in

Tuanze kumuomba samahani Onyango!

Yanga Vs Simba

Usajili wake ulipofanyika kitu kikubwa ambacho kilikuwa kinazungumzwa ni umri wake kuonenkana kuwa mkubwa jambo lilipelekea watu wengi tumwiite “Babu”.

Tulimuita “Babu” na kumuona kama mchezaji ambaye hataendana na kasi ya mpira wetu. Tulimuita “Babu” na kumuona kama mchezaji ambaye hatotimiza majukumu yake ya ulinzi ipasavyo.

Tulimuita “Babu” na kufikia hitimisho kuwa Simba wamesajili mlinzi ambaye hatokuwa na faida kubwa katika kikosi chao cha kwanza. Mahitaji ya Simba tuliyaona ni makubwa kuliko uwezo wa Joash Onyango.

Tuliona Simba wanahitaji mlinzi wa kati ambaye angeendana na matamanio yao makubwa ya kufika mbali katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.

Simba walikuwa na picha kubwa sana ya ndoto yao. Ndoto ya kushindana na vilabu vikubwa barani Afrika kama TP Mazembe, Zamaleki, Mamelodi Sundown na vilabu vingine vingi.

Kwetu sisi tuliokuwa tunasikia ndoto hii ya Simba vichwani mwetu tulikuwa na aina ya wachezaji ambao Simba walitakiwa kuwa nao ili kuyafikia matamanio yao.

Tuliona Simba inahitaji wachezaji wa kiwango kikubwa kwenye kila idara. Michuano ya klabu bingwa barani Afrika mara nyingi huamiliwa na ubora wa wachezaji walio ndani ya kikosi husika.

Wachezaji hawa kuna wakati hutumia uwezo wao mkubwa kama kitu kitu cha ziada kuibeba timu baada ya mbinu za mwalimu kuonekana kutotoa matokeo ambayo ni mazuri.

Tuliiona Simba inahitaji mabeki imara , viungo bora na washambuliaji ambao ni bora ili wao kuyafikia matamanio yao ya kila siku waliyokuwa wanapenda kuyahubiri.

Usajili wa Joash ulionekana ni usajili ambao haukidhi mahitaji halisi ya klabu ya Simba kwa wakati huu. Joash Onyango alionekana ni beki mwenye umri mkubwa.

Umri ambao ungeleta kikwazo juu ya kasi yake uwanjani. Kumbuka michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika ina wachezaji wengi ambao ni bora.

Wachezaji ambao wana kasi kubwa sana uwanjani. Swali kubwa lilikuwa ni jinsi gani ambavyo Joash Onyango angeweza kuwadhibiti wachezaji hawa wenye kasi kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.

Mpaka sasa hivi Simba imefanikiwa kuingia kwenye hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika. Imeingia kwa kuzitoa timu ambazo zinatoka sehemu ambayo kuna maendeleo makubwa ya mpira.

Mechi ya kwanza ya Simba walicheza nchini Nigeria, pamoja na kucheza ugenini lakini walifanikiwa kutoka na ushindi kwenye mechi hiyo huku safu ya ulinzi ya Simba chini ya Joash Onyango ikisimama imara bila kuruhusu goli.

Hata kwenye mechi ya pili ya marudiano iliyochezwa hapa Dar es Salaam safu ya ulinzi ya Simba chini ya Joash Onyango haikuruhusu goli la aina yoyote .

Mpaka Simba wamefanikiwa kuingia kwenye hatua ya makundi barani Afrika wameruhusu goli moja kwenye mechi nne. Ukuta wao ukiwa chini ya Joash Onyango, mchezaji ambaye awali tulimsema ni mzee hana uwezo mkubwa wa kulinda kutokana na umri wake.

Tuachane na michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, turudi kwenye ligi kuu ya Vodacom. Simba ndiyo timu ambayo mpaka sasa imefungwa goli chache sana ukilinganisha na timu zingine , kumbuka Simba iko chini ya ukuta wa Joash Onyango tuliyemuita mzee.

Jana kulikuwa na fainali ya kombe la mapinduzi ya Zanzibar. Fainali ambayo iliwakutanisha Simba na Yanga, achana na matokeo ya fainali hiyo, tuzungumzie kiwango cha Joash Onyango. Jana alisimama imara kuilinda safu ya ulinzi ya Simba pamoja na kumsema kuwa ana umri mkubwa. Mimi nasimama kama mtu wa kwanza kumuomba msamaha Joash Onyango, namuomba anisamehe .

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Patrick Aussems

Natamani kocha wa Simba awe PATRICK AUSSEMS

Chikwende

Ujio wa Chikwende ndiyo mwisho wa Morrison?