in , ,

Usain Bolt aingia Olimpiki kwa unyonge

*Apunguzwa kasi, washindani wapania kumpiku

Homa ya mashindano ni jambo la kawaida kabla hayajaanza, lakini kwa Olimpiki 2012 inayofanyika London, Uingereza, ni zaidi ya hofu.

Mtu aliyekuwa na kasi zaidi duniani, akidhaniwa kuwa nyota pekee kwenye mashindano yote haya wala si mkimbiaji bora zaidi hata kwenye kambi yake ya mazoezi.

Usain Bolt – bingwa aliyebadili dhana nzima yam bio, akavunja rekodi ya riadha kwa kubadili mara nne historia zilizoandikwa kwenye vitabu, ghafla amekumbwa na masaibu katika hadhi yake hiyo.

Watu walianza kupigana ukope mwishoni mwa Mei mwaka huu, pale alipokimbia mbio za mita 100 kwa kasi ndogo zaidi katika zama zake hizi, kwamba huenda ndio mwisho wa yale makeke yake mchezoni yanayohitimishwa kwa kumaliza mbio ndani ya sekunde chache.

Hayo yalitokea Ostrava, Jamhuri ya Czech, ambako alihitimisha mbio zake baada ya sekunde 10.04, mwenyewe alichanganyikiwa hivi akiwa haamini kilichotokea, kama ilivyokuwa kwa walimwengu waliokuwa wakimfuatilia.

“Miguu yangu inakuwa kama imekufa vile…na sijui kwa nini mambo haya,” akakiri Bolt mwenyewe.

Sasa kuja kupoteza rekodi yake mara mbili kwenye mbio za mita 100 na mita 200 za majaribio ya Olimpiki nchini Jamaica mwezi uliopita, kumemweka Yohan Blake mbele yake.

Simulizi kuhusu kushindwa kwake kuwika kwenye mbio zilihusisha mambo mengi, ikiwa ni pamoja na wingi wa matembezi ya starehe nyakati za usiku, kubanwa nyama za paja na kukabiliwa na matatizo ya mgongo.

Hayo yakadhaniwa kwamba ndiyo yamemsababisha akaporomoka, akashindwa kushikilia rekodi yake au kuendelea kuivunja kama alivyokuwa ameahidi. Hata hivyo simulizi nyingine zilitiwa chumvi tu.

Umaarufu wa Bolt na mvuto wake ni vitu vinavyoweza kusababisha kuzushiwa mambo ya ajabu kuliko inavyowezekana kwa nyota mwingine yeyote duniani.

Wiki moja baada ya kushikwa ufufutende kwenye mbio za mjini Ostrava, alikimbia kwa sekunde 9.76 jijini Roma, Italia, sawa na kasi kubwa kiasi cha 15 ya 100 kuliko alivyokimbia katika kipindi kile alipovunja rekodi mwaka 2009.

Hata sasa, tunapoikaribia Michezo ya Olimpiki ya London bado anashikilia rekodi tatu kati ya tano za wakimbiaji wa kasi zaidi duniani kwa mwaka huu, ikiwamo rekodi hiyo ya Roma ambayo si ajabu inatisha kuliko ile ya Blake.

Kwa rekodi hizo, ingekuwa ni mwanariadha mwingine yeyote ingetosha kurejesha imani na kuingia kwenye viwanja vya Stratford akiachia tabasamu na kutembea kifua mbele kwa kujiamini.

Lakini Bolt si mwanariadha mwingine yeyote. Unapokuwa umeweka rekodi za aina yake mara mbili kwenye michuano ya Olimpiki iliyotangulia, tena ukiwaacha wenzako wakiwa kama wameganda walikoanzia mbio, ni kama umejijengea jukwaa lako mwenyewe.

Maana mjini Beijing, China, miaka minne iliyopita Bolt alikimbia mbio za mita 100 kama mtu anafumba na kufumbua tu, sekunde 0.2 na mita 200 kwa sekunde 0.66.

Ni wachache wanaokumbuka jinsi Richard Thompson alivyoshinda medali ya fedha kwa mita 100 miaka minne iliyopita, au Shawn Crawford alivyoambulia ile medali ya fedha kwa mbio za mita 200. Lakini safari hii Bolt akishika nafasi ya pili kwenye mbio zozote kati ya hizo, hakuna atakayesahau kwa muda mrefu ujao.

Kabla ya michuano ya majaribio ya Jamaica, Bolt hakuwa amepoteza nafasi yake ya kwanza kwenye mita 200 kwa miaka minne.

Blake alipomshinda, si tu kwa mamia matatu ya sekunde bali kwa kutoka nyuma na kumpita Bolt aliyekuwa anaongoza na amebakisha mita 50 kumaliza mbio, aliacha washabiki wamechanganyikiwa, mikono vichwani na vinywa wazi.

Kwanza Blake aliwahi kumshinda Bolt kwenye mbio za mita 100 na kutwaa medali ya dhahabu kwenye Mashindano ya Dunia msimu uliopita wa kiangazi yaliyofanyika Daegu, lakini inasemwa kwamba kulikuwa na utata. Simulizi zikawa sawa na kubatilisha ushindi badala ya kutangaza mfalme mpya.

Lilikuwa jambo la ajabu kwenye mchezo huu, kwani wakati Blake akishangilia ushindi wake mjini Kingston, Jamaica, Bolt alikuwa akigangwa na mtaalamu wake wa viungo, ikidaiwa kwamba alibanwa na nyama za paja.

Siku chache baadaye aliruka hadi Munich, Ujerumani kwenda kumwona daktari maarufu wa wanamichezo, Hans-Wilhelm Müller-Wohlfahrt – lakini wakala wa Bolt akasema ilikuwa ni katika utaratibu wa kawaida wa uchunguzi wa afya yake.

Kilichofuata baada ya hapo ni kujitoa kwenye michuano ya Monaco, maarufu kwa jina la Diamond League ya Julai 20.

Hiki ndicho kingekuwa kipimo cha ushindani wa kweli kabla ya Olimpiki, lakini maelezo yamekuwa kwamba hakuwa fiti kwa michezo hiyo.

Je, kama hakuwa fiti, itakuwaje kwa Olimpiki ambayo ndiyo tayari imebisha hodi?  Pengine muda huo mfupi umemsaidia kujiweka sawa kwa changamoto kubwa iliyo mbele yake.

Ama kwa uhakika, kuingia kwake kwenye Michuano ya Olimpiki na rekodi hii, kunampa kazi ya ziada, hasa akiwa ameshajua kuna washindani wanaowania kwa udi na uvumba nafasi yake na medali ya dhahabu.

Mbaya zaidi ni pale washindani wenyewe wanapokuwa wameshamsoma vyema, halafu yeye nguvu zake, kama anavyodai, zinamwishia, huku zao zikiongezeka.

Ndio akina Blake na Tyson Gay. Si mmoja wala wawili tu, bali kuna waliokuwa kimya baada ya kufika kileleni na sasa wanarejea – Asafa Powell na Justin Gatlin.

Pengine hawa watamtikisa Bolt safari hii, mwanariadha ambaye kwa miaka ya karibuni amechukuliwa kuwa nyota kwenye michezo yote.

Bolt amekuwa akiwatisha wengine wanapojiandaa kuanza ushindani uwanjani kwa jinsi anavyochekea kamera, akinesanesa kwenye matofali wakati wenzake wakitetemeka.

Pengine safari hii naye atachukua nafasi zao na kulisikilizia shinikizo nafsini mwake, akiwa hana uhakika tena wa kuendeleza ubingwa wake kwa kuvunja si rekodi za wengine tu, bali hata za kwake mwenyewe. Tusubiri tuone.

[email protected]

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Juventus yamfanya Suarez chambo ya Van Persie

Vionjo vya Ufunguzi wa Olimpiki London