in

Tamati ya Ligi Kuu: Kinachoweza kutokea

PAZIA la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) linaelekea kushushwa kwa mechi za mwisho wa msimu Jumapili hii. Japokuwa ndiyo tamati yenyewe, bado kuna mtanziko katika mambo kadhaa muhimu ambayo hayajaamuliwa, na wa kuamua ni timu zenyewe dimbani kwa matokeo ya ama kushinda, kushindwa au sare. Kombe Lenyewe Mwali bado kafichwa kwa sababu mwenye dau kubwa bado hajajulikana, japokuwa ni kati ya wababe wawili wa Manchester – Manchester City na Manchester United. Timu zote hizi mbili zina pointi 86, lakini City wana uwiano mzuri wa mabao ambayo ni manane kuliko United. Kwa kuzingatia hayo, mechi muhimu zaidi Jumapili hii ni ile inayozikutanisha Manchester City na Queen Park Rangers (QPR), mchezo unaofanyika Etihad, nyumbani kwa City mbele ya washabiki wake. Mechi nyingine inayotia wadau matumbo joto ni ile ya Manchester United na Sunderland, United safari hii wakichezea ugenini. Ili City watwae ubingwa wanatakiwa kuwa na matokeo kama ya United au mazuri zaidi. Kwa kifupi ni kwamba, City wakishinda kuna uwezekano mkubwa wa kutangazwa wafalme wa soka wa Uingereza.

Ni katika hali hiyo Kocha Mkuu wa Manchester United, Sir Alex Ferguson anasema wao wanaombea litokee jambo la ‘kijinga’ dhidi ya jirani zao (Manchester City) ili wanyakue tonge mdomoni mwao. Kwamba wao United watatekeleza wajibu wao kujitahidi kushinda mechi yao, lakini kulipata kombe itategemea nyumba ya jirani. Lakini ikumbukwe kwamba vijana hao wa Roberto Mancini katika msimu wote wamepoteza pointi mbili tu katika uwanja wao huo wa Etihad, yaani wameshinda mechi zote isipokuwa mbili tu walizotoka sare. Ndiyo maana washabiki wao wengi wana matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa walioupata mara ya mwisho mwaka 1968. Wanachotegemea dhidi ya QPR ni ushindi tu. QPR wananolewa na kocha wa zamani wa City, Mark Hughes aliyetupiwa virago Desemba 2009 baada ya kushinda mechi mbili tu kati ya 11 City walizocheza mfululizo. Kocha huyo pia ameichezea United na Ferguson anamtegemea ‘amsaidie kuiangamiza City’. Kwa ujumla timu mbili hizi za Manchester zinatarajiwa kuibuka na ushindi kwenye mechi zao hizi za mwisho. Ligi ya Mabingwa Ulaya Moja ya mambo yanayotafutwa kwenye mbio za Ligi Kuu ya Uingereza ni nafasi za timu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kwa minajili ya Uingereza wakati huu, panaweza kuwapo nafasi moja au mbili, wakati timu zinazowania ni Arsenal wenye pointi 67, Tottenham waliojikusantia pointi 66 na Newcastle waliovuna pointi 65. Mechi muhimu katika kuamua hili ni kati ya Everton na Newcastle; Tottenham Hotspur dhidi ya Fulham na West Brom wanaoikaribisha Arsenal. Hali ilivyo ni kwamba hatima ya Arsenal imo mikononi mwao wenyewe, kwa maana kwamba wanachotakiwa ni kushinda tu ili kufuzu moja kwa moja, bila kusubiri matokeo ya mechi nyingine. Ushindi utawahakikishia kubaki nafasi ya tatu wanayoshikilia Hata hivyo, ikiwa Arsenal watatoa sare dhidi ya Baggies, wanaweza kuvukwa na kutupwa nafasi ya nne ikiwa Tottenham watawafunga Fulham. Maana yake ni kwamba Washika Bunduki hao wa London hawatakuwa na chaguo zaidi ya kuingia kwenye mechi za mchujo ili kufuzu, huku Spurs wakisonga moja kwa moja kwenye mashindano hayo makubwa ya Ulaya. Ikiwa Arsenal watachezea kichapo nyumbani kwa West Brom, ni dhahiri pia watakuwa wamejiweka pabaya, kwa sababu wataweza kupitwa na Spurs watakaohitaji sare tu ikiwa Arsenal itafungwa mabao mawili au zaidi. Arsenal pia watapitwa na Newcastle inayonolewa na Alan Pardew, ikiwa watawafunga Everton. Vinginevyo ni kwamba Tottenham wakishinda mechi yake tu itakuwa imejihakikishia kupata nafasi ya nne na sare pia inaweza kuitosheleza ikiwa Newcastle hawatawafunga Everton. Kwa upande mwingine, ili Newcastle waweze kuingia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lazima wawafunge Everton na kuomba ama Arsenal au Tottenham wasishinde mechi zao. Ngekewa hizo tatu zikitokea, basi Newcastle itamaliza ligi ikiwa katika nafasi ya tatu. Hata hivyo, ikiwa Chelsea itatwaa Kombe la Mabingwa Ulaya kwenye fainali dhidi ya Bayern Munich mjini Munich Mei 19 mambo yatabadilika Uingereza, kwa sababu timu itakayoshika nafasi ya nne kwenye EPL mwaka huu haitakuwa na nafasi kwenye ligi hiyo tena. Badala yake, timu hiyo itaingia kwenye Ligi ya Europa pamoja na watakaomaliza ligi wakiwa nafasi ya tano, kwani timu inayotwaa kombe hilo inashiriki msimu unaofuata kulitetea. Katika mazingira haya, Arsenal watatakiwa kutumia vyema nguvu na fursa kuwamaliza West Brom, kwani kwao msimu ni kama umeshaisha tu, hawana kikubwa cha kupata wala kupoteza. Spurs wanaelekea pia kwamba watawafunga Fulham, na maana ya haya ni kwamba kuna kila dalili za Newcastle kuachiwa simanzi bila kupenda. Pengine Bayern watalitwaa kombe la Ligi ya Mabingwa, na kwa kufanya hivyo mazingira ya EPL na ushiriki wa msimu ujao kimataifa kutoathiriwa. Ligi ya Europa Katika Ligi ya Europa kuna nafasi moja au mbili, nazo zinaaniwa na timu tatu: Arsenal, Tottenham na Newcastle. Mechi muhimu kwa minajili ya kupata uwakilishi huko ni kati ya Everton na Newcastle; Tottenham dhidi ya Fulham na ile ya West Brom dhidi ya Arsenal. Mazingira yakoje hapa? Timu itakayoshikanafasi ya tano itaingia kwenye Ligi ya Europa. Hata hivyo, Chelsea ikinyakua Kombe la Mabingwa wa Ulaya ni kwamba timu itakayoshika nafasi ya nne kwenye EPL itatupwa kwenye Ligi ya Europa. Matarajio ni kwa Newcastle kumaliza ikiwa nafasi ya tano. Kushuka Daraja Sehemu nyingi penye zawadi pia huwa hapakosi adhabu au karipio na kwa Ligi Kuu ya Uingereza timu zenye matokeo hasi zaidi hushushwa daraja. Tayari timu mbili zimeshaonyeshwa njia ya kushukia, nazo ni Blackburn Rovers, Wolverhampton Wanderers. Nafasi moja imebaki kwenye safari hii ya kushuka, nayo inapatikana siku hii ya mwisho wa msimu wa ligi pia. Timu zinazowindwa kwa hili ni Aston Villa yenye pointi 38, QPR iliyoambulia pointi 37 na Bolton iliookoteza pointi 35 tu katika mechi zake zote. Mechi za kuzingatia kwa hili ni kati ya Norwich City dhidi ya Aston Villa; Manchester City wanaokabiliana na QPR na Stoke City dhidi ya Bolton Wanderers. Ilivyo ni kwamba, kutokana na uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, Aston Villa wana mabao 17 hivyo itakuwa muujiza wakishushwa daraja. Ni katika msingi huo tunawaondoa kwenye kundi hilo na kuwaacha walio vitani hasa; na kivutio ni ikiwa Bolton itaweza kuipiku QPR na kukwepa kushuka daraja. Bolton lazima iifunge Stoke City ili walau kujiweka katika nafasi ya kuweza kubaki ligi kuu. Ikiwa QPR itatoka sare na Manchester City, basi Bolton watahitaji idadi kubwa ya mabao (tisa) ambayo si rahisi, ili kubadili msimamo na kumaliza ligi juu ya QPR kwa tofauti ya mabao. Kihalisia ni kwamba, njia pekee ya Bolton kukiepuka kikombe cha kushuka daraja ni kushinda mechi yake na kuomba QPR wafungwe. Kwa hali ilivyo, kuna uwezekano mkubwa wa QPR kufungwa na City, lakini halitakuwa jambo la kushangaza kuiona Bolton ikimaliza ligi ikitweta kwa sare au hata kufungwa, hivyo kushuka.

Report

Tottenham Hotspur

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published.

Loading…

0

Tamati ya Ligi Kuu (EPL) : Kinachoweza kutokea kesho…

Stars, brewers strike new deal