in , ,

Tuanze kumuonea huruma kwanza Ajib au Yanga ?

Ibrahim Ajibu Yanga

Rudia tena swali, kisha njoo hapa tutafakari kwa pamoja. Yupi anahitaji huruma yetu kati ya hawa wawili? Huduma yetu ianzie kwa Ibrahim Ajib au kwenye klabu ya Yanga?

Ibrahim Ajib amekuwa mchezaji rafiki na benchi tofauti kabisa na msimu uliopita ambapo alikuwa na urafiki mkubwa sana na nyasi za viwanja vya mpira wa miguu ya ligi kuu Tanzania bara.

Aliisaidia Yanga goigoi, akaibeba kwenye mabega yake, akakimbia nayo bila kuchoka, akawa anafunga Lakini kazi kubwa kwake ilikuwa kupiga pasi za mwisho za magoli.

Leo hii hadithi ni tofauti kabisa, Ibrahim Ajib ambaye alikuwa anapata nafasi kubwa kwenye klabu ya Yanga msimu uliopita nafasi hiyo haipo tena kwenye klabu ya Simba msimu huu.

Mimi nitabaki nikiamini Ibrahim Ajib ni moja ya wachezaji bora kuwahi kutokea kwenye nchi yetu, wachezaji ambao wanastahili kupata nafasi kubwa ya kucheza kuliko nafasi kubwa ya kukaa benchi.

Nina imani kubwa sana na miguu ya Ibrahim Ajib Lakini sina imani kubwa na moyo wake. Moyo wake hauna tamaa ya kujituma zaidi. Hatamani kuyafikia mafanikio makubwa.

Kwake yeye alipo ndipo anapoamini amefika. Kuna wakati huwa natamani Ibrahim Ajib awe sehemu fulani kubwa Lakini yeye hujiona anafaa kuwa hiyo sehemu aliyopo sasa hivi.

Hataki mabadiliko kwenye maisha yake. Hataki kupiga hatua za kwenda mbele yeye huzitamani hatua za kurudi nyuma ndiyo maana alikataa kwenda TP Mazembe na kurudi Simba.

Simba ambako hapati nafasi, miguu yake inaliwa na mchwa uliopo kwenye mbao alizokalia. Naumia sana kila nikimuona akiwepo amekaa kwenye benchi wakati anauwezo wa kusimama na kwenda uwanjani.

Lakini moyo wa kuisikuma miguu yake haupo, sijui moyo huu haupo tena pia kwenye klabu ya Yanga? Mechi nne mfululizo wanapata sare kwenye ligi kuu ya Tanzania bara.

Sare ambayo inawaweka mbali na taji la ligi kuu. Ni ngumu sana kwao wao kwa sasa kufikiria taji la ligi kuu ya Tanzania bara kwa sasa hivi, alama 21 nyuma na anayeongoza ligi.

Hawa kosa walianza kulifanya baada ya kumtoa Mwinyi Zahera, walipoamua kuwaacha wachezaji wengi na kusajili wachezaji wengine wengi wapya kwenye kikosi.

Tena ugumu walisajiliwa katikati ya ligi kuu, akaletwa na kocha mpya, kocha ambaye hawajui vizuri wachezaji alioletewa. Kazi ya kwanza ikawa kujuana wao kwa wao.

Kazi ambao huchukua muda mrefu kukamilika, na kwa bahati mbaya zoezi hili la kujuana hutumika kwenye pre-season (maandalizi ya ligi ) Lakini kwa bahati mbaya wakawa wanalifanya katikati ya ligi.

Mzoeane, muelewane mbinu alafu ndiyo mcheze kwa pamoja? lilikuwa zoezi gumu ambalo lilihitaji muda mrefu ili kupata wepesi wake. Wanachokipata sasa hivi Yanga ni matokeo ya walichokifanya kwenye dirisha dogo.

Kufukuza wachezaji wengi na kocha afu ukaongeza wachezaji wengine wapya na kocha mpya katikati ya msimu ukitegemea unaweza ukafanya vizuri, ni ngumu hili kutokea.

Ukiwatazama Ibrahim Ajib na Yanga utagundua wote wanafanya makosa ambayo mioyo yao iliamua kuyafanya huku wakijua kuwa ni kosa. Swali kubwa linabaki nani tuanze kumhurumia kati yao?

Tumhurumie huyu ambaye hataki kabisa kujituma na kuwa na njaa ya kufikia mafanikio makubwa, mafanikio ambayo yanaendana na ubora/ ukubwa wa miguu yake? au tumhurumie huyu aliyesajili wachezaji wapya wengi na kocha mpya katikati ya ligi akitegemea mafanikio makubwa ?

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Mabingwa Ulaya sasa patamu

Tanzania Sports

Corona inavyoharibu utamu wa michezo