in , , ,

Ligi Kuu: Ni vita ya nafasi ya nne

EPL

Ubingwa wa England tayari umeamuliwa, baada ya Chelsea kufanya biashara mapema na kuutwaa wakiwa bado na mechi tatu.Kwa mwenendo ulivyo, nafasi ya pili na ya tatu zitashikwa na Arsenal na Manchester City wanaofungana kwa pointi 70, zikiwa ni 13 nyuma ya mabingwa wateule na Arsenal wana mechi moja mkononi.

 

Zimebaki mechi tatu kwa klabu nyingine zote isipokuwa Arsenal na Sunderland na kwa msingi huu, nafasi moja inayopiganiwa ni ile ya nne kwa ajili ya ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) msimu ujao.

 

Mashindano hayo ni makubwa kwa sababu huleta fedha, na hadhi, ndiyo maaan Arsene Wenger wa Arsenal husema kufuzu huko ni moja ya makombe anayoyatambua.

 

Nafasi hiyo ya nne, kama tunakubaliana kwamba zile tatu za juu ni kana kwamba zimeshatwaliwa, inawaniwa na timu nne, nazo ni Manchester United, Liverpool, Tottenham Hotspur na Southampton. Tutazame timu hizo na fursa husika.

 

MANCHESTER UNITED

 

Msimu wa kwanza wa Louis van Gaal utamalizika kwa mechi za ugenini dhidi ya Crystal Palace na Hull, lakini pia watakuwa na mechi ya nyumbani dhidi ya Arsenal.

 

Siku chache zilizopita ilionekana kwamba United walishajihakikishia nafasi ya nne, hasa baada ya kushinda mechi sita mfululizo.

Walitiwa moyo zaidi na kujiamini baada ya kushinda pia dhidi ya wale walio katika sita bora, Liverpool na Spurs, achilia mbali kuwachana mahasimu wa jiji lao, Manchester City.

 

Lakini mambo yalibadilika kwa sababu Mashetani Wekundu walikuja kuanza kupoteza mechi, ikawa ni tatu mfululizo dhidi ya Chelsea, Everton na West Bromwich Albion – tena bila kufunga hata bao moja.

Kuteleza huku kumewafungulia milango wengine na kuwapa matumaini kwamba wanaweza kuwashika. Rekodi hii ya kufungwa mechi tatu mfululizo haijawahi kuwekwa na United katika miaka 13 iliyopita na inatishia nafasi ‘yao’ ya tatu.

 

 

LIVERPOOL

 

Liverpool wanaelekea ukingoni wakiwa na mechi tatu ambazo zinaweza kusemwa ni ngumu, maana moja ni dhidi ya Chelsea, nyingine watacheza na Crystal Palace waliofufuliwa na kocha Alan Pardew kisha dhidi ya wagumu Stoke.

 

Ili wapate nafasi ya nne pengine watatakiwa kushinda zote na kuwaombea Man U wavurunde. Hiyo ingewasaidia sana kupunguza maumivu yao, hasa ikizingatiwa msimu uliopita nusura wawe mabingwa.

 

Zingatia kwamba baada ya kutofungwa katika mechi 13 tangu Desemba 21 hadi Machi 16, wakiwa wameshinda 10 kati ya hizo, Liverpool wamekuja kupoteza mechi tatu kati ya sita tangu hapo. Wana kazi ngumu na muda unawatupa mkono.

 

TOTTENHAM HOTSPUR

 

Uwezekano wa Spurs kuvuka na kuingia kwenye nne bora, ikiwa ukweli utasemwa, ni mdogo lakini kihesabu inawezekana kwa sababu wako nyuma ya Manchester United kwa pointi saba.

 

Ili washike nafasi hiyo muhimu kwa UCL watatakiwa washinde mechi zote tatu walizobakiwa nazo, zikiwa ni dhidi ya Stoke, Hull na Everton.

Kana kwamba hiyo haitoshi, Spurs wanaofundishwa na Mauricio Pochettino watahitaji United wafungwe mechi zote tatu walizobakiza.

 

United wakipata hata pointi mbili tu kuanzia sasa watawaacha mbali Spurs, ikizingatiwa tofauti ya uwiano wa mabao, Man U wakiwa na 19 zaidi ya Spurs.

 

 

SOUTHAMPTON

 

Vijana hawa wa pwani ya kusini mwa England kiufundi bado wamo kwenye hili jambo japokuwa ni kwa shida. Walianza vyema sana ligi wakiongozwa na Kocha Ronald Koeman, wakawa nafasi za juu kabla ya kuanza kuyumba.

 

Walishangaza wengi kwa sababu timu ilikuwa imeporwa wachezaji wake nyota kama watano, lakini bado wakadunda vyema.

 

Ili wapate hadhi ya kucheza UCL watatakiwa washinde mechi zao zote zilizobaki, mbili zikiwa ngumu dhidi ya Aston Villa waliohuishwa na Kocha Tim Sherwood, Manchester City wanaowania heshima ya nafasi ya pili na Leicester wanaoendelea vyema na mapambano kuepuka kushuka daraja.

 

Hata wakishinda, bado watatakiwa kuongeza mabao kwa wingi ili kuwa na uwiano mzuri kuliko wenzao ambao watatakiwa kuwaombea pia washindwe mechi zao, na hili la pili ni gumu.

 

Kwa ujumla jinsi hali ilivyo, Manchester United wana nafasi kubwa ya kuvuka, maana hata tukisema kwamba kuna uwezekano wakafungwa na Arsenal, wakiwafunga Palace na Hull, kazi inayoonekana kuwezekana, basi watakuwa wamevuka bila kujali wapinzani wao watakuwa wamefanya nini.

 

Tuiweke hivi; ikiwa Liverpool hawatawafunga Chelsea kwenye mechi ya wikiendi hii, si ajabu hili jambo likawa limeshaamuliwa na watu wakacheza kukamilisha tu ratiba na kuwania Ligi ya Europa.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Wahamiaji watikisa kandanda Italia

LIGI YA EUROPA