in , , ,

Juventus wawaduwaza Real Madrid

 

Real Madrid wameduwazwa na Juventus baada ya Carlos Tevez na mchezaji wao wa zamani, Alvaro Morata kufumania nyavu zao kwenye mechi waliyopigwa 2-1.

 

Wakicheza mjini Turin, Real Madrid waliendeleza unyonge kwa timu za Italia kwenye ardhi yao, kwani katika safari zao nane huko hawakuweza kushinda.

 

Ilikuwa ni katika mechi ya nusu fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) Jumanne hii, ambapo Juventus wanajaribu kufika fainali kwa mara ya kwanza tangu 2003.

 

Cristiano Ronaldo aliwafungia mabingwa hao wa Ulaya bao lake la 54 kwa msimu huu kwenye mashindano yote, huku akimzidi Lionel Messi wa Barcelona kwa bao moja kwenye UCL, kwani anayo 76 wakati Messi anayo 75.

 

Carlo Ancelotti, kocha wa Real atatakiwa kusuka mipango upya ili walau wapate ushindi wa bao 1-0 nyumbani Mei 13, ambao utatosha kuwafikisha fainali watetee taji lao.

 

Morata alifunga bao baada ya kipa wa Real, Ike Casillas kuutema mpira wa Tevez. Ronaldo alisawazisha baada ya kunasa majalo ya James Rodriguez.

 

Real waliteleaz tena kipindi cha pili, ambapo Tevez akienda kufunga alikwatuliwa na Dani Carvajal, Juve wakapewa penati iliyotiwa kimiani vyema na Tevez.

 

Kocha wa Juventus, Massimiliano Allegri alionekana kuridhishwa na mabao hayo, kwani muda mfupi baada ya kuingia bao la pili, aliongeza beki wa kati, Andrea Bazagli badala ya mshambuliaji Sturaro na kuwamaliza Real.

 

Ancelotti alijaribu kutupa karata nyingine kwa kumwingiza Javier Hernandez ‘Chicharito’ aliyewavusha hatua iliyopita, akimtoa Isco, lakini mambo yalibakia magumu.

 

Nahodha wa Juve, kipa Gialuigi Buffon aliongoza wachezaji na washabiki kushangilia kwa nguvu baada ya kipenga cha mwisho.

 

Hata hivyo, ikiwa tofauti hiyo ya bao moja itawasaidia, itajulikana kwenye mechi ya marudiano itakayopigwa Santiago Bernabeu.

 

Juventus waliweka rekodi UCL kwenye mechi hiyo, ambapo kabla ya Morata kufunga bao, walipigiana pasi 27 ambazo hazijapata kutokea msimu huu, Real wakionekana kupoteana.

 

Wataliano hao wamepoteza mechi moja tu kati ya 18 za mashindano ya Ulaya kwenye uwanja wao na ushindi dhidi ya Real umekuja siku chache baada ya kuutwaa ubingwa wa Italia kwa mara ya nne mfululizo.

 

Kufungwa huku kunamuweka Ancelotti wa Madrid katika hali ngumu, ambapo tayari kuna tetesi za kwamba huenda akafutwa kazi mwisho wa msimu

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

TETESI ZA USAJILI

Mourinho ataka sura mpya Chelsea