in

Timu 5 za kuchungwa Ligi Kuu Bara msimu ujao

LIGI kuu Tanzania bara itaanza rasmi mara baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii, ambapo Yanga na Simba zitakuwa uwanjani kuashiria ufunguzi huo. Mbali ya vigogo hivyo vya soka nchini, Ligi hiyo inaonekana kuwa kivutio zaidi msimu ujao. Kuanzia usajili wa wachezaji, makocha, wataalamu, matangazo na hamasa ya mashabiki imeumba taswira ya kwamba msimu ujao mambo yatakuwa supa kwa timu zingine za ligi hiyo. Makala haya yanaziangazia timu tano ambazo inatarajiwa kufanya vizuri Ligi Kuu msimu ujao.

KMC FC

Watoto wa mkoa wenye kila aina ya starehe ndani ya jiji la Dar es salaam. KMC wanatoka Kinondoni, ambapo kunasifika kuwa na majumba mengi ya starehe za kila aina, wakiwa chini ya kocha msaidizi Habibu Kondo. Usajili wao umevutia wengi ambapo wanatabiriwa kuwa mwiba mkali Ligi Kuu Bara.

Usajili wao unaonekana kuwa makini zaidi hali ambayo imeubua vitaya namba katika kikosi cha kwanza. Wachezaji wapya waliosajiliwa KMC ni Farouk Shikalo aliyemaliza mkataba wake Yanga, Hassan Kessy, Miraj Ibrahim,Awesu Awesu, Iddy Kipagwile na Nickson Kibabage. Pia wamefanikiwa kumrejesha mshambuliaji wao wa zamani Charles Ilamfia kwa mkopo wa msimu mmoja akitokea Simba.

BIASHARA UNITED

Hawa walimaliza Ligi Kuu msimu uliopita wakiwa nafasi ya nne. Nafasi hiyo iliwapa nafasi ya kuwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa kupotia Kombe la Shirikisho.

Biashara United ni wageni wa mashindano ya Kombe la Shirikisho, wamepangwa kuchuana na FC Dikhil ya Djibout ambapo mchezo wa kwanza utachezwa jijini Dar es salaam atika uwanja wa Benjamin Mkapa. Mshindi wa mchezo huo atakwenda kupambana na mshindi kati ya Hay Al Wadi ya Sudan na Ahli Tripoli ya Libya.

Hii ni mara ya kwanza Biashara United kushiriki mashindano ya Kimataifa. Kwa msimu wa pili mfululizo Tanzania inatoa mwakilishi mpya kwenye mashindano ya kimataifa baada ya Namungo kushiriki hatua ya makundi kwenye mashindano ya Shirikisho CAF.

Lakini msimu ujao wanatabiriwa kuwa tiu kali kwa sababu itakuwa imepata uzoefu wa kutosha kwenye mashindano ya kimataifa na ndani hivyo kutisha Ligi Kuu.

GEITA GOLD MINE

Hii ni timu mpya katika Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa imepanda kutoka daraja la kwanza. Vibopa hao wa madini wenye makao yake huko Geita wwapo katika mkakati wa ujenzi wa uwanja wao wa soka ambao wamepanga kuanza kuutumia mwezi Novemba mwaka huu ikiwa mambo yatakwenda sawa kama inavyotakiwa.

Hivi karibuni wamemtangaza kocha wao mpya Ettiene Ndayiragije. Kocha huyo amewahi kuinoa tiu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na kukiongoza kikosi chake kwenye mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani yaliyofanyika nchini Cameroon. Ndayiragije pia amewahi kuzinoa Azam FC, Mbao FC na KMC Fc zote za Ligi Kuu Tanzania. kocha huyo anao uzoefu wa Ligi Kuu na anatabiriwa kuzichachafya timu mbalimbali za Ligi Kuu.

MBEYA KWANZA

Jiji la Mbeya limeweka rekodi ya aina yake kuwakilishwa na timu nyingi za Ligi Kuu nje ya Dar es salaam. Mbeya Kwanza ni timu kutoka jijini Mbeya, imeungana na wenzao Mbeya City na Tanzania Prisons kuwakilisha jiji hilo katika soka Tanzania. bahati mbaya jirani zao Ihefu FC kutoka Rujewa mkoani humo imeshuka daraja.

Hii ina maana Ihefu imeshuka lakini Mbeya Kwanza imeziba nafasi hiyo. Mbeya Kwanza wanatabiriwa kuchukua njia waliyoanza nayo Mbeya City mara baada ya kupanda Ligi Kuu na kutikisa soka nchini Tanzania katika kipindi walichokuwa na kocha Juma Mwambusi.

Usajili wao mkubwa ni golikipa Abdallah Makangana ambaye amewahi kuzidakia Geita Gold Mine na Mbao FC amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Mbeya Kwanza.

MTIBWA SUGAR

Baada ya kunusurika kushuka daraja msimu uliopita, wengi wataitupia macho timu hiyo kuona itafanya nini kuwa bora. Wapo hini ya kocha Thiery Hitimana aliyerejea baada ya kuachana nao kutokana na matatizo ya uongozi.

Mtibwa Sugar baada ya kuondokewa na kocha huyo walimchukua Mohamed Badru ambayue aliinusuru timu hiyo isishuke daraja, lakini sasa amekabidhi majukumu hayo kwa Thiery Hitimana huku yeye akisubiri majukumu mengine kutoka kwa waajiri wake hao.

Ili kujiweka sawa timu hiyo imefanya usajili wa nyota kadhaa, Abdi Banda, Hassan Kibailo,Said Ndemla na Ibrahim Ame. Je nini kitafanywa na wakata miwa hao wa Turiani msimu ujao? Ni jambo la kusubiri na kuona.

TIMU ZENYE HOFU

Mbeya City wamebaki Ligi Kuu kwa kuunga unga tu. Hali yao kwa msimu mzima uliopita ulikuwa mbaya na walikuwa kwenye mstari wa kushuka daraja. Hata hivyo mechi tano za mwisho ziliwasaidia kubadili upepo hivyo kufanikiwa kubaki  Ligi Kuu, huku wakishuhudia ndugu zao ihefu wakiporomoka daraja.

Coastal Union ni kama ilivyokuwa kwa Mbeya City. Angalau Mbeya City wao walipanda nafasi, lakini Coastal Union ilibidi wasubiri hadi siku ya mwisho ya mchezo wa mtoano (play off) dhidi ya Pamba ya Mwanza ili kubaki Ligi Kuu.

Coastal Union wakiwa chini ya kocha Juma Mgunda walikuwa katika hali mbaya lakini wakafanikiwa kuifunga Pamba hivyo kubaki Ligi Kuu. Haikushangaza mara baada ya kubaki Ligi Kuu wakimtupia virago kocha wao Juma Mgunda. Na sasa wanaingia msimu mpya wakiwa na mipango mipya ya kutorudia makosa. Je watafanikiwa kutetemesha Ligi Kuu Bara? Hilo lapaswa kuwa jambo la kusubiri.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

70 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Dar young africans

Septemba ni mwezi mgumu kwa Yanga

Zacharia Hans Poppe

Zacharia Hans Poppe mtetezi,mkosoaji wa soka la Tanzania