in

Mnyama atafuna hadi mifupa Jangwani

Wachezaji wa viongozi wa Simba wakishangilia baada ya kukabidhiwa Ngao ya Jamii kufuatia ushindi wa 2-0 dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Taifa jana usiku.

Simba jana ilitwaa Ngao ya Jamii kwa ushindi uliostahili wa 2-0 dhidi mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga katika mechi ambayo wana Jangwani walitumia usiku mzima wa jana kukimbizwa mchakamchaka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Haruna Moshi ‘Boban’ na mshambuliaji mpya, Mzambia Felix Sunzu, walifunga magoli mawili ya kipindi cha kwanza na kumpa mwanzo mbaya kipa wa timu ya taifa, Shaban Kado, aliyekuwa akicheza mechi yake ya kwanza tangu ajiunge na klabu hiyo ya Jangwani akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro.

 

Wekundu wa Msimbazi walitawala kipindi chote cha kwanza huku Yanga, wakionekana “kulewa” Kombe la Kagame na kipigo cha jana kilimaanisha kwamba klabu hiyo ya Jangwani imefungwa mechi zote tangu ilipotwaa taji hilo klabu Bingwa wa Afrika Mashariki na Kati.

 

Ilifungwa na Polisi Dodoma katika mechi ya kirafiki kabla ya kukumbana na vipigo viwili vya 3-1 kutoka kwa El Mereikh na El Hilal za Sudan wakati ilipozuru nchini humo kujiandaa na msimu mpya.

 

Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kuingia uwanjani na hata kwenye dimba la kuchezea huku robo saa kabla ya mechi kuanza uwanja ulikuwa bado una mapengo mengi pengine kutokana na kauli za utata za kutishia kutoingiza timu uwanjani kutoka kwa viongozi wa pande zote mbili.

 

Hata hivyo, Simba ndio waliouanza mchezo vyema zaidi na beki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alifanya kazi ya ziada kuuzuia mpira wa krosi uliopigwa na Emmanuel Okwi katika dakika ya kwanza tu ya mchezo.

 

Dakika tatu baadaye, kiungo Machaku Salum, aliyejiunga na Simba katika kipindi hiki cha usajili akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro, alikosa bao la wazi kwa kupiga juu mpira na kuharibu kazi nzuri iliyofanywa na Okwi.

 

Shambulizi la mapema zaidi la Yanga lilikuja katika dakika ya 5 wakati kiungo Kigi Makasi alipopiga shuti la kustukiza lakini kipa wa Simba, Juma Kaseja alilidaka kiufundi.

 

Simba waliendelea kutawala mchezo katika dakika za mwanzo na katika dakika ya 8 tayari walikuwa wameshafanya shambulizi la tatu langoni mwa Yanga wakati Boban na Okwi walipogongeana pasi safi lakini Okwi alishindwa kuuwahi mpira uliorejeshwa kwake wakati wakielekea kumuona kipa wa Yanga, Shaaban Kado.

 

Juhudi ya mashambulizi mfululizo langoni kwa Yanga zilizaa matunda kwa Simba wakati kiungo aliyekataa kucheza soka la kulipwa Sweden, Haruna Moshi ‘Boban’ alipoifungia Simba goli la kwanza katika dakika ya 15 kufuatia kazi nzuri ya mshambuliaji mpya aliyejiunga na klabu hiyo ya Msimbazi katika kipindi hiki cha usajili, Felix Sunzu, aliyetokea El Hilal ya Sudan.

 

Simba iliongeza goli la pili katika dakika ya 39 kwa penalti iliyofungwa na Mzambia Sunzu baada ya beki Nadir Haroub kumuangusha Boban wakati akielekea kufunga goli na refa Israel Nkongo akaamuru iwe ‘tuta’. Sunzu alifunga penalti ya kwanza lakini mwamuzi alilikataa goli kwa maelezo kwamba wachezaji wa Simba waliingia ndani ya boksi kabla ya penalti hiyo kupigwa. Mzambia huyo alifunga kiufundi tena penalti yake ya marudio.

 

Hadi mapumziko Simba walikuwa wakiongoza kwa magoli 2-0.

 

Kipindi cha pili Yanga walionekana kurejea kwa nguvu kiasi tofauti na kipindi cha kwanza ambacho walipotezwa “mwanzo-mwisho”.

 

Huku ikionyesha uhai, Yanga katika dakika ya 66 ilimpumzisha mshambuliaji wake Kenneth Asamoah aliyeipa Kombe la Kagame kwa bao pekee dhidi ya Simba, na nafasi yake kuchukuliwa na Rashid Gumbo, ambaye katika fainali hiyo ya Kagame ndiye aliyempikia Mghana huyo goli la ushindi.

 

Hata hivyo, kutawala mchezo katika kipindi cha pili kwa Yanga hakukuwa na matunda yoyote na kuwafanya mashabiki wa klabu hiyo ya Jangwani kuanza kuondoka mapema uwanjani huku mashabiki wa Simba wakirukaruka kwa furaha, bendera za rangi nyekundu na nyeupe zikitawala anga.

 

Kiungo mpya wa Simba, Patrick Mafisango aliyetawala katikati ya dimba, alitwaa tuzo ya “Mchezaji Bora wa Mechi” hiyo.

Vikosi vilikuwa; Simba: Juma Kaseja, Nasoro ‘Chollo’ Said, Amir Maftah, Juma Nyosso, Victor Costa, Patrick Mafisango, Machaku Salum/ Amri Kiemba (dk.61), Jerry Santo, Felix Sunzu, Haruna Moshi ‘Boban’/Gervais Kago (dk.61) na Emmanuel Okwi/ Shomari Kapombe (dk. 73).

 

Yanga: Shaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Chacha Marwa, Juma Seif ‘Kijiko’, Godfrey Taita, Haruna Niyonzima, Kenneth Asamoah/Rashid Gumbo (dk.66), Jerryson Tegete na Kigi Makasi/ Hamis Kiiza (dk. 52).

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

TFF bows to Simba claim

Premier League – Wenger fury at ‘scandalous’ decisions