TP Mazembe wafalme

 

Mtanzania Mbwana Samatta amewawezesha TP Mazembe wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kutwaa ubingwa wa Afrika.

Mchango mkubwa wa Samatta ulikuwa bao lake la kwanza kwenye mechi ya mkondo wa pili kama ilivyokuwa kwa ile ya mkondo wa kwanza dhidi ya USM Alger ya Algeria.

Wafalme hao wapya miongoni mwa klabu za Afrika walitangazwa Jumapili hii baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mechi iliyopigwa katika uwanja wao wa nyumbani jijini Lubumbashi.

Bao la Samatta lilikuwa kwa njia ya penati na la pili likatiwa kimiani na raia wa Ivory Coast, Roger Assale na kuwaacha washabiki wao wakishangilia kwa nguvu, kwani walijihakikishia ushindi wa uwiano wa mabao 4-1. Kwenye mechi ya kwanza walishinda 2-1.

Samatta alitanzua hali katika dakika ya 75 akiwainua vitini washabiki kwa penati yake ya kifundi iliyotolewa baada ya Zinedine Ferhat kumchezea vibaya Roger Assale. Hilo lilikuwa bao la saba kwa Samatta na sasa ndiye ameibuka mfungaji bora wa mashindano hayo sambamba na Bakry ‘Al Medina’ Babiker wa Al Merrikh wa Sudan.

Advertisement
Advertisement

Assale alitia bao la pili dakika nne kabla ya mpira kumalizika, akifunga akiwa karibu kabisa na lango baada ya Samatta kuanzisha mashambulizi ya kushitukiza.

Makipa Kidiaba Muteba wa Mazembe na Ismail Mansouri wa USM walionekana wakishangilia sana na kuwatia moyo wachezaji wao katika kipindi cha kwanza. Kuingizwa kwa Assale na Mghana Daniel Nii Adjei kuliwaimarisha zaidi ndipo wakapata mabao mawili muhimu.

Algeria walimaliza mechi wakiwa pungufu ya mchezaji mmoja, baada ya Zinedine Ferhat kupewa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje. Mazembe wanaofundishwa na kocha wa zamani wa Mali, Patrice Carteron, wametwaa kombe hili kwa mara ya kwanza tangu 2010 walipowacharaza Esperance wa Tunisia kwa jumla ya mabao 6-1.

Wanaungana na Zamalek wa Misri kuwa timu za pili zilizopata manufaa zaidi, nyuma ya Al Ahly wa Misri waliotwaa ubingwa huo mara nane. Timu za kaskazini mwa nchi zimekuwa zikitawala zaidi soka ya Afrika, ambapo mwaka jana Entente Setif wa Algeria ndio walitwaa ubingwa huo.

Kwa ubingwa huo, ina maana kwamba Mazembe watawakilisha Afrika kwenye michuano ya Kombe la Dunia la Klabu la Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) mwezi ujao nchini Japan.

Comments