PSG wamvalia njuga Di Maria

*Arsenal, Man United vikumbo

 

matajiri wa Ufaransa, Paris St-Germain (PSG) wapo tayari kutoa pauni milioni 45 kumsajili winga wa Manchester United, Angel Di Maria.

 

Raia huyu wa Argentina aliyesajiliwa kiangazi kilichopita kutoka Real Madrid ameshindwa kuchanua kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) na sasa PSG wanadhani watampa raha.

 

Di Maria (27) aliwagharimu United pauni milioni 59.7, akivunja rekodi ya usajili nchini Uingereza lakini Kocha Louis van Gaal amemchezesha namba tofauti bila mafanikio.

 

Katika mechi tano zilizopita alianzia benchi hivyo kuonekana kushindwa kutimiza kilichotarajiwa kutoka kwake, huku familia ikiwa haina raha baada ya wezi kujaribu kuvamia nyumba yake familia ikiwa ndani jijini Manchester.

 

Wezi hao walikimbia baada ya Di Maria kubonyeza kitufe cha kuita polisi na king’ora kulia nje ya kasri hilo. Amehamishiwa hotelini tangu wakati huo.

 

Hata hivyo, Man U wanadai hawana nia ya kumuuza winga huyu lakini PSG wanadaiwa watawajaribu kwa kuwasilisha ofa rasmi karibuni baada ya kushindwa kumsajili msimu uliopita.

 

United wanadaiwa kutia nia ya kumsajili mlinzi wa kati wa Athletic Bilbao, Aymeric Laporte, ambaye mkataba wake unasema anaweza kuuzwa ikiwa klabu inayomtaka itatoa pauni milioni 30.

 

Hata hivyo Man U watakabiliana na upinzani kutoka kwa Arsenal ambao pia wanataka kumsajili Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 21.

 

United wataongeza nguvu kwa chipukizi huyu iwapo mipango yao ya kumsajili mlinzi mahiri wa Borussia Dortmund, Mats Hummels.

 

Klabu ya Marseille ya Ufaransa inataka kuwasiliana na Manchester City kwa ajili ya kumchukua kocha wao wa timu ya vijana, Patrick Vieira ili awe kocha nchini mwake kuanzia msimu ujao.

 

Hata hivyo, City wanamthamini sana Vieira na si rahisi kumwachia aondoke, ambapo pia amekuwa akifikiriwa kupewa kazi ya kocha Manuel Pellegrini iwapo bosi huyo atafutwa kazi.

 

Tottenham Hotspur wanajaribu kumsajili kiungo wa Southampton, Morgan Schneiderlin, 25. Inaelezwa kwamba Saints wanataka pauni milioni 20 huku Spurs wakiwa tayari kuwapa kiungo wao, Andros Townsend, 23, au Benjamin Stambouli, 24, na kiasi kidogo cha fedha.

 

Spurs na Arsenal wamekuwa wakimtaka Scheiderlin tangu msimu uliopita na haijulikani kati ya watani hao wa kaskazini mwa London yupi atafanikiwa safari hii, au iwapo wote watamkosa.

 

Arsenal, Chelsea Spurs wanapigana vikumbo kwa ajili ya kumsajili kiungo wa Luton, Charlie Patino mwenye umri wa miaka 11 tu.

 

Bosi wa Chelsea, Jose Mourinho amebainisha kwamba mmiliki wa klabu hiyo, Roman Abramovich ndiye atakuwa na kauli ya mwisho juu ya hatima ya mshambuliaji wao, Didier Drogba, 37, ambaye mkataba wake wa mwaka mmoja unamalizika kiangazi hiki.

 

Newcastle wanataka kumsajili mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Vijana ya England, Patrick Bamford aliyefunga mabao 19 akiwa kwa mkopo Middlesbrough kutoka Chelsea.

 

Manchester United wanataka kumsajili kipa wa Spurs, Hugo Lloris, 28, ikiwa kipa wao, David De Gea, 24, atarudi nyumbani kwao Hispania kujiunga na Real Madrid.

 

Mshambuliaji wa Arsenal, Theo Walcott, 26, amedai kwamba Arsenal ndio timu bora Ulaya kwa 2015, ikiwa ni dalili kwamba hataondoka Emirates.

 

Mmiliki wa Napoli, Aurelio De Laurentiis amemtaka kocha wao, Rafael Benitez kuacha mipango ya kurudi England ili abaki na vijana wake.

 

Torino wanasema huenda wakamuuza beki wao, Matteo Darmian wakipata ofa ‘kichaa’. Arsenal na Manchester United ni kati ya klabu zinazohusishwa na mchezaji huyu wa kimataifa wa Italia.

 

Mshambuliaji wa Newcastle, Adam Campbell, 21, anafanya majaribio katika klabu ya West Bromwich Albion kwa minajili ya kusajiliwa huko.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Chelsea wakaribia ubingwa

Bournemouth, Watford kamili EPL