in , , ,

Bale, Kane watakiwa Man United

*Angel Di Maria na Van Persie kuuzwa
*Arsenal, Liver, Man U wamtaka Ayew

Manchester United wapo katika mchakato wa kusuka kikosi kikali kwa kutaka kuwasajili Gareth Bale, 25 wa Real Madrid na Harry Kane, 21, wa Tottenham Hotspur.

Katika kuzalisha fedha za kumnunua mchezaji huyo ghali zaidi, kocha Louis van Gaal anafikiria kuwauza Angel Di Maria, 27, na Robin van Persie, 31, waliokuwa chini ya kiwango msimu huu.

Van Gaal anaona Di Maria na Van Persie ni mzigo na wanamuongezea tu ankara ya mishahara pasipo kuzalisha, ikizingatiwa kwamba Di Maria alisajiliwa kwa pauni milioni 59.7 na kuvunja rekodi ya England.

Kuondoshwa kwa wawili hao kutapunguza malipo ya mishahara ya pauni 500,000 kwa wiki, ambapo kila mmoja wao analipwa pauni 250,000 kwa wiki.

United wanasema kwamba Bale ndicho kipaumbele kwa sasa na wanatumia sintofahamu iliyopo baina yake, timu na washabiki huko Santiago Bernabeu kumshawishi arudi Ligi Kuu ya England.

Mwaka 2013 Man United walijaribu kumsajili Bale kutoka Spurs lakini wakashindwa pale Real Madrid walipotoa pauni milioni 85 na kumfanya mchezaji huyo wa Wales kuwa ghali zaidi duniani hadi sasa.

Bale hajakuwa na msimu mzuri tangu ajiunge misimu miwili iliyopita Madrid na washabiki wamekuwa wakimzomea, huku wakala wake akidai kwamba wachezaji wenzake hawampi ushirikiano.

Real Madrid wanaelekea kumaliza msimu bila taji lolote baada ya kutolewa kwenye Kombe la Mfalme, Ligi ya Mabingwa Ulaya na sasa wapo pointi nne nyuma ya Barcelona katika La Liga.

Real Madrid walitolewa kwenye nusu fainali na Juventus wiki hii, kocha Carlo Ancelotti akasema hana uhakika wa uwapo wake msimu ujao, na Rais Florentino Perez anatarajiwa kuchukua hatua, ikiwa ni pamoja na kuuza baadhi ya wachezaji, Bale akidhaniwa kuwa mmoja wao.

United wana nguvu ya kifedha ya kumpata Bale, na wanaweza kutoa hata pauni milioni 80, ikizingatiwa ni karibuni wameingia mkataba mnono na wadhamini wapya, Adidas, kwa pauni milioni 750, wakivunja rekodi ya dunia.

Inaelezwa kwamba sasa United wanasubiri klabu yoyote kuwapa ofa kwa ajili ya kumnunua Van Persie kiangazi hiki, akiwa amebakisha miezi 12 kumaliza mkataba wake.

Hakuna klabu iliyosema inamtaka, lakini Di Maria anatakiwa na matajiri wa Ufaransa, Paris Saint-Germain. United watakubali pia kumtoa Di Maria kwa mkopo kisha klabu husika imnunue moja kwa moja mwisho wa msimu ujao.

Inasemekana kwamba PSG wapo tayari kulipa karibu pauni milioni 45 kumnasa nyota huyo wa zamani wa Real Madrid. Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa United, Ed Woodward anaamini watakuwa na kikosi imara kinacholenga kupigania makombe yote msimu ujao.

Tayari wamekamilisha taratibu za kumsajili nyota wa PSV Eindhoven, Memphis Depay na Woodward amesema kwamba wataendeleza kasi hiyo hadi mwisho wa dirisha la usajili.

TETESI NYINGINE

Nahodha wa Liverpool anayeondoka, Steven Gerrard anatarajiwa kurejea Anfield na kuwa kwenye benchi la ufundi pindi akimaliza mkataba wake wa kuchezea LA Galaxy.

Gerrard (34) ameshafanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Liverpool, Tom Werner na kocha Brendan Rodgers juu ya mpango huo.

Liverpool, Arsenal na Manchester United wanapigana vikumbo kumpata mshambuliaji wa Ghana, Andre Ayew, 25, anayecheza Marseille.
Arsenal wanajipanga kumsajili kipa wa Leicester, Kasper Schmeichel, 28, ikiwa mipango yao ya kumsajili yule wa Chelsea, Petr Cech, 32, haitafanikiwa.

Atletico Madrid wanalenga kuwazima Chelsea wanaotaka kumsajili mshambuliaji wao anayeibukia, Antoine Griezmann, 24, na kiungo Koke, 23.

Atletico wanacholenga kufanya ni kubadilisha kifungu cha kuwaruhusu kuondoka kwa kupandisha dau kutoka pauni milioni 43 hadi milioni 100 katika mikataba mipya kiangazi hiki.

Uongozi wa Inter Milan umesema utaendelea na mipango yake ya kumsajili kiungo wa Manchester City, Yaya Toure, 32, kiangazi hiki.

Liverpool wameambiwa kwamba itabidi watoe zaidi ya pauni milioni 20 ili kumpata mlinzi Inigo Martinez, 23, wa Real Sociedad.

Arsenal watapokea pauni milioni tatu kutoka Barcelona ikiwa Barca watatwaa ubingwa wa Ulaya, ikiwa ni sehemu ya dili lilivyokuwa walipomsajili beki wao wa kati, Thomas Vermaelen, 29 aliyekuwa pia nahodha wao.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Sunderland hoi England, hai Afrika

Dnipro, Sevilla fainali Europa