in

TFF, Vilabu wamtazame Christian Eriksen, wajihadhari Ligi Kuu Bara

MASHINDANO ya EURO 2020 yanayoendelea katika miji mbalimbali barani  Ulaya yametuleta mshtuko ambao kila kona dunia iliduwaa kwa muda ili kungojea  hatima yake. Ni mashindano ambayo yamekuja katika nyakati ngumu, kwa sababu  kibano cha idadi ya mashabiki viwanjani na muundo wa ukaaji vinazingatiwa  kutokana na mlipuko wa ugonjwa virusi vya corona. Angalau kwa sasa tunawaona  mashabiki viwanjani, lakini bado mwendo ni wa kobe na furaha haijafika kwa  asilimia 100. 

Mojawapo ya matukio makubwa yaliyotokea katika mashindano hayo ni kuanguka  kwa mchezaji Christian Eriksen wa Denmark wakati wa mchezo kati ya taifa lake  dhidi ya Finland kutokana na tatizo la mshtuko wa moyo. Ulikuwa mchezo ambao  mashabiki walijua utasisimua na kuoneshwa ufundi wa timu zao. Bahati mbaya  Erikssen akiwa anatuliza mpira wa kurushwa pembezoni mwa uwanja ili aelekee  lango la adui, ghafla akaanguka na kupoteza fahamu.  

Mwili wake ulijitupa chini bila kinga yoyote. Jambo ambalo liliwashtua watu. Hata  hivyo nahodha wake aliyekuwa karibu Simon Kjaer aliwahi kudhibiti shingo ya  shingo ya mwanasoka huyo isiendelee kulala ardhini ili kumpa nafasi ya kuweka  vizuri na kuepusha madhara zaidi. Yaliyotokea ni simulizi za kusitikisha katika  soka.  

Dunia imewashuhudia nyota kadhaa wakianguka viwanjani baadhi yao kupoteza  maisha. Marc Vivien Foe nyota wa zamani wa Manchester City na Cameroon  alipoteza maisha wakati mchezo unaendelea. Kutoka tukio la Foe hadi Erikssen ni  wazi mabadiliko kadhaa yamefanyika ili kuhakikisha ulinzi na usalama wa  wachezaji wanaoshiriki mchezo kuwa na afya njema.  

Utimamu na uimara wa miili yao ndicho kitu kinachosisitizwa zaidi. kwa hiyo timu  ya madaktari zimekuwa katika maandalizi ya kutosha kukabiliana na matukio  kama ya Erikssen kuliko ilivyo huko nyuma.  

Mchezo wa soka miaka nyuma haukuwa na matukio ya namna hii. Lakini kutokea  kwake yanatukumbusha kuwa yapo miongoni mwetu. Ni matukio ambayo si 

kwamba yanawaumiza wachezaji na viongozi wao, bali mashabiki wa timu zote  ambao kama binadamu husikitishwa na kutokea kwake. 

Mpaka sasa nyota huyo angalipo hospitali akiendelea kupatiwa matibabu ambapo  kocha wa tiu ya taifa ya Denmark, Morten Boesen ameviambia vyombo vya habari  kuwa nyota wao Erikssen atawekewa kifaa maalumu cha ambacho kitaaluamu  kinaitwa ICD kwa sababu mapigo ya moyo yamekuwa ya kasi kuliko kawaida. 

Mwaka 2019 tukio lingine lilimhusisha beki wa Ajax Amsterdam, Daley Blind  ambaye alipata tatizo la moyo, lakinio alirejea uwanjani Februari mwaka 2020  baada ya kuwekewa kifaa cha ICD. Blind naye yupo katika kikosi cha tiu ya taifa  ya Uholanzi kinachoshiriki mashindano ya Euro 2020 na alicheza mchezo wa  ufunguzi dhidi ya Ukraine.  

Maka 2016 mchezaji mwingine wa mchezo wa Kriketi wa Uingereza, James  Taylor naye alilazimika kukatisha maisha ya kucheza mchezo huo baada ya  kuwekewa kifaa cha ICD kutokana na matatizo ya moyo. 

Sasa, tukiachana na mashindano ya Euro tuangalie Ligi Kuu Tanzania Bara  inayoendelea katikla viwanja mbalimbali. Suala la Afya za wachezaji wa Ligi Kuu  Tanzania Bara sioni kama limepewa kipaumbele.  

Afya ya wachezaji wetu wakiwa uwanjani bado ni suala linalotia mashaka zaidi,  huku Shrikisho la soka Tanzania halionekani kuchukulia uzito mkubwa matatizo  ya wachezaji viwanjani.  

TFF ndiye mlezi na msimamizi wa mchezo wa soka kote nchini pamoja na  kuwasimamia wanachama wake ambao ni vilabu vya Ligi Kuu, Ligi Daraja la  Kwanza na Daraja la Pili na kadhalika. 

Kwamba TFF na wanachama wake ambao ni vilabu na vyama vya soka nchini  vinatakiwa kuliangalia kwa umakini tukio la kuanguka Erikssne. Mara nyingi  tunaweza kudhani labda hayatatokea kwenye Ligi yetu, lakini ukweli ni kwamba  mwili wa binadamu aitwaye mchezaji ni sawa na ule wa Erikssen.  

Tofauti ya mchezaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Erikssen ni malezi na elimu ya  mchezo wa soka. Erikssen amekulia katika maizngira bora ya 

vifaa,walimu,ataalamu wa saikolojia,wachua misuli,madaktari na huduma zingine  ambazo zinamwezesha mchezaji kuwa bora zaidi ya kipaji anachokuwanacho. 

Kwa mazingira hayo klabu nyingi Tanzania si jambo rahisi kukutana na wataalamu  wa saikolojia au wachua misuli na wale wanaohusika na afya ya mwili na akili ya  binadamu katika utendaji wa kazi kwa ufanisi. 

Ndiyo maana mwezi uliopita taarifa kutoka moja ya klabu kubwa ya soka nchini  ilibainisha kuwa kocha wao anahitaji wataalamu wa saikolojia kwa ajili ya  kuwaweka sawa wachezaji wake.  

Hilo lilikuwa na maana pamoja na kushiriki mchezo wa soka na kupata fedha  nyingi bado mazingira ya utendaji wa kazi hususani miundombinu ya viwanja na  elimu na rasilimali watu ni changamoto. Wachezaji wa Ligi Kuu wanapitia  changamoto nyingi.  

Makocha wengi wa timu za Ligi Kuu wanakabiliwa na kibarua kigumu, wakati  wao wanajua kufundisha mbinu za mchezo na maendeleo ya mchezaji lakini suala  la saikolojia ya wachezaji wao bado linahitaji wataalamu. 

Vilevile, huduma za afya katika viwanja vingi ni duni kuanzia miundombinu na  uongozi wa timu unavyochukulia masuala ya afya za wachezaji. Suala la majeruhi  ya mchezaji si kuumizwa katika mchezo au mazoezini bali pia kuumia kihisia  ausaikolojia yake. hilo ni jambo ambalo linahitaji kukutanishwa na  wanasihi(wataalamu wa saikolojia) ambao wanafanya kazi ya kushughulikia afya  ya akili.  

TFF na wanachama wake wanatakiwa kujua suala la afya ya mchezaji ni la  kwanza, na inapotokea tatizo la ghafla uwanjani haliwezi kutibiwa kwa kuweka  barafu pekee ambazo mara nyingi zimekuwa zikionekana viwanjani.  

Madaktari wa timu wanatakiwa kuwezeshwa kuwa na vifaa maalumu vya  kukabiliana na matatizo kama ya Erikssen. TFF wanatakiwa kuketi na vilabu vya  soka kuangalia mara mbili mbili suala la afya za wachezaji vinginevyo kuna siku  tunaweza kupoteza wachezaji kutokana na matatizo mfano ya moyo kama  Erikssen. 

Ni muhimu TFF kukagua masuala la utabibu kwa matatibu wote wa vilabu vya  Ligi Kuu. Vitengo vya afya vya vilabu vinatakiwa kuangalia suala la Erikssen  kama sehemu yao ya kuonesha ujuzi na kuokoa maisha ya wachezaji sio kuzoea  kujiandaa kwa matatizo madogo madogo kama mchezaji kuchubuka,kugongana na  kuumia kwa kawaida.  

Madatakari wa timu za Ligi Kuu Tanzania bara wanapaswa kujua kilichotokea kwa  Erikssen kinawezekana kutokea kwenye viwanja vya Jamhuri, Majaliwa, Sokoine,Majimaji,Uhuru,Taifa,Kambarage,Kirumba na vingine.  

Ni wakati wa TFF kuhakikisha wanajiandaa kuepusha kupoteza maisha ya  wachezaji kama vile Marc Vivien Foe. Wanajiandaa kwa matukio ya Erikssen.  Kama TFF,Vilabu na vyama vyama vya soka nchini vinadhani mchezo wa soka  unahusu kuendesha na kumaliza ratiba bila afya za wachezaji basi kuna siku  tutashudia maafa kizembe kabisa. Mwenendo wetu katika Ligi hauridhishi  hususani suala la afya za wachezaji. Inaogopesha sana.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
England

Watoto wa Malkia watawika Euro 2020?

Tanzania Sports

Faida na hasara za kuondoka Sergio Ramos