in , , ,

TUIPE KWANZA YANGA KIOO IJITAZAME

Inawezekana umri alionao Yanga haujui, na inawezekana kabisa bado anajiona ni mtoto mdogo, mtoto ambaye anategemea kila kitu kutoka kwa wazazi.

Hata hela ya nguo za ndani inatoka mfukoni wa wazazi wake bila kuangalia kwa muda huu siyo muda mzuri kwake yeye kuendelea kumtegemea mzazi wake.

Na inawezekana kabisa Yanga hajui kama ni masikini na kama anajua basi haumizwi na umasikini wake. Kwake yeye anaona umasikini ni kitu cha kawaida. Hafikirii hata kidogo jinsi ya kutoka kwenye umasikini, mawazo yake yote yapo kwenye namna ambavyo wazazi wake wanaweza kutumia muda mrefu kumtunza.

Umri wa miaka 83 hana nyumba, hana mke, hana kiwanja hana hata chombo chochote cha ndani. Hata benki hakuna akiba yoyote ambayo itamfanya atatue matatizo yake zaidi ya yeye kutegemea pesa za mfukoni mwa wadau.

Wadau ambao siku zote huwa hawadumu milele, leo hii watakuwa na hela kesho hawatokuwa na hela na maisha yanakuwa magumu kwako kwa sababu hakuna msingi wowote ambao uliujenga kwa ajili ya kujitegemea.

Kujitegemea ambako kunatengenezwa na kiongozi bora, imara na mwenye maono kuhusu familia.

Leo hii familia ya Yanga imekosa watu wenye maono ya kuiwezesha Yanga kujitegemea yenyewe bila kutegemea pesa za wadau.

Hata jina “Yanga” hawaoni kama ni jina ambalo linamtaji mkubwa sana kwao. Tumekuwa kila siku tukiongea na kuishauri Yanga na timu zingine hapa nchini namna ya kutumia nembo zao kibiashara.

Somo ambalo tumeliandika sana mpaka mikono yetu imegeuka kuwa na sugu, ndimi zetu zimeongea sana lakini mwisho wa siku masikio yao wameweka kufuli.

Hawataki kutusikia, hata kutusoma pia huwa wanatupuuzia mwisho wa siku wao hugeuka kutapa tapa kipindi mambo yanapokwenda kombo.

Leo hii Yanga imekosa ni upande gani wa dunia ni sahihi kwao wao kutazama ili walione jua. Wamekuwa wakigeuka kila upande kwa tumaini ya kuliona jua na kusahau kuwa jua lilizaliwa mashariki na kuzikwa magharibi.

Kwao wao bado wanaamini hata  Kaskazini na Kusini kuna jua. Ndiyo maana wanarudia kufanya vitu vile vile katika mtindo ule ule ambao ulisababisha wao washindwe awali.

Leo hii Yanga imeamua kuanza utaratibu wa kuwahamasisha wanachama, wapenzi wa Yanga kuchangia kiasi cha Pesa kwa ajili ya maandalizi ya timu.

Wazo ambalo ni zuri kwa sababu kila mwanachama na mpenzi wa timu fulani huwa ni mtu wa kwanza kuchangia maendeleo ya timu husika.

Na wazo hili lilikuwepo awali kipindi ambacho aliyekuwa katibu mkuu wa Yanga Boniface Mkwasa alisimamia utaratibu huu lakini haukuunufaisha timu kwa kiwango kikubwa.

Leo hii utaratibu umerudi tena, tumefikiria ni kwanini awali utaratibu huu haukuwa na mafanikio makubwa?

Ni wapi kina Boniface Mkwasa walipokosea? na kipi wamekifanya ili kuepukana na makosa ya kina Boniface Mkwasa?

Moja ya vitu ambavyo wengi huwa tunakipuuzia ni mahusiano ya kijamii “Public Relation”. Kwenye biashara yoyote ile ambayo mfanyabiashara huifanya lazima ahakikishe bidhaa yake na jamii husika ina mahusiano mazuri.

Hata siku ambayo mfanyabiashara huyo atakapoleta bidhaa nyingine itamlazimu tena atangeneza mazingira ambayo yatatengeneza urafiki kati ya bidhaa mpya na mteja. Mteja anatakiwa aielewe ipasavyo bidhaa hiyo na anatakiwa awekewe mazingira ambayo yatamsababisha atoe pesa yake kwa ajili ya kununua bidhaa hiyo.

Bidhaa nyingi za Yanga zimekuwa hazina uhusiano mzuri na jamii licha ya kwamba Yanga inawapenzi wengi. Kuwa na wapenzi wengi pekee haitoshi kumshawishi mtu kununua bidhaa yako ila kuna njia ya ziada ambayo inahitajika kumshawishi mtu aweke mkono wake mfukoni kutoa pesa yake kwa ajili ya kununua bidhaa yako.

Yanga waliingia utaratibu na mtandao mmoja wa mawasiliano hapa nchini kwa ajili ya mwanachama kujipatia habari za klabu kwa kiasi cha shilingi mia.

Wazo lilikuwa zuri lakini hakukuwepo na mazingira ya kulitangaza na kuliweka vichwani mwa wanachama hilo wazo. Nguvu ya kutengeneza mahusiano kati ya wazo lao na jamii ilikuwa ndogo.

Leo hii wanatembea katika mwendo huo huo , wanatengeneza utaratibu wa mwanachama kuichangia timu, lakini hawajatengeneza mazingira ya kumwelimisha zaidi mwanachama mpaka ahamasike kutoa pesa yake mfukoni kwa ajili ya kuichangia timu.

Kungetengenezwa kampeni kubwa hata yenye jina la “Mikono yangu Imara itaijenga Yanga Imara” kampeni ambayo ingesambaa nchi nzima kila tawi litembelewe na waelimishaji wa kampeni hii ili kila mwanachama aone kuwa ana nafasi kubwa ya kuijenga Yanga kwa mikono yake.

Kila mwanachama ajivunie kumlipa mshahara Mrisho Ngassa. Hii itasaidia na hii inaweza kutumika kama njia ya muda mfupi kuwapitisha katika matatizo yao.

Hata njia ya kupata habari za klabu kwa njia ya siku iboreshwe na iwe njia endelevu. Mfano kama wakifikiria kuongeza kipengele cha mashabiki kujibu maswali kuhusu Yanga kupitia ujumbe mfupi wa simu ambapo kuwe na alama kwa kila anayejibu kwa ufasaha na mwisho wa mwezi kuwe kunatoka zawadi kama jezi kwa washindi hamsini bora na washindi kumi bora wawe wanapewa tiketi ya kuangalia mechi ya kila mwisho wa mwezi. Utaratibu huu utawahamasisha wengi kushiriki kuichangia timu kupitia kujibu maswali yanayohusu klabu kupitia ujumbe wa simu kwa sababu wanajua kuwa mwisho wa mwezi watapewa zawadi.

Kuwepo na utaratibu wa kuchat na wachezaji husika kupitia namba maalumu ya kibiashara. Shabiki anakuwa na uwezo wa kuchat na Papy “Kabamba” Tshishimbi au mchezaji yoyote. Na hii ifanyike kwa viongozi kutenga siku moja kwa wiki kwa ajili ya zoezi hili. Gharama zitakazotumika kuchat na hawa wachezaji wa Yanga zitatumika kuisaidia Yanga.

Tatizo linakuja pale pale Yanga bado inajiona ina umri mdogo ndiyo maana inalilia kulelewa na wadau na kusahau kuwa umri umeenda na inatakiwa kujitegemea, labda kioo hiki nilichowapa kujitazamia wataona makunyazi yao na watashituka kuwa uzee umeshawavaa mwili mzima.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Ronaldo tumuelewe tu jamani amesoma alama za nyakati

Tanzania Sports

CANNAVARO, UDONGO TUNAOENDA KUUPUZIA