in ,

Tanzania: Mkazo zaidi michezoni unatakiwa..

Sports Charity Mwanza

Kuna kipindi miaka ya nyuma nilikuwa na majadiliano na wana taaluma wenzangu kuhusu maneno haya mawili-kipaji na utalaam. Wengine wakasema, huna haja ya kuwa na kipaji, unaweza kuwa mwandishi wa habari wakati wowote maadam umepewa au umefunzwa ujuzi wa taaluma hii. Baadhi wakasema, uandishi wa habari ni kipaji.

Wakataja majina ya waandishi wa habari hasa watangazaji ambao majina yao yaliwika au yanaendela kuwika ulingoni hadi leo, wakisema vipaji vyao viliwafikisha mbali. Kuna waliotangulia mbele ya haki na wengine bado wako ulingoni. Hiyo ilihusu taaluma ya uandishi wa habari. Lakini leo nayaleta maneno haya mawili nikiangazia zaidi eneo la michezo.

Miaka zaidi ya ishirini iliyopita, kwa neema ya Mwenyezi na bidii bila shaka nilifanikiwa kujiunga na elimu ya sekondari. Wakati huo ni kushindana kwa kila hali na ulikuwa ni mchakato kwelikweli.

Kuna ambao hawakufaulu moja kwa moja kujiunga na elimu hii, mipango ikafanywa na wakarudia elimu ya msingi hata kwa kuazima majina ya wengine ili wafanikiwe kujiunga sekondari, kwangu haikuwa hivyo. Ndio maana nasema, kwa neema ya Mwenyezi.

Nilipangiwa Ruvu Sekondari mkoani Pwani. Pale Ruvu Sekondari miaka hiyo, utaratibu wa masomo na michezo vilikuwa vinakwenda sambamba. Pamoja na michezo mingine, nilipenda sana mchezo wa kikapu-Basketball-Kila saa kumi jioni, nilivaa jezi zangu na kukimbilia uwanjani. Sikuwa peke yangu. Ilikuwa ni utaratibu wa shule. Lazima.

Kwa nini naleta mfano huu hapa. Tunafahamu kuwa wachezaji wengi ikiwemo wanariadha wenye vipaji wanaibuka sana kutoka Afrika.  Kuna baadhi ya nchi barani Afrika, zinawika kwa kutoa vipaji michezoni kila mwaka iwe ndani au nje ya nchi.

Tanzania Sports
Vipaji huanzia hapa (picha toka Sports Charity Mwanza)

Kuna wanaosema ni asili ya maumbile yao (genetics) lakini kuna wanaoanisha mafanikio hayo na maeneo wanayotoka, vyakula wanavyokula, hali ya hewa, na miinuko, au vilima vilivyopo. Yako mengi, lakini hebu tutazame maeneo machache.

Miaka ya nyuma, wanafunzi wa sekondari walikuwa wanachanganywa wakitokea mikoa mbalimbali. Hii ililenga pamoja na mambo mengine, kujenga udugu na kufahamiana kwa karibu. Lakini pia iliibua vipaji na kuoanisha ubunifu.

Nilisoma na wanafunzi kutoka Mara, Singida, Kilimanjaro, Iringa, Ruvuma, Manyara na kadhalika. Wengi watalikumbuka hili. Lakini tulipofika mashuleni, kulikuwa na mwendelezo wa michezo…kimfumo.

Sitaki kuleta historia hapa, lakini nataka kuunganisha mfumo na vipaji, na pia mfumo na taaluma. Haya yote yanakwenda pamoja. Hoja hizi zinaungwa mkono na mwandishi wa michezo na mtunzi wa filamu Jackie Lebo kama alivyonukuliwa na jarida la Quartz Africa, “Ni mfumo bora kwa wachezaji ambao umeigwa duniani kote…ulioendelezwa na maafisa michezo mapema katika miaka ya 50 na 60. Ilisababisha mafanikio makubwa katika michezo ya Olimpiki miaka ya sitini na nane.”

Kumbe basi mfumo wa makusudi wa kutafuta vipaji na kuvikuza kwa mafunzo mujarabu unasaidia kuibua vipaji na kuviendeleza kitaalamu na kitaaluma mpaka kufikia ngazi ya juu ya kitaifa na kimataifa.

Hili linaungwa mkono na Filbert Bayi, mwanariadha mashuhuri enzi hizo miaka ya themanini akisema, “Mfumo mzuri unaosaka wachezaji kuanzia shule za msingi na sekondari hadi kufikia kwenye vilabu…” umeziwezesha nchi kama Kenya na nyingine za Afrika Magharibi kupata wanariadha na wachezaji imara kwa mwendelezo.

Bayi, bila shaka akiwa ni matokeo ya utalaamu wa kimfumo na kuibuliwa kwa kipaji,  ni Mtanzania aliyewahi kuwa bingwa wa dunia wa mbio za mita 1,500. Hatujasikia wengi wakiwika kama wakati huo kwa miaka hii tuliyonayo.

Kama kuna kitu kinachowachelewesha wengi kufikia malengo ni ile hali ya kuzungumza sana bila kuchukua hatua. Hii inaathiri sana hata maisha ya mtu binafsi. Sasa, sisi kama Taifa, kwa miaka mingi tumezungumzia kuhusu kufufua michezo kama ile miaka ya zamani.

Lakini hatua zinazochukuliwa  ama ni chache au hakuna kabisa. Licha ya changamoto tulizopitia katika uongozi na utawala wa michezo, imebakia lawama tu. Na wanaolaumiwa wengine wameshatangulia mbele za haki.

Mimi nadhani, wakati wa kulaumu umepita. Au wakati wa kuzungumza tu umepita. Kama miaka hiyo michezo ilikuwa inasimamiwa vilivyo na serikali, basi wakati huu ambao serikali inawezesha michezo kisera tu tuiangalie michezo kama burudani na biashara, wajitokeze kwa wengi watu binafsi wanaoweza kuwekeza kwenye michezo ili kuwe na tofauti.

Isibakie juu tu kwenye mpira wa miguu–kuna michezo mingine ambayo uwekezaji wake unahitaji mkakati na malengo ili kujitwalia ubingwa na haina ushindani mkali.

Kinachopungua na ambacho nadhani kinaweza kufufuliwa ni mfumo wenye mikakati. Kuanzia kwenye kusaka vipaji kwa watoto wadogo hadi kwenye vilabu. Ama hakuna, au haupewi kipaumbele. Mfano, kuna wanaodhani elimu ni kufaulu darasani tu.

Vipi kuhusu sanaa na michezo? Kweli, ni muhimu kupata msingi wa elimu, lakini ikiwa mtoto na hatimaye mtu mzima anapenda kuwa ‘msanii’, ‘muigizaji’, mchezaji wa soka, mwanariadha na kadhalika–atajulikanaje bila mfumo wa kumfahamu au kumuibua?

Mara nyingi utakuta wazazi wanasema…”umekalia kucheza tu!” na pengine mzazi hafikirii kuwa hatima ya mwanae iko kwenye ‘mchezo’ ambao mzazi haoni faida. Na mtoto huyu akienda shuleni, walimu hawana muda wa kugundua kipaji chake…kwanza kwa kuwa hakuna mfumo wa kuwatambua na pili kwa kuwa mkazo uko kwenye hisabati na kuzungumza Kiingereza.

Kwa jinsi maisha yalivyo kwa sasa…Tanzania ingekuwa kwenye nafasi nzuri sana kuwa na mfumo chotara-‘hybrid.’ Kukopa kwa waliotutangulia na kuunganisha na hali yetu ya asili kama Watanzania-tubuni mifumo ambayo itawatambua na kuwaibua wenye vipaji kuanzia ngazi ya chekechea hadi juu zaidi. Haya nayo yanahitaji kuchukua maamuzi magumu-kiserikali na kwa watu binafsi.

Mwalimu Nyerere alifaulu. Lakini inasikitisha ikaja kuishia kwenye ‘hakuna fedha za kuendesha michezo.’ Michezo enzi za Mwalimu ilikuwa kuanzia mashuleni-UMITASHUMTA, UMISETA, Majeshi, Mashirika, Wizara na kadhalika. Hali ni hiyo hiyo kwenye Sanaa na Utamaduni.

Leo hayo hayapo na kama yapo basi kwa kweli mvuto wake ni mdogo sana, licha ya kuwa tuna dunia ya mitandao ya kijamii inayoweza kututangaza vyema. Bila shaka yaliachwa nyuma. Pengine hayajawa na umuhimu. Lakini sina uhakika kuwa yamekosa umuhimu katika zama hizi.

Tangu mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa yatokee miaka 1990, michezo nayo ikawa haina mwenyewe. Mafanikio yoyote yanataka kujipanga. Kuna usemi maarufu unaosema, kushindwa kupanga ni kupanga kushindwa. Mafanikio hayaji kwa muujiza. Mafanikio yanapangwa.

Michezo haitakiwi kuchukuliwa kama ‘by the way,’ inahitaji mikakati na utekelezaji. Na hii inaanzia chini kabisa. Mfano mzazi…japokuwa unakimbizana na maisha…unapata muda wa kumfuatilia mtoto wako? Anapenda nini? Anafanya nini? Au ndio hivyo tena…hamuonani mpaka unashtukia yuko sekondari? Na mwalimu, je unawafuatilia wakati wakienda michezoni au unaangalia tu kama wamefanya mazoezi ya masomo uliowaachia?

Tukiangalia mifano ya nchi zingine kubwa duniani…(fursa ya kukopa mafanikio yao.) Utafiti unaonyesha kuwa vijana wengi wana ndoto na matazamio makubwa ya maisha yao. Hivyo kutambua vipaji vyao, hasa wakiwa kwenye taasisi maalum kama shuleni, ni muhimu sana lakini pia ni eneo nyeti.

Siku hizi wana michezo wataalam kwenye vilabu na kwenye timu makini wanasaka na kutambua vipaji vya watoto wakiwa na umri wa miaka saba. Na wakati huu kwa nchi yetu mtoto anakuwa ameanza shule ya msingi.

Kuna sababu zinazowafanya watoto waingie michezoni. Moja kubwa ni kujifurahisha. Ni sehemu yao ya kukua kiakili na hata kimwili, lakini wanacheza kujifurahisha. Na watoto wanapoungwa mkono na wazazi wao na walimu wao wanapata ari–mchezo wowote ule wanaoamua kuucheza kwa kufuata mfumo, ari ya kushinda ndio msukumo wao wa ndani. Tujiulize, kama nchi–mfumo huu upo? Na kama upo unafika hadi ngazi gani? Taifa, au unaishia shuleni tu.

Mambo kadhaa ya kuyagundua pindi mfumo rasmi unapowasaidia watoto kukuza vipaji vyao ni ‘kutambua ikiwa mtoto anaupenda mchezo huo na ana shauku nao.” Na pili “ikiwa wana nafasi kuelezea hisia zao na kupewa fursa ya kuendeleza kile wanachokipenda.” Ugonjwa mkubwa hapa unatokea pale wazazi na hata walimu wanapoua ndoto za watoto na vijana kwa kuwachagulia nini wanatakiwa kufanya katika maisha yao.

Yako mengi. Lakini kuna haja ya kuchukua hatua thabiti, kama si kurejea kwa aliyotuanzishia Mwalimu na kuyakuza, basi tuunde yetu ambayo yataitambua michezo kama kiungo muhimu kukuza udugu, biashara na hata mapato kwa taifa na maisha ya watu binafsi. Miaka imeenda ya kulalamika tu au kuwa mashabiki tu na kuacha kuibua vile vinavyokwenda sambamba na karne ya ishirini na moja.

Inahitaji wadau waingilie kati, lakini pia wasikilizwe. Na nani? Na wenye dhamana. Tuliowapa dhamana ya kuonyesha njia. Hasa wale ambao wamepewa dhamana hiyo kama ajira. Weka mbali wale wa kuchaguliwa, hao watakuja, watateuliwa, watamaliza muda wao watakwenda.

Nadhani wakati ni huu, hebu tujipe changamoto…Wizara ya Elimu, Wizara ya Michezo, na wizara nyingine–michezo ni sekta mtambuka. Kama hakuna uwekezaji wa kutosha kuanzia chini kimfumo, kitaaluma na hata kitaalamu, wale wenye vipaji vyao, vitakufa kila mwaka na wataingia kwenye fani ambazo si zao kihalisi. Na huko watafanya madudu kwa kuwa kimsingi hawakutakiwa kuwa huko…pengine walitakiwa kuwa wanarusha tufe au mkuki uwanjani…

Report

Written by Zawadi Machibya

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Dar Young Africans

Yanga wachague kuwa na Mkwasa au Luc Eymael

Mashabiki Uwanjani

Ubingwa bila mashabiki uwanjani unanogaje?