in , , ,

*TFF YAOMBA KUMKABILI WAZIRI KUHUSU KATIBA*

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema ipo haja kwa Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kufikiria upya
uamuzi wake wa kutengua usajili wa Katiba ya TFF ya mwaka 2012 na kutaka
itumike ya mwaka 2006, kwani hautekelezeki.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mchana, mara baada ya kikao cha
Kamati ya Utendaji, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema ni muhimu jambo
hilo likaangaliwa upya kwa sababu athari zake ni mbaya, na pengine Dk.
Mukangara hakushauriwa vizuri kabla ya kufanya uamuzi huo.

“Kamati ya Utendaji ya TFF haitaki kubishana na Mheshimiwa Waziri hata
kidogo, ila tunaamini wakati anatamka haya hakufahamu madhara yake, athari
zake na ugumu wa utekelezaji wake. Kwa waliomshauri hili, wamemshauri
vibaya,” amesema Rais Tenga.

Amesema rai ya TFF kwa Waziri ni kuwaita ili wamweleze ni kitu gani wafanye
kunusuru mpira wa miguu wa Tanzania, kwani wanaamini jambo hili litakwisha
baada ya kumwelimisha hasa kutokana na ukweli kuwa kabla ya kufanya uamuzi
huo hakuwasikiliza.

Katika mkutano huo, Rais Tenga alianza kwa kusema kuwa TFF inaiheshimu sana
Serikali, hivyo inaheshimu maagizo yaliyotolewa na Waziri, lakini akaongeza
kuwa TFF ina wajibu wa kutoa ufafanuzi juu ya maagizo hayo.

Amesema lengo la kuelezea historia ya TFF ilikotoka ni kubaini migongano ya
maagizo hayo na taratibu za TFF ambazo kwa bahati mbaya zinasigana na
maagizo hayo.

Rais Tenga amesema TFF ni chombo cha wanachama, ambapo wanachama wake ni
vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu, na ina taratibu za
kufanya uamuzi kwa mujibu wa Katiba yake na za wanachama wake ambazo
zimeidhinishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema si TFF pekee, bali vyama vya nchi zote ambavyo vimeunganishwa na
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), zinaheshimu na kufuata
maagizo na miongozi ya shirikisho hilo la kimataifa la mpira wa miguu.

Rais Tenga amesema TFF haitakiwi kuingiliwa katika uongozi na uendeshaji
wake, kwani jambo hilo likitokea rungu la FIFA litaiangukia TFF, na madhara
yake ni makubwa. Miongozo ya FIFA inasisitiza uhuru wa wanachama wake
katika uendeshaji shughuli za mpira wa miguu, na iko kwenye Katiba ya TFF.

“Sheria za nchi ndizo zilizozaa Katiba ya TFF. TFF ni chama kamili
kinatakiwa kufanya uamuzi wake ili mradi uzingatie madhumuni ya kuanzishwa
kwake. Leo TFF ikiacha mpira wa miguu na kuanza kujishughulisha na gofu,
hapo Msajili ana haki ya kuingilia,” amesema Rais Tenga.

Kuhusu maagizo ya Waziri, Rais Tenga amesema kifungu cha 11 cha Sheria ya
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kinazungumzia usajili wa chama, na si
marekebisho ya katiba, ingawa kanuni zinahusu marekebisho ambapo ameongeza
kuwa uamuzi wa marekebisho ni wa Mkutano Mkuu na si Msajili.

“Ukienda kuomba viza, fomu unapewa na yule anayekupa viza. TFF
tulipowasilisha marekebisho ya Katiba hatukupewa fomu. Msajili akasema
sawa. Jambo la kujaza fomu si la TFF, ndiyo maana tunasema ipo haja ya
jambo hili kufikiriwa upya.

“Usajili tayari umepita, kwamba Msajili hakutoa fomu, mwathirika anakuwaje
TFF? Tunaona ni muhimu jambo hili likaangaliwa upya,” amesema Rais Tenga na
kuongeza kuwa utaratibu wa kusajili Katiba ya 2006 ambayo ndiyo Waziri
ameagiza itumike ulikuwa huo huo uliosajili Katiba ya 2012.

Akizungumzia historia ya TFF kutoka mikononi mwa BMT, Rais Tenga amesema ni
zao za Katiba ya 2004 ambayo ilifanyiwa marekebisho ukumbini na kugongwa
mhuri na Msajili hapo hapo na kuingia kwenye uchaguzi. Katiba hiyo ndiyo
iliyoiondoa BMT kuisimamia TFF.

“Huko ndiko tulikotoka, si kwa kulazimishwa, bali kwa kupewa Katiba ya
2004. Katiba ina utaratibu mzima wa kufanya uamuzi. Maelekezo ya Waziri
yamesahau huko tulikotoka siku nyingi. Uhalali wa marekebisho unatokana na
ridhaa ya Mkutano Mkuu. Hiyo ni kwa mujibu wa Katiba yenyewe, hakuna nafasi
ya BMT,” amesema.

Amesema katika maagizo ya Waziri, ameitaka TFF kufuata Katiba ya 2006 na
kanuni za BMT, lakini Katiba hiyo hiyo ya 2006 haina nafasi ya BMT, na hata
kama TFF ingetaka kutekeleza hilo haliwezekani.

“Kwa maagizo haya inaonekana Waziri kashauriwa vibaya. Tunajua hakuwepo
katika nafasi hiyo (2004) wakati wa makubaliano kati ya Serikali na FIFA
kuacha mpira wa miguu ujiendeshe wenyewe,” amesema Rais Tenga.

Pia amezungumzia umuhimu wa Katiba toleo la 2012, kwani kuna marekebisho
mengi yalifanyika mwaka 2007, 2008, 2009 na 2011 ambapo ukiyafuta maana
yake unakiweka pembeni Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Bodi ya
Wadhamini, wanachama wapya (mikoa), Bodi ya Ligi, Kamati ya Rufani ya
Uchaguzi, Leseni za Klabu na Kanuni za Fedha.

“Kwa uamuzi huu yote yaliyofanyika hayana maana. Waziri sidhani kama
alikuwa anafahamu athari za maagizo yake. Kama angelijua asingefanya uamuzi
huo. Si rahisi kurudi katika Katiba ya 2006. Hao wajumbe wa Katiba ya 2006
unawapata wapi? Maana yake hata vyama wanachama ni batili kwa vile
vimerekebisha Katiba zao 2009 na 2010,” amesema Rais Tenga.

Amesema kwa Serikali kufuta, maana yake ni kutengua uamuzi wa TFF ambapo
madhara yake ni nchi kufungiwa, ambapo timu za Taifa hazitacheza mpira,
klabu hazitashiriki michuano ya kimataifa na wadhamini nao watakaa pembeni
kwa vile hawawezi kudhamini timu ambazo hazishindani kimataifa.

“Dhana kwamba tukae tu tusicheze nje, ni dhana ya watu walio nje ya mpira
wa miguu. Dhamira yetu ni kuhakikisha hatufungiwi. Waziri ametuagiza
tupeleke barua FIFA kuwa ametengua marekebisho ya katiba. Hatupeleki hivyo,
kwani hiyo ni Government interference, watatufungia.

“Nia yetu bado ni Waziri kutupa nafasi ya kutusikiliza,” amesema Rais Tenga
na kuongeza kuwa kuhusu uchaguzi kwa vile FIFA wanakuja ombi la TFF kwa
Waziri ni kuacha kwanza mchakato uendelee hadi ufike mwisho.

“FIFA wanakuja, tuwasubiri. Nilidhani utaratibu huo utaheshimika. Kama mtu
wa mpira haitaki FIFA anataka nini? Ahadi yetu ni kuhakikisha watu wanapewa
haki. Hiyo ndiyo ahadi yetu na tumeisimamia, na ndiyo maana FIFA wanakuja,”
amesema.

Akijibu swali kuhusu waraka, Rais Tenga amesema marekebisho ya Katiba
hayakufanywa kwa siri, ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kufanya
marekebisho hayo kwa njia ya waraka ilipatikana ambapo 70 waliunga mkono na
33 walikataa.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Kutoka TFF Leo…

Man United mbele kwa mbele