in , , ,

NABY KEITA NA UKAMILISHO WA TORATI YA LIVERPOOL

April 28 mwaka 1990, ndiyo ulikuwa mwaka wa mwisho kwa Liverpool kubeba kombe la ligi kuu ya England.

Miaka 28 iliyopita, umri wa mtu mzima. Na kuna uwezekano kabisa asilimia kubwa ya mashabiki wa Liverpool wa sasa hawajawahi kushuhudia timu yao ikibeba kombe la ligi kuu ya England.

Muda umepita, tena muda mrefu tangu Kenny Dalglish awape pombe tamu mashabiki wa Liverpool. Mashabiki ambao ni walevi wakubwa wa mpira lakini wamebaki wakiwa kwa muda mrefu sana.

Hata Liverpool walipojaribu tena kumrudisha Kenny Dalglish awape chakula kama kile alichowapa mwaka 1990 ilikuwa ngumu kwake.

Vizazi vingi sana vilipita, tena vizazi shupavu kama kile cha mwaka 2005. Kizazi ambacho kimebaki kwenye historia ya wapambanaji dunia.

Kitabu chake hutumika kwenye majeshi mbalimbali duniani. Hakuna mwanajeshi anayeshindwa kuhamasika kuipigania nchi yake kila anaposoma kitabu cha kikosi cha Liverpool cha mwaka 2005.

Moyo wa kupigana huongezeka, nguvu za kufanya kitu kikubwa wakati wowote huongezeka kwa kiasi kikubwa kwa sababu tu ya hamasa ya historia ya kikosi cha Liverpool ya mwaka 2005.

Liverpool ambayo hata watu wanaohamasisha ujasiriamali hutumia kuwahamasisha vijana kutokata tamaa mpaka tone la mwisho.

Na hii ni kwa sababu Liverpool kipindi hicho ilijaza wanaume wenye roho ya paka. Kwao wao jiwe moja halitoshi kutoa uhai wao.

Tamaa ilikuwa mbali sana na kiini cha mioyo yao, walikuwa na mioyo ya jiwe. Kwao wao maumivu kuyapata wakati unawapiga ilikuwa ngumu zaidi ya wewe mpigaji kupata maumivu.

Haya yote yalikuwa matokeo ya Rafael Benitez kutengeneza jeshi lisilo kata tamaa.

Jeshi ambalo lilikuwa na viongozi wengi ndani ya uwanja. Utajisikiaje kulia kwako ukawa na kiongozi kama Steven Gerrald?, kushoto kwako ukawa umebeba busara za Xabi Alonso?

Hamasa ya Javier Mascherano haiwezi kukufanya kujihisi kutochoka muda mrefu?, hata kipindi unapokuwa unakosea Jammie Carragher anaweza kukufuata kwa busara na kukuelekeza.

Kwa kifupi Liverpool hii ya kizazi hiki ndiyo Liverpool ambayo ilifanya dhambi kubwa sana.

Dhambi ya kumaliza maisha yao ya mpira katika nyasi za Anfield bila kubeba kombe la ligi kuu ya England.

Inawezekana ushindi wa roho ya paka kule Uturuki mwaka 2005 dhidi ya Ac Milan inaweza kutumika kama poda ya kupaka nyuso zao lakini ukweli unabaki pale pale kuwa nyuso zao zilikuwa na doa moja tu ambalo siyo rahisi kulitoa kwa kupaka poda.

Doa ambalo mpaka leo mashabiki wa Liverpool hawalisahau kwa sababu ya shauku yao kubwa ya kubeba kombe la ligi kuu ya England kwa muda mrefu.

Walijivunia hiki kizazi, walikiamini sana na wakatoa mapenzi yao yote kwenye hiki kizazi lakini ni kosa moja tu ambalo mashabiki wa Liverpool walikosewa, nalo ni kutopewa kombe la ligi kuu ya England.

Hapa ndipo kiu yao ilipo hata Brendan Rogders alipojaribu kuwaaminisha kuwapa maji ya kukata kiu chao walimwamini sana.

Sifa nyingi sana zilienda kwake, akaonekana yeye ndiye Musa katika ardhi ya wa Misri. Aliheshimika sana mwanzoni na dalili zote zilionesha anaenda kuwafikisha kanani.

Lakini kosa alilofanya Steven Gerrald lilikwamisha matumaini ya Liverpool kubeba ubingwa, na baada ya Luiz Suarez kuondoka matumaini ya Liverpool yalizikwa.

Ikahitaji muda kumsubiri mtu atakayekuja kufufua matumaini ya Liverpool. Mategemeo yao yakalalia katika roho ya kijerumani.

Jurgen Klopp alipewa nafasi hiyo, kocha ambaye aliifanya Borrusia Dortmund iwe na sura ya kigori kutoka kwenye uso wa kizee.

Hakuna shaka kuhusiana na uwezo wake, ni moja ya makocha bora duniani ndiyo maana alifanikiwa kuifikisha Liverpool fainali ya UEFA msimu jana.

Mafanikio ambayo ni makubwa sana. Mikono yake imebaki na deni moja tu. Deni ambalo wengi wameshindwa kulilipa kwa muda wa miaka 28 sasa.

Alifanikiwa kutengeneza kikosi kizuri msimu jana lakini kilikosa vichache kukamilisha ubora.

Safu ya kiungo ya Liverpool msimu jana ilichangia upatikanaji wa magoli 11moja kwa moja kati ya magoli 64 waliyofunga katika ligi kuu ya England.

Msimu huu wamemwongeza Naby Keita, mchezaji muhimu aliyekosekana msimu jana kukamilisha ubora wa Liverpool.

Anahusika moja kwa moja kwenye upatikanaji wa magoli, anakaba na kushambulia kwa wakati mmoja , kwa kifupi huyu ndiye aliyekuwa anasubiriwa kukamilisha torati ya Liverpool.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

UNAI EMERY…

Tanzania Sports

NI MAPEMA MNO KUMHUKUMU EMERY