in , , ,

Balotelli aenda AC Milan

 

*Chelsea wampeleka Quadrado Juventus

 

*West Brom wamkatalia Saido Beraniho

 

Hatimaye Mario Balotelli anaelekea kuondoka Liverpool kurudi nyumbani kujaribu maisha AC Milan kwa mkopo wa msimu mzima, baada ya kuvurunda msimu uliopita Anfield.

 

Mshambuliaji huyo wa kati alikamilisha vipimo vya afya Milan, ambapo atapunguziwa malipo yake kiasi, huku Liverpool wakiendelea kulipa sehemu ya mshahara wake akiwa Italia. Huenda atacheza mechi ya Jumamosi dhidi ya mahasimu wa Milan, Empoli.

 

“Milan wamekuwa daima moyoni mwangu na nilikuwa na matumaini kwamba siku moja ningerudi hapa. Je, nitamalizia maisha yangu ya soka hapa? Hilo litakuja baadaye, natakiwa kufanya kazi kwa bidii ili niwe na mwaka mzuri.

 

“ Nasubiri kwa hamu kuanza mazoezi na kuonesha watu kwamba nina thamani. Nina motisha nyingi za kufanya vizuri lakini naomba nianze kufanya kazi na si kuongea,” akasema Mtaliano huyo mtata mwenye umri wa miaka 25.

 

Balotelli akiwa ndiye tegemeo la Liverpool msimu uliopita alifunga bao moja tu kwenye ligi kuu nchini England, baada ya kuwa amesajiliwa kwa pauni milioni 16 kutoka Milan Agosti mwaka jana.

 

Hakuambatana na timu kwenye ziara ya kabla ya msimu Mashariki ya Mbali na Australia na amekuwa akifanya mazoezi nje ya kikosi cha kwanza.

 

Alikuwa anaonesha hapendi kuondoka Liverpool kutokana na malipo mazuri licha ya kocha Brendan Rodgers kujenga mazingira ya kumwondoa, lakini baada ya kusajiliwa kwa washambuliaji wakali, Christian Benteke, Roberto Firmino naDanny Ings, huku  Divock Origi akirejea Anfield kutoka Lille alikokuwa kwa mkopo, Balotelli ameona hana namba kabisa.

 

JUAN QUADRADO NAYE AUNGISHWA JUVENTUS

Juan Cuadrado
Juan Cuadrado

Katika hatua nyingine, winga wa Chelsea, Juan Quadrado aliyeshindwa kuonesha makali kwenye msimu wake wa kwanza Stamford Bridge ameelekea Torino, Italia kwa ajili ya kujiunga na Juventus ikiwa atafuzu vipimo vya afya.

 

Quadrado, 27, ambaye ni mchezaji wa kimataifa wa Colombia alipokewa uwanja wa ndege na viongozi wa klabu hiyo, ikiwa ni miezi sita tu tangu ajiunge Chelsea kwa ada kubwa ya pauni milioni 23.3 kutoka Fiorentina na sasa anatarajiwa kukipiga na mabingwa hao wa Italia.

 

Quadrado alicheza mechi 15 tu kwa Chelsea, ambapo ni mara nne tu alianza tangu dakika ya kwanza. Kocha Jose Mourinho amekuwa akionesha dalili za kutaka kumtoa kwa mkopo, akijilaumu pia kwa kitita kizito alichotumia kumsajili bila yeye kulipa fadhila uwanjani.

 

Chelsea walimsajili winga wa Barcelona, Pedro Rodriguez kwa pauni milioni 21.1 Alhamisi hii na tayari katika mechi yake moja ameonesha cheche, akifunga bao na kusaidia kupatikana kwa jingine.

Pamoja na viongozi, Quadrado alipokewa na washabiki na yeye akasema kwamba Juventus ni klabu kubwa inayoheshimika kote duniani na kwamba angependa kuanza kuitumikia kwa nguvu.

 

WEST BROMWICH WAMKATALIA BERAHINO

Saido Berahino
Saido Berahino

West Bromwich Albion wamemkatalia mchezaji wao, Saido Beraniho, 22, aliyewaomba kwamba aondoke akajiunge na Tottenham Hotspur, wakisema kwamba bado mchezaji huyo mwenye mkataba hapo Hawthorns anahitajika.

 

West Brom wamesema msimamo wao uko pale pale kama alivyoueleza mwenyekiti wao, Jeremy Peace, wakisisitiza kwamba kuuza wachezaji si moja ya ajenda zao. Katika mechi ya wikiendi hii dhidi ya Chelsea, bosi Tony Pulis alimwondoa kikosini, akisema hakuwa vyema kisaikolojia kucheza.

 

Beraniho, mzaliwa wa Burundi ambaye ni mshambuliaji pia wa Timua ya Taifa ya Vijana ya England, alifunga mabao 20 msimu uliopita na katika mechi dhidi ya Chelsea West Brom walifungwa 3-2 na Chelsea wakati mechi ya mwisho msimu uliopita waliwapiga The Blues 3-0.

 

Pulis, hata hivyo, alieleza kusikitishwa na dirisha la usajili kubaki wazi baada ya ligi kuanza, akisema huwafanya wachezaji kushindwa kujituma wakati wakitakiwa na klabu nyingine. Amekiri inaweza kuwawia vigumu kumbakisha ikiwa Spurs watatia shinikizo zaidi.

 

“Nina uhakika Tottenham walitaka kubaki na (Gareth) Bale na Manchester United wangetaka kwa nguvu zao zote kubaki na (Cristiano) Ronaldo. Mie si mjinga kiasi cha kusema ‘sifanyi hivi au sifanyi vile,” alinukuliwa akisema Pulis wiki iliyopita.

 

Msimu huu West Brom wamesajili washambuliaji wawili, Rickie Lambert kutoka Liverpool na kuvunja rekodi ya klabu kwa kumsajili Salomon Rondon kwapauni milioni 12 kutoka Zenit St Petersburg, Urusi. Pulis anadai watawashangaza watu kwa kusajiliw achezaji zaidi kabla ya dirisha kufungwa Septemba mosi.

advertisement
Advertisement

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

TIMU YA WIKI EPL

Arsenal wamtaka Cavani