in

Tuachane na kina Morrison tuwekeze kwa kina Miraji Athumani

Miraji

Simba kwa sasa inazidi kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya mashindano ya ligi ya mabingwa barani Afrika ambapo wamefanikiwa kufika katika hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Hatua hii ni ngumu sana kama huna aina ya wachezaji ambao ni bora katika kikosi chako ndiyo maana Simba kwa sasa inatumia muda mwingi kusajili wachezaji wa nje kwa ajili ya kujiimarisha.

Wamemsajili Doxa Gikanji kutoka DRC Congo. Wamemleta Taddeo Lwanga kutoka Uganda na Perfect Chikwende kutoka Zimbambwe. Sajili zote hizi lengo lake ni kujiimarisha kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.

Kuna kitu kimoja ambacho ni tahadhali. Wachezaji hawa wa kigeni wanakuja kwenye kikosi cha Simba huku kukiwa na hatari ya baadhi ya wachezaji wa ndani kuhatarisha nafasi zao.

Kitu hiki ni kawaida kabisa kwenye ulimwengu wa ushindani. Kwenye ulimwengu huu unatakiwa kupambana ili kushinda nafasi ambayo unaitamani kuifikia.

Lakini kuna kitu kimoja ambacho tunatakiwa kukitazama kwa undani wakati tunasajili hawa wachezaji wa kigeni. Asilimia kubwa ya wachezaji hawa wa kigeni huwa wanakuwa na kiwango ambacho ni cha kawaida.

Kiwango ambacho kinaweza kupatikana kwenye miguu ya wachezaji wetu wazawa. Kwa bahati mbaya wachezaji hawa wageni hupewa mshahara mnono, marupurupu mazuri kuzidi wachezaji wetu wazawa.

Kuna wakati huwa nawaza. Hivi vilabu vyetu haviwezi kuwekeza kwa wachezaji wazawa ambao wana vipaji vizuri tu vinavyolingana na baadhi ya wachezaji wa kigeni ambao huja kama wachezaji wa kulipwa?

Kuna uwekezaji unatakiwa kuwekwa kwa baadhi ya wachezaji wetu wa ndani. Wapewe pesa nzuri kwenye mshahara na marupurupu kama ambavyo wachezaji wengine wa kigeni wanavyopata.

Naamini wakipewa kiasi kikubwa cha pesa kuna kitu ambacho kinaweza kuongezeka kwenye viwango vyao uwanjani. Tatizo letu linaanzia pale tunapoamua kusajili kwa mihemko kisa cha mchezaji fulani katoka nje .

Bernard Morrison hakuwa na kikubwa cha ziada kumzidi Hassan Dilunga au Miraji Athumani. Miraji Athumani akipewa nafasi kubwa kwenye kikosi , akapewa pesa nzuri kwenye mshahara wake kama ambavyo anapata Bernard Morrison anaweza kuonesha makubwa ambayo Bernard Morrison ameshindwa.

Kuwaleta kina Bernard Morrison kwenye ligi yetu kunatoa nafasi kubwa ya kudidimiza viwango vya kina Hassan Dilunga na Miraji Athumani.

Leo hii tunaumia kwa kutokuwa na wachezaji bora kwenye kikosi cha CHAN kwa sababu kina Miraji Athumani hatuwapi nafasi kubwa kwenye vilabu vyetu kuanzia kwenye nafasi ya pesa mpaka nafasi ndani ya uwanja.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Bado tunamhitaji Chama timu ya Taifa

Ndayiragije

Makocha wa Burundi wanatoa somo gani kwa wazawa?