in , , ,

Arsenal wamtaka Cavani

 

*Chelsea wawavalia njuga Pogba, Stones

*Barca wakana tetesi za Neymar Man U

 

Wakati dirisha la usajili likielekea ukingoni klabu zipo katika pilika za kupigana kufa na kupona kujiimarisha kwa kuongeza wachezaji wanaowataka, ambapo Arsenal wamegeukia kwa Edinson Cavani wa Paris Saint-Germain (PSG).

 

Walikuwa wakihusishwa sana na Karim Benzema wa Real Madrid, lakini jana alitoa ujumbe kwa mtandao wa jamii akieleza kwamba Madrid ndio kwake, jambo linalowafanya wahusika wa Arsenal kuangalia kwingine.

 

Inaelezwa kwamba wana kiasi cha pauni milioni 50 kwa ajili ya kuimarisha eneo la ushambuliaji, na japokuwa wanafuatilia kwa makini uwezekano wa kumpata Cavani, inadaiwa kwamba wanaweza kupeleka ofa Madrid pia kuona kama watapewa Benzema, kipaumbele cha Arsene Wenger, japo kwa siri.

 

Kocha wa zamani wa Arsenal, George Graham amenukuliwa akisema kwamba ili wawe washindani wa kweli kwenye ligi kuu, wanahitaji mchezaji mwenye uwezo wa kufunga mabao 25 msimu huu, na anasema anayefaa ni Cavani.

 

Naye nyota wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry alisema lazima wasajili mshambuliaji mahiri kama alivyokuwa yeye enzi zake ili wapate mafanikio. Mshambuliaji wa kati tegemeo kwa sasa ni Olivier Giroud huku Danny Welbeck akiwa na majeraha kitambo sasa na hakuna uhakika wa kuwa timamu karibuni na kwa muda mrefu.

 

Cavani, 28, raia wa Uruguay, ameanza ligi kuu nchini Ufaransa msimu huu pasipo makeke, lakini Arsenal wanakubaliana kwamba ni aina ya mtu wanayemhitaji mbele kuwahakikishia ushindi, madhali nyuma tayari wanaye kipa Petr Cech.

 

Katika mechi nane za mwisho Ufaransa mchezaji huyo alifunga mabao 12, hivyo akifanya kazi na akina Alexis Sanchez, Mesut Ozil, Alex Oxlade-Chamberlain na wengineo, Arsenal wanaweza kuwa na mafanikio makubwa kuchuana vilivyo na Chelsea, Manchester City, Manchester United, Liverpool na wengineo msimu huu.

 

Mchezaji huyo anaweza kukubali kirahisi kuondoka PSG, kwa sababu anafunikwa na mshambuliaji mwenzake, Zlatan Ibrahimovic.

CHELSEA KUKOMAA KUWAPATA POGBA, STONES

John Stones
John Stones

 

Chelsea wanaelekea kukaza uzi kuhakikisha wanapata wachezaji wawili muhimu waliokusudia kuwasajili, kiungo Paul Pogba wa Juventus na beki wa kati, John Stones wa Everton.

 

Mkurugenzi wa masuala ya usajili wa Chelsea, Marina Granovskaia, anaendelea na mawasiliano na Juventus kwa ajili ya kumpata mchezaji huyo anayesadikiwa kuthamanishwa kwa pauni milioni 70.

 

Wataliano hao wanasema hawataki kumuuza mchezaji huyo, lakini ukweli kwamba wanaendelea na mazungumzo kunawapa matumaini Chelsea kwamba watampata mchezaji huyo.

 

Mmiliki wa Chelsea ameruhusu zitumike pauni milioni 100 katika kipindi hiki cha mwisho cha msimu kuwapata wachezaji hao wawili.

 

 

Ikiwa Pogba, 22, hataingia Chelsea kiangazi hiki, kuna kila dalili kwamba Barcelona watamchukua mwakani, watakapomaliza kutumikia adhabu ya kutosajili, baada ya kwenda kinyume na kanuni za usajili wa wachezaji chipukizi za Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa).

 

Kwenye suala la Stones, 21, kuna maendeleo, kwani mchezaji huyo amewaandikia Everton kuwaomba wamruhusu aondoke ili akachezee Chelsea. Chelsea wakifanikiwa kumpata Pogba, atavunja rekodi za usajili England, kwani itakuwa pauni kati ya milioni 60 na 70.

 

Kwa Stones, Chelsea walianza na dili la pauni milioni20 likakataliwa mara moja sawa na lile la pauni milioni 26, kisha kwa muda mrefu wakawa wanazungumzia ofa ya pauni milioni 30.

 

Kocha wa Everton, Roberto Martinez amekuwa akisisitiza kwamba Stones hatauzwa kiangazi hiki, lakini kwa hali ilivyo, kuna uwezekano Toffees wakalainika.

 

 

BARCELONA WAPUUZA NEYMAR KWENDA MAN U

neymar
neymar

 

Barcelona wamepuuza taarifa zilizotoka kwamba Manchester United wanajiandaa kutoa ofa ya kihistoria itakayovunja rekodi ya usajili duniani, kutaka kumsajili Neymar kwa pauni milioni 240, zikijumuisha kodi na vitu vingine.

 

Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu amesema taarifa hizo ni potofu, hakuna kitu kama hicho na kukomelea msumari akisema kwamba mabingwa hao wa Ulaya wanatarajia kumwongezea kinda huyo wa Brazil mkataba mpya.

 

Inadaiwa kwamba kwenye mkataba wa Neymar, 23, kuna kifungu kinachosema kwamba klabu yenye kutaka kumnunua itatakiwa kutoa euro milioni 190, lakini Bartomeu amesema hawapo tayari kumuuza kwa sababu wamepanga kubaki naye kwa miaka 15 ijayo.

 

“Hizi nitetesi tu na watu wanaandika tu wakati hakuna kitu kama hicho. Neymar mwenyewe ana furaha sana kuwa hapa Barca. Nasi hatutaki aondoke hata kidogo ni mchezaji mdogo mwenye uwezo mkubwa na amechangia makubwa kwenye mafanikio yetu ya karibuni,” Bartomeu ameeleza akizungumza kupitia Catalunya Radio.

advertisement
Advertisement

 

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Balotelli aenda AC Milan

Kombe la Ligi ni hivi