiasi kwamba wanashindwa mbinu za kumdhibiti. 

TK Master ni mchezaji ambaye anampa kocha kitu kizuri, kupunguza nguvu ya wapinzani kwa kuwachosha mabeki wao hivyo kulazimika kumchunga zaidi yeye kuliko wengine. 

Makocha wa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara wanapokutana na Yanga hatua ya kwanza ni kupanga mbinu za kumdhibiti TK Master na wazalishaji wanaosababisha kasi yake. wanatafuta namna ya kupunguza makosa ambayo yanahatarisha timu zao, kw avike kasi yake huchangia mabeki kumchezea faulo hali ambayo wanaadhibiwa na waamuzi.

HAPA NDIPO ILIPO SIRI YA YANGA

Uhalisi wa mambo unaonyesha kuwa mabingwa wa zamani wa soka Yanga wamebahatika kuwa na mawinga wazuri na wenye kasi kila nyakati. Katika maisha ya soka ya Yanga wamewahi kuwa na mawinga wakali na wenye vipaji vya hali ya juu kama vile Selestine Sikinde Mbunga, Akida Makunda, Edibily Lunyamili, Simon Msuva, Said Maulid, Mrisho Ngassa na Shamte Ally kwa kuwataja wachache.

Shamte Ally alijiunga na Yanga akitokea Kagera Sugar  wakati ilipokuwa inafundishwa na Kocha Sylvester Marsh. Alikuwa mahiri wa kutumia mguu wa kushoto na uwezo mkubwa wa kupiga mashuti makali na faulo. Shamte Ally niliupenda uwezo wake wa soka ingawa alipohamia Yanga hakudumu kutokana na majeraha aliyoyapata. 

Kwangu mimi kama kipaji Shamte Ally alikuwa bora kuliko winga mwingine wa sasa Deus Kaseke. Kifundi namkubali Shamte Ally. Hata kama tunaweza kuchambua udhaifu wa kila mmoja katika mfumo wowote ule Shamte Ally alikuwa mahiri katika jicho la kiufundi hasa pale kocha anapohitaji kitu cha ziada kutoka kwa mchezaji. Kipaji chake ndicho kingeweza kumpa nafasi kubwa kwenye kandanda.  

Kwa kutumia mfumo mfumo 3-4-3 Shamte Ally alikuwa mchezaji mzuri ambaye hakupata wasaa wa kutosha kutamba katika soka Yanga. Ni mzuri kawernye mashambulizi ya kushtukiza,mashuti,muono wake na jinsi alivyocheza alikuwa ananivutia sana. 

Mawinga wengine niliowataja hapo juu wamecheza nyakati tofauti pale Yanga. Ninachosema ni kwamba kila nyakati Yanga wamekuwa na bahati ya kuwa na mawinga wazuri. Sisemi winga huyu ni mzuri kuliko mwingine. Ninachosisitiza Yanga wamekuwa wakipata mawinga wazuri kila nyakati. Shamte Ally alipewa jina la B52  kwa sababu ya uwezo wake wa kupiga mashuti na spidi. 

TK Master naye anapita mulemule ambako walipita akina Shamte Ally, Said Maulid, Mrisho Ngassa,Lunyamila,Makunda na wengine. Kwamba kwenye eneo la winga Yanga wamekuwa na bahati mno kuwa na wachezaji wenye kuvutia kuwatazama, kasi na vishindo vyao huwa ni hatari kwa timu pinzani. Kwa TK Master kasi yake inaweza ‘kuwatapisha damu’ mabeki wa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kama wasemavyo wahenga kuwa historia inajirudia, bila shaka kwa Yanga historia yao itajirudia mara nyingi zaidi. Hadi kumpata TK Master ni ushahidi anapita mulemule mwa mawinga wakali waliowahi kuichezea Yanga. Na historia itajirudi miaka na miaka hata TK Master akiondoka klabuni hapo.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Hekaheka za EPL mwishoni mwa wiki

Taratibu shangwe zinarejea viwanjani

Michael Sarpong

Sarpong anaweza kuyakuta mabegi yake ‘Airport’