in

Mikel Arteta anataka nini kwa mshambuliaji wake?

KOCHA wa Arsenal Mikel Arteta anakabiliwa na kigugumizi cha uamuzi katika uteuzi wa nafasi ya mshambuliaji. Tatizo linalomkabili si lile ambalo unaweza kufikiria kwanza, kuchagua mmoja kati ya wawili Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette. Tatizo liko hivi, inaonekana wote wawili hakuna hata mmoja anayemshawishi kocha huyo kwa sasa kwa kile anachokihitaji kwa mshambuliaji wa kutumikia mbinu zake. 

Arsenal walipata kipigo cha kwanza kutoka kwa Aston Villa, ambako katika mchezo huo Mikel Arteta alimpanga Lacazette, kisha akamtoa nje baada ya dakika 59 za mchezo. 

“Ulikuwa uamuzi mgumu sana kuliko unavyodhani. Nilifikiri wachezaji waliocheza dhidi ya Wolves wanastahili kupewa nafasi nyingine katika siku hii,” alisema Arteta baada ya mchezo huo.

Lakini hiyo ndio imani kwa mshambuliaji mmoja au ameshindwa kumshawishi kocha wake kwa namna fulani? Lacazette hakupangwa tena si kwa sababu Arteta aliona anakidhi mipango yake. Lacazette anapangwa kwa sababu anafanya kazi ya mshambuliaji ambayo inavutia kocha huyo katika mipango yake. 

Lacazette kazi yake katika timu hii ni kubwa, kusema ukweli. Anaunganisha mfumo wa kucheza na anarudi chini zaidi, anatengeneza nafasi kwa Bukayo Saka na kumfikishia Nicolas Pepe. Anafanya kazi ngumu bila mpira,kuziba mianya inayoweza kutumiwa na adui na kupandisha mashambulizi mbele zaidi. yeye ni silaha ya kwanza,ndiye muunganishaji.

Huwezi kutilia mashaka uwezo wa kutimiza majukumu wa Lacazzette. Anapambana bila kuchoka, na anatakiwa kufaya hivyo kwa sababu anapigania jambo ambalo hakupaswa kulifanya. Arteta anatamani labda Lacazzette angekuwa mrefu angalau kwa inchi sita kwenda juu,mwepesi na mwenye ubora wa kukaa na mpira mguuni. Lakini vyote hana.

Wakati Arsenal ilipoanza kipindi cha kwanza, Lacazette alikuwa na nafasi nzuri ya kutoa pasi kwa Pepe au Saka, lakini alishindwa kubuni namna sahihi ya kuwafungua mabeki wa timu pinzani. Hilo halishangazi kwa sababu hajawahi kuwa hodari katika eneo hilo. Lacazette si mahiri wa kubuni mbinu na pia si fundi wa kutengeneza nafasi. Lacazette ni aina ya mtu ambaye unaweza kuwa naye kwenye mahusiano ya mapenzi kwa matumaini kuwa utambadilisha tabia, kila siku unajiaminisha nitambadilisha lakini hakuna kitu. 

Halafu kuna Aubameyang. Kwa kipindi chote cha Mikel Arteta kuwa kocha wa Arsenal amepangwa kucheza akitokea pembeni kushoto, ikiwa na ujumbe tosha yeye si chaguo lake katika nafasi ya mshambuliaji wa kati. Kuna namna ya kumchezesha Aubameyang katika mtindo wa mchezaji huru na mshambuliaji ndani ya boksi. Kwa umri wake inaleta maana zaidi kama atapunguziwa eneo la kucheza na kuzunguka kwenye timu kama wanavyomtumia James Vardy pale Leicester City. 

Juni mwaka jana, Vardy alisema namna kocha wake Brendan Rodgers alivyomsaidia kumudu mbinu zake. “Kocha amenisaidia mengi. Amenifanya nicheze tofauti na awali, hasa namna ya kupokea pasi katika nafasi. Anapenda kuona tunatawala mchezo kwa kupigaiana pasi za kutosha lakini haina maana kutumia nguvu kusaka mpira  hadi eneo la beki wetu na kwenda mbele, ni kupoteza nguvu. Ananiambia naweza kusogea chini kama kuna uwezekano wa kuwapokonya mpira maadui. Zamani nilikuwa nakimbia kushoto hadi kulia,nyuma tena hadi mbele, jambo ambalo kocha anasema ni kutumia nguvu vibaya. Kwa sasa ni kutunza nguvu na kuelekeza akili kuwa tayari kupachika mabao.”

Arsenal wangeweza kumtumia Aubameyang kwa mtindo ambao unatumiwa na Leicester City. Wanatakiwa kumzunguka Aubameyang kuliko kumzungusha kila kona kusaka mpira au kutumia majukumu ya Lacazette kumwezesha Aubameyang. Kwa kipindi hiki Arteta anaonekana kutengeneza mazingira ya kuhitaji mshambuliaji mpya kitu ambacho hakiwezi kufanywa na Arsenal.,

Pengine, namna ya kumtumia ndicho chanzo cha kushuka kiwango cha Aubameyang msimu huu. Kati ya mechi 19 alizoanza amepachika mabao matano. Japo kumekuwa na maboresho ya kiwango chake hivi karibuni, lakini kukosa kupachika mabao ni tatizo linalomkabili kwa sasa. Na kama hafungi mabao, Aubameyang basi hana mchango mwingine. Kumchezesha kutokea pembeni kunamwezesha Arteta kupunguza majukumu ya Lacazette lakini inamaanisha pia kukosa kuwa na mchezaji mbunifu kwenye maeneo ya pembeni.

Kipindi cha kocha Unai Emery aliamini namna nzuri ya kuwatumia Aubameyang na Lacazette ni kuwachezesha kama washambuliaji pacha ili kuziba mapungufu yao. watu wa karibu wa Arteta wanasema anamtumia Lacazette kama nambari 10 nyuma ya nahodha wake Aubameyang na kumwomba Mfaransa huyo kucheza kivingine kulikoalivyozoea. Haiwezekani kucheza kama washambuliaji kamili wawili kwa mbinu za Arteta.

Kama Aubameyang si silaha ya mashambulizi ya Arteta, inaleta swali, kwanini alilazimika kumwongezea mkataba wa miaka mitatu? Kama ilivyo kwa Lacazette, Arsenal bado hawajaanzisha mazungumzo ya mkataba mpya ambapo wa sasa unakwisha mwaka 2022.

Hilo linaonesha kuwa Lacazette si mchezaji aliyepo kwenye mipango ya Arteta miaka ijayo. Kimsingi tatizo hapo sio ubora wa Aubameyang na Lacazette, bali mbinu za timu wanayochezea kwa sasa. Arteta ana tabia ya kutumia neno “umaalumu’ kuzungumzia suala la ubora wa mchezaji katika nafasi fulani, na inasemekana anahitaji kitu kingine kwa mshambuliaji wake wa kati, hivyo wawili alionao kwa sasa wanaonekana kutokidhi matarajio yake. 

Pengine Arteta atatazama zaidi mechi ya dhidi ya Astna Villa kujifunza mengi zaidi kuhusu wapinzani wake hao. Si kwa mara ya kwanza katika msimu huu, lakini mshambuliaji mwenye uchu wa ushindi Ollie Watkins alionesha kitu anachotaka Arteta.

Tanzania Sports

Watkins alicheza dakika nyingi kuliko Lacazette, lakini hata kwa kuangalia hilo, tofauti za viwango vya washambuliaji hawa wawili ni namna ya kuwaweka kwenye mbinu. Watkins alifanikiwa kupokonya mipira mara tano wakati Lacazette hawezi. 

Watkins alisababisha kufanyiwa madhambi mara 9 wakati Lacazette amefanyiwa mara moja. Watkins amegombania mipira ya juu mara 7. Arsenala wana matatizo ya kushindwa kugombania mipira ya juu, jambo ambalo limekuwa likiwaathiri kwenye mechi mbalimbali, wanachezewa krosi 35 huku 25 kati ya hizo zikipigwa kwenye maeneoya wazi.

Si suala la utimamu wa miili kwenye tofauti za Watkins na Lacazette. Mshambuliaji wa Aston Villa, Watkins alimudu kupiga mashuti manne kuelekea langoni mwa Asrenal. Mashuti matatu yalilenga lango, wakati moja lilitoka nje. Lacazette hakupiga shuti hata moja. Takwimu zinaonesha kuwa katika mechi mbili walizokutana Aston Villa na Arsenal msimu huu, Watkins amepiga mashuti mengi kulenga lango la Arsenal kuliko washambuliaji wa  Arteta.

Licha ya kwanza Watkins hana jina kubwa katika soka la Uingereza na kimataifa, lakini mashabiki wa Arsenal wanaweza kuwa na matumaini kwa mshambiliaji kuwa sahihi kwa timu yao. hana ustaa kama Aubameyang au Lacazette.

Laiti kama nafasi anayopata Lacazette ingekuwa anapewa Gabriel Martinelli upo uwezekano mkubwa kuwa asingetolewa kutokana na kitu ambacho angekionesha kumridhisha Arteta. Bahati mbaya katika mchezo dhidi ya Aston Villa Martinelli alikuwa benchi, badala yake akaingizwa Willian kwa matumaini ya kutoa uzoefu wake na ubunifu wa Kibrazil. Martinelli hajacheza mechi yoyote tangu alipoumia kwenye mchezo dhidi ya Manchester United ambapo tulimwona akichezeshwa kama mshambuliaji wa kati. 

Kwa hali ilivyo sasa, nafasi ya ushambuliaji ni eneo ambalo litakuja kuibua mjadala zaidi wakati wa usajili. Katika dirisa la usajili la kiangazi Lacazette na Eddie Nketiah watakuwa wamebakiza miezi 12 katika mikataba yao, uamuzi wa kuwabakiza au kuwatema haujafanyika lakini hali zao za baadaye ni changamoto. Kwa mazingira haya kama wote wawili wataondoka, maana yake Arteta ataingia sokoni kusajili mshambuliaji mpya.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Aishi Manula

Ni lini Aishi Manula tutamuuza nje ?

Kanu

Nyota wa Afrika wameyeyuka ‘Top Five’ Ulaya