in , , ,

Villa watarudia makali?

Yapo maswali wakati huu ambapo klabu za Ligi Kuu ya England (EPL) zikijiandaa kuanza mazoezi ili mwezi ujao zirejee kwenye mtanange wa kumalizia mechi zilizobaki kwa msimu huu wa 2019/2020.

Baadhi ya maswali yanayoibuliwa kwenye korido mbalimbali za soka ni juu ya klabu ambapo Mtanzania wa kwanza yumo katika EPL – Aston Villa na huyu si mwingine zaidi ya Mbwana Samatta ambaye pia ni nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania – Taifa Stars.

Moja ya maswali hayo ni juu ya kipi kiliwapata klabu husika kabla ya kusitishwa kwa EPL, ligi na michezo mingine kutokana na janga la kusambaa kwa virusi vya Corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu, Covid-19 na ambayo imeua mamia kwa maelfu ya watu duniani.

Swali ni kipi kilitokea kwenye mtindo wao wa uchezaji kabla ya kusitishwa ligi na kama wanaweza kurejea kwenye makali waliyokuwa nayo ambayo yaliwapandisha daraja kutoka Championship.

Kwa sasa klabu wapo kwenye nafasi za kushuka daraja, ambapo Samatta na wenzake kama Jack Grealish wanategemewa kutumia vipaji, nguvu na mbinu zao kuwaondoa kwenye eneo hilo baya.

“Tunaitaka Villa yetu irudi,” ni maneno waliyokuwa wakisema au kuimba kwa pamoja washabiki kindakindaki wa Villa kwenye dimba la Villa Park nyakati za taabu hivi karibuni, ambapo hawakupenda kuona wakifungwa au kuishia kwenye sare.

Kwa hiyo Dean Smith, yule kocha wao aliyemsajili Samatta na wengine kadhaa, alipokuja na mtindo tofauti akiifanya timu kuonekana kucheza vyema, washabiki wakaona kwamba hatimaye matakwa yao yanatekelezwa na kuanza kuota tena kuwa watakuwa wakali na hata kushika nafasi za juu kwenye jedwali la msimamo wa ligi.

Hisia walizokuwa nao washabik wakati msimu unaanza zilikuwa kwamba sasa watabaki juu, maeneo ya kati ya msimamo au hata juu zaidi ili kujihakikishia kwamba hawawi miongoni mwa timu tatu za chini ambazo hushuka daraja kila msimu.

Ni wazi kwamba washabiki hao walijua kuwa ushindani ni mkubwa baada ya kurudi EPL msimu huu, lakini wakiwa ni timu yenye soka ya kuvutia, na chapa yao ikiwa tofati na wengine, washabiki waliamini kwamba wangefanikiwa, na wamekuwa wakiwaunga mkono kwa kushangilia kwa wingi.

Hata hivyo imetokea kwamba kabla ya kusitishwa ligi, walikuwa katika mwenendo usio mzuri, wakipoteza mechi kutokana na mfumo wao wa kushambulia na kujaribu kuwafungua wapinzani wao kwa kasi badala ya kubaki nyuma kwanza, kuweka mipango, kutoa pasi na kuhakikisha hawazidiwi kule nyuma.

Dalili zilionekana juu ya aina ya timu ambayo kikosi hiki kingekuwa. Hasa kwa kuanzia na mechi za kwanza nyumbani dhidi ya Bournemouth na Everton, katika safari yao kuja Arsenal Septemba na mwisho siku 12 hivi baadaye, walipokwenda kupata ushindi mnono wa 5-1 dhidi ya Norwich.

Baada ya Smith kuonekana ni mkombozi, akiwa pia amewapandisha daraja baada ya ushindi wa 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa – Wembley dhidi ya Derby County, walitumia takriban pauni milioni 150 kwa ajili ya wachezaji.

Kwa pamoja, wachambuzi wa soka, washabiki na wale watu wasiokuwa na upande waliona kwamba huu ni msimu ambao Villa wangefanya alama yao ionekane, kuheshimiwa na jina lao kuanza tena kuogopwa kwenye EPL.

Lakini sasa inaonekana kwmaba mbinu zao haziendi sawa; ama kocha hawaelekezi vyema wachezaji au wachezaji wenyewe hawafuati maelekezo ya kocha na matokeo yake wanaweza kushuka baada ya kukaa kwenye daraja hili kubwa kwa msimu mmoja tu. Washabiki wataumia.

Villa hawakutarajiwa kuwa walipo; wamefungwa mabao mengi kuliko timu nyingine yoyote – mabao 56 msimu huu na wana moja ya uwiano mbovu zaidi wa mabao (-22). Wana matatizo ya kujilinda na wanashindwa kufunga mabao ya kutosha – wanapwaya. Labda wakirudi watakuwa wazuri zaidi.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Jamal Malinzi, Usiniulize alipo Yohana Nkomola

Basketball players

Tanzania inaelekea wapi Kikapu?