in

Timu ya Taifa ya Kuogelea….

TIMU ya Taifa ya kuogelea ya Tanzania imeshindwa kwenda kushiriki kwenye mashindano ya 14 ya kuogelea yaliyoandaliwa na Shirikisho la kimataifa la mchezo huo FINA yanayoendelea huko Shanghai, China.

Timu hiyo ya taifa ya kuogelea ya Tanzania iliyotakiwa kuundwa na wachezaji watatu ilishindwa kwenda Shanghai kwa sababu ya baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Tanzania (TSA) kupinga utaratibu uliotumika kuwapata waogeleaji hao.

Waogeleaji hao watatu walipatikana baada ya timu 14 kuingizwa kwenye hatua ya mchujo uliofanywa na Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Tanzania (TSA), ambapo timu 4 zilionekana hazikidhi vigezo vya TSA hivyo kuenguliwa, lakini timu 10 ziliingizwa kwenye mashindano na katika mashindano ya timu hizo 10 walipatakana wachezaji watatu kwa ajili ya kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano hayo ya Shanghai.

Ni wazi Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Tanzania (TSA) lilitakiwa kwa umoja wao kutoa tamko la suala hili mapema badala ya kukaa kimya mpaka siku ya mwisho Tanzania kushindwa kupeleka wanamichezo katika mashindano hayo ya kuogelea yanayofanyika nchini China.

Kwa jinsi hili suala lilivyo inaonyesha wazi TSA ndiyo wahusika wakuu na viongozi wake wamekuwa wakiliendesha shirikisho hilo kiubabaishaji kwa sababu haingii akili wachague timu halafu ipingwe na watu wengine kwamba utaratibu uliotumika kuwachagua waogeleaji wa timu ya taifa ya kuogelea haukuwa sahihi.

Tunajiuliza maswali mengi, je, hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa shirikisho hilo kuchagua wachezaji wa timu ya taifa?, je, walikuwa wakitumia utaratibu gani?, je, kwa nini utaratibu wa mwaka huu upingwe?, ni nani hasa anayepaswa kuchagua timu hiyo?,je, wanatumia vigezo gani kuchagua wachezaji wa timu ya taifa? na maswali mengi mengineyo.

Tunavyofahamu sisi kwa mujibu wa sera ya maendeleo ya michezo ili kufanikisha zoezi la uteuzi  wa timu ya taifa, vyombo vinavyohusika vinatakiwa kuunda kamati maalum za wataalamu anbazo zitapewa madaraka ya kuchagua wachezaji wazuri kutokana na michezo mbalimbali.

Kwa mujibu wa sera hiyo ya maendeleo ya michezo, uteuzi wa timu ya taifa utafanywa na kamati ya wataalamu ya kitaifa ambayo itakuwa imeundwa na chama cha taifa cha mchezo unaohusika. Uteuzi wa mwisho utafanywa na mwalimu wa timu hiyo.

Sasa tunashangazwa iweje viongozi wa juu wa shirikisho la mchezo wa kuogelea kulumbana kuhusiana na uteuzi wa timu ya taifa ya kuogelea wakati wao ni watawala tu na siyo wana kamati ya wataalamu au siyo walimu wa timu hiyo ya taifa ya kuogelea?.

Hapa tunaamini kabisa kuna tatizo la rushwa katika chama hiki ambapo tunaamini TAKUKURU inatakiwa kuingilia kati katika suala hili na pia, kufutailia uteuzi wa wachezaji wa timu ya taifa kuogelea katika siku za nyuma ulikuwa vipi.

Tunasema hivi kwa sababu hatukubali nchi ishindwe kupata uwakilishi wa kitaifa katika mashindano ya kimataifa kwa sababu ya uzembe wa watu wachache, wakati shirikisho la kimataifa la mchezo wa kuogelea ndiyo lilikuwa linalipa gharama zote kwa wachezaji wetu watatu ambao wangeshiriki katika mashindano hayo.

Pia, tunashangazwa na serikali kushindwa kuingilia kati suala hili na kuinusuru timu yetu ya taifa kushiriki katika mashindano hayo ya kuogelea yanayofanyika nchini China.

Katika hali ambayo hatukuitarajia, serikali kupitia mkurugenzi wa michezo katika wizara ya habari, vijana, utamaduni na michezo ilisema yenyewe haina upande katika sakata hilo na wameliacha suala hilo kwa chama husika.

Tunaamini serikali ilitakiwa kuingilia kati zaidi suala hili badala ya kuliachia shirikisho la mchezo wa kuogelea nchini ambalo linaonekana kugubikwa na viongozi wake kutofautiana katika uteuzi wa wachezaji wa timu ya taifa ya kuogelea.

Tunafahamu mara nyingi serikali imekuwa haijihusishi kuingilia ingilia maamuzi ya viongozi wa vyama vya michezo kwa mfano katika mchezo wa soka, lakini katika hili la mchezo wa kuogelea tunaliona ni tatizo tofauti kidogo kwa sababu linahusu timu ya taifa, tena ni malumbano katika uteuzi wa timu ya taifa wakati sera ya maendeleo ya michezo ya serikali imeliweka wazi suala hilo.

Tunaamini wachezaji wa mchezo wa kuogelea nchini hawatakata tamaa ila wataendelea na mazoezi hayo, lakini tunatarajia uongozi wa shirikisho la kuogelea nchini watatueleza umma wa watanzania tatizo ni nini hasa mpaka timu yetu ya taifa imeshindwa kwenda Shanghai.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Nasria akiwa mashindanoni….

TSA amkeni….Olimpiki inanukia London…