in ,

Rodriguez wa Everton na wa Real Madrid..

Miongoni mwa nyota wapya walioingia EPL ni James Rodriguez. Ni mara  yake ya kwanza kucheza Ligi hiyo. Tangu alipoanza kandanda amecheza  Ligi za kwao Colombia kisha akaelekea Benfica nchini Ureno na baadaye  Monaco ya Ufaransa.  

Real Madrid ilimsajili akiwa Monaco. Ni staa ambaye anafuatiliwa kwa  ukaribu. Jina lake ni kubwa kuanzia mashindano ya ngazi ya klabu na timu  za taifa. James ni nyota ambaye aling’ara kwenye fainali za Kombe la dunia  mwaka 2014 na baadaye kujiunga na vibopa wa Ulaya, Real Madrid. Msimu  huu wa 2020-2021 amesajiliwa na E verton. James amejiunga na kocha  Carlo Ancelotti ambaye alifanya kazi naye Real Madrid. 

TOFAUTI IKO HAPA 

James Rodriguez anaonekana kuwa mchezaji tofauti tangu ajiunge Everton  msimu huu. Mcolombia huyo anajiamini,anatafuta mpira,anachangamka,  anatengeneza nafasi na tishio kwa tiu pinzani ambazo zinatakiwa  kumwekea ulinzi maalumu kila dakika ya mchezo.  

Chini ya Ancelotti, kikosi cha Everton msimu huu kimeanza vema, huku  James akiwa mchezaji wa kutumainiwa tofauti na alipokuwa chini ya  Zinedine Zidane kule Real Madrid.  

Uhusiano mbovu,kukosekana ukaribu kati ya James Rodriguez na Zidane  unajulikana kwenye kolido za uwanja wa Santiago Bernabeu. Hii ni  miongoni mwa sababu iliyochangia James Rodriguez kupelekwa Bayern  Munich kucheza kwa mkopo, na hata aliporejea hakupata nafasi ya kutosha  kucheza klabuni hapo. 

Sasa chini ya kocha wa zamani za Real Madrid na Bayern Munich, bosi  Ancelotti, kiungo huyo amekuwa chachu ya ushindi wa Everton. Safu ya  ushambuliaji ya Everton yenye kuongozwa na Richarlison, James na  Calvert imekuwa tishio tangu kuanza kwa msimu huu. 

Jose Mourinho akiwa na kikosi chake cha Tottenham Hotspurs  walicharazwa mabao 3-0 wakiwa nyumbani. Everton wamechangamka na  kumfanya James aonekane kuwa mchezaji muhimu.  

James amekuwa akicheza nyuma ya washambuliaji wawili; Richaelison na  Calvert. Ni grisi iliyoanza kulainisha ‘vyuma’ na kuipa ufanisi kazi ya  Ancelotti. Je tofauti ya makocha Ancelotti na Zidane ni ipi katika kutumia  kipaji cha James Rodriguez? 

1. IMANI 

Kati ya vitu vyote muhimu kwa mchezaji na kocha ni kuwa na imani baina  yao. kocha anatakiwa kumwamini mchezaji na mchezaji nae anatakiwa  kuwa na imani na kocha wake. Ancelotti anamwamini James Rodriguez,  wakati Zidane hakuwa akimwamini staa huyo kwenye kikosi chake.  

Ushahidi wa hilo upo katika mifumo ya uchezaji, mbinu na mahusiano  binafsi. Kimbinu Ancelotti anaamini James anaweza kuifanya kazi ya  ufungaji Everton kuwa rahisi zaidi kutokana na umahiri wake,kipaji na  maarifa aliyonayo kuelekea lango la adui. Yote yameonekana Everton. 

2. NAFASI 

Zidane alipendelea kumtumia James kama winga akiwa Real Madrid, hali  ambayo ilimtenga nyota huyo kwenye ‘move’ nyingi zilizokuwa zikisukwa  kwenye mchezo. Kumweka nafasi ya winga ilikuwa kumfanya achangie  maarifa yake badala ya kuwa sehemu kamili ya uzalishaji kama ambavyo  Ancelotti anamtumia kwa kuwa kiunganishi cha safu ya ushambuliaji. 

Chini ya Ancelotti pale Eveton tunamwona James akichza kwa uhuru zaidi,  timu inamzunguka yeye na ndiye anapanga mipango ya kutengeneza  mabao. James hashughuliki na suala la ulinzi, kazi yake ni kushambulia tu  kwa mechi nzima. 

3. KUUNGWA MKONO 

Ancelotti amekuwa akimuunga mkono James kila wakati, iwe ndani ya  uwanja au nje ya uwanja. Hilo halikuwepo kati ya Zidane na James  walipokuwa Real Madrid. Zidane hakuwa akimsapoti nyota huyo, hata pale 

alipompanga hakutoa nafasi ya kumsifu kwa uwezo mzuri anaojaribu kuonesha. 

4. HADHI 

Ndani ya kikosi cha Real Madrid, James alionekana kuwa mchezaji wa  kutoa mchango katika Ligi Kuu pekee, lakini lilipofika suala la mashindano  ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hakupewa nafasi. Jambo hilo lilisababisha  sintofahamu, kwani hakuelewa kwanini anawekwa kando kwenye  mashindano ya Ligi ya Mabingwa ilhali anacheza vizuri kwenye La Liga. 

Kwenye mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2017, James  aliwekwa nje ya kikosi cha Real Madrid dhidi ya Juventus. Hakuwa kwenye  benchi, badala yake alituowa jukwaani hali ambayo ilimuumiza mchezaji  huyo. 

5. MALENGO 

Takwimu zinaonesha kuwa hii ni mara ya tatu kwa kocha Carlo Ancelotti  kumsjaili James Rodriguez akiwa katika timu tatu tofauti. Kwanza  alimsajili James akiwa kocha wa Real Madrid mwaka 2014. Pili alipokuwa  kocha wa Bayern Munich alimsajili James kwa mkopo wa misimu miwili.  Tatu, sasa ni kocha wa Everton amemsajili James kwa mara nyingine tena. 

Wakati akiinoa Napoli, alifanya jaribio la kumsajili James ingawa  hakufanikiwa. Kwa upande wa Zidane hakuwa na malengo ya kumbakiza  James kikosini mwake. Hii ina maana makocha hao wana malengo tofauti  linapokuja jina la James Rodriguez. 

Bila shaka sasa tutamshuhudia James akiwa kwenye kiwango bora na  kuthibitisha kuwa alipokuwa Real Madrid hakupewa nafasi ya kutosha,  lakini sasa yuko Everton na amepewa nafasi anayopenda kucheza, bila  shaka watanufaika naye. Ni muda tu utaongea iwapo Ancelotti, James na  Zidane nani alikuwa sahihi kufanya maamuzi.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Man city

Ni lini Man City watajifunza kwa makosa yao?

cedric kaze

Kaze Kumrithi Zlatko