in , ,

Tuanze kumlaumu Mwigulu kwenye kifo cha Singida United ?

Magoli ya Meddie

Kumbukumbu zangu zinanirudisha nyuma mpaka msimu juzi, msimu wa mwaka 2017/2018, msimu ambao ligi yetu ya Tanzania bara ilipokea zawadi ya kuwa na Singida United.

Timu ambayo awali ilikuwa inaonekana ni timu yenye mipango dhabiti ya kufika mbele, timu ambayo viongozi wake walionekana ni viongozi ambao wanatazama kesho na siyo Leo.

Timu ambayo ilionekana kuwa na mipango dhabiti katika uendeshaji wa timu yao, kuna sehemu ambazo vilabu vingi vilivyokuwa kwenye ligi kuu awali vilikuwa haviwezi kufika lakini Singida United ilifanikiwa kufika.

Ndiyo timu pekee ambayo ilikuwa na wadhamini wengi kwenye msimu huo wa mwaka 2017/2018. Hapa ndipo watu wengi tulianza kushtuka na kuanza kuitazama Singida United katika jicho la tofauti.

Swali kubwa ambalo lilikuwa linatembea vichwani mwetu ni namna ambavyo Singida United ilivyopanda ligi kwenye msimu huo na wakafanikiwa kupata wadhamini wengi kitu ambacho hakikuwepo awali kwenye vilabu vingine.

Mbinu gani walitumia kufanikisha hawa wadhamini wawe sehemu ya timu? ukizingatia ilikuwa timu ambayo ndiyo ilikuwa imepanda ligi kuu kwa mara ya kwanza gains ushawahi mkubwa wa mashabiki, mashabiki ambao ndiyo wateja wa kununua bidhaa za wadhamini.

Lakini wao walifanikiwa kupata majibu katikati ya msitu mkubwa wa maswali yetu. Wakapata pesa , wakasajili kikosi cha kushindania ubingwa, wakaleta kocha wa ubingwa na mwisho wa siku wakawa wanalipa mishahara ya kibingwa.

Wengi tukawa tunaitazama Singida United kama ni moja ya timu ambayo ilikuja kuingia katikati ya Simba na Yanga ili kuleta ushindani kwa hawa mafahari wawili wakubwa kwenye mpira wetu.

Swali kubwa lililokuwa limebaki vichwani mwetu ni moja tu, wataendelea kusimama hivi mpaka lini? wanaweza kuhimili mawimbi makubwa ya bahari ya ligi kuu Tanzania bara mpaka lini?

Swali ambalo halikuchukua muda mrefu likapata jibu, ndani ya msimu mmoja jibu tukaliona. Singida United ikatoka kuwa timu ambayo ilikuwa na uwezo wa kushindania kombe mpaka kuwa timu ambayo ilikuwa inapambana kutokushuka daraja.

Wadhamini wakapulizwa na upepo, wakapepea kuelekea sehemu ambayo palikuwa hapajulikani na Singida United ikabaki na miguu tu inayokanyaga popote baada ya kichwa kukatwa.

Akakosekana tena kiongozi ambaye angeweza kuwa na maono ya kuona mbali. Akakosekana tena mtu ambaye angeweza kuwashawishi wadhamini waje kuwekeza pesa kwenye klabu hii na kwa bahati mbaya hata viongozi wakaingiza siasa za Simba na Yanga.

Singida United ikaanza kuonekana kama tawi la Yanga. Kiongozi wa Singida United alikuwa tayari kuisajilia Yanga mchezaji mzuri na kuiacha Singida United ikiwa haina wachezaji wazuri.

Mpasuko ukawa mgeni rasmi kwenye makao makuu ya Singida United. Umoja ukaanza kuhesabu hatua za kuondoka kwenye jengo kuu la Singida United. Hakuna aliyebaki kama mhimili kwenye klabu.

Leo hii Singida United inacheza mechi bila ya daktari wa timu. Kutokuwepo kwa daktari na vifaa tiba vya michezo ndani ya timu hii inatosha kukuonesha kuwa ndani ya Singida United maisha ni magumu.

Wachezaji hawana motisha wanachosubiria ni wao ligi iishe na waanze kupiga mahesabu ya namna ya kucheza ligi daraja la kwanza. Inauma kuona timu ambayo ilikuwa inaonekana na mipango dhabiti.

Timu ambayo ilikuwa na wadhamini tisa kwenye ligi kuu , leo hii hawana hata mmoja na wanakoelekea ni kaburini. Swali kubwa linalobaki hapa ni kina Mheshimiwa Mwigulu Nchemba wanasehemu ya kulaumiwa kwenye kifo hiki cha Singida United?

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Liverpool: Machungu kuvuliwa ubingwa UCL

Tanzania Sports

Mvutano Corona soka ya EPL