in , , ,

TAARIFA YA MAKABIDHIANO YA OFISI YA TFF YALIYOFANYIKA KATIKA OFISI ZA TFF JIJINI DAR ES SALAAM TAREHE 2 NOVEMBA 2013

Mheshimiwa Rais wa TFF,

Pongezi na Shukurani

1.​Naomba nianze kwa kushukuru kwa kukubali kufanyika kwa shughuli hii ya makabidhiano ya Ofisi. Utaratibu huu haupo kikatiba wala katika kanuni zetu, lakini ni muhimu sana kwa vile unatoa taswira ya uongozi endelevu na ushirikiano unaostahili kuwepo baina ya uongozi mpya na ule wa zamani.

2.​Aidha napenda, kwa mara nyingine, kukupongeza kwa dhati wewe binafsi kwa kuchaguliwa kwako kuwa Rais wa Shirikisho letu pamoja na kumpongeza Makamu wa Rais na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kwa ushindi wao.

3.​Tumeshuhudia mchakato wa uchaguzi uliofanyika kwa uwazi, na ulio huru na wa haki. Ninawashuru sana na kuwapongeza Wajumbe wa Kamati ya Uchanguzi kwa ueledi na kazi nzuri walioifanya. Kwa kiwango hicho hicho ninawapongeza na kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi na wa Kamati za Maadili – ngazi ya awali na ya rufani – kwa kutekeleza wajibu wao kikamilifu na vyema.

4.​Nawajibika kutoa pongezi kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kukamilisha kazi muhimu ya kutuchagulia viongozi wetu kwa utulivu mkubwa.

5. ​Utulivu wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi – kuanzia mwanzo hadi mwisho – ni kielelezo cha ukomavu wa uongozi wa mchezo wa mpira wa miguu nchini. Natoa shukurani za dhati kwa wanachama na wadau wote wa mpira wa miguu nchini kwa mchango wao wa hali na mali katika kufanikisha zoezi hili muhimu kwa mustakabali wa mpira wa miguu nchini.

Dira na Malengo ya Uongozi Uliopita

6.​Dira ya uongozi uliopita ilikuwa ni kujenga mazingira mazuri na endelevu ya maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu nchini. Hii ilitokana na hali ya migogoro isiyoisha na malumbano ya mara kwa mara yaliyokuwepo kabla ya kuingia madarakani.

7. ​Ili kufanikisha dira yetu, uongozi uliopita ulidhamiria kujenga msingi bora wa uongozi wa mpira wa miguu nchini, hivyo kujiwekea malengo yafuatayo:

• Kutengeneza Katiba mpya na Kanuni zitakazokidhi mahitaji ya nchi yetu ya kudumisha demokrasia na utawala bora – uwazi, uwajibikaji, na kadhalika.

• Kuhakikisha kuwa Katiba yetu na Kanuni zetu zinazingatiwa na kuheshimiwa.

• Kuweka Kanuni za Fedha na kuchukua hatua za kujenga uaminifu katika usimamizi wa ukusanyaji, utunzaji na matumizi ya fedha. Tuliazimia kuona hesabu za Shirikisho zinakaguliwa na wakaguzi wenye sifa za kimataifa, na taarifa ya ukaguzi kuwasilishwa kwenye Mkutano Mkuu kila mwaka, bila ya kukosa.

• Kuwa na mfumo wa mashindano utakaongeza ushindani na kuchochea uwekezaji. Azma ilikuwa ni kuongeza idadi ya mashindano ili kutoa fursa kwa vipaji kuonekana na kuendelezwa.

• Kuweka jitihada katika mafunzo ya wataalamu wa mpira wa miguu nchini kwa kuongeza idadi na kozi/semina za mafunzo ya uongozi, uamuzi, ualimu na udaktari wa michezo.

• Kujenga mfumo mpya wa uongozi wa timu za taifa. Lengo lilikuwa ni kuhakikisha kuwa timu za taifa zinakuwa na uongozi wake chini ya Mwalimu/Walimu wa timu ya taifa na kuzitofautisha na Idara ya Ufundi, pamoja na kuhakikisha timu zetu za taifa zinashiriki michezo mingi iwezekanavyo ya mashindano na ya kirafiki.

• Kujenga uhusiano mzuri na wadau na washirika wetu, hususan wadau wetu wakuu ambao ni Serikali na vyombo zake; Mashirikisho ya mpira tuliyojumuika nayo – FIFA, CAF, na CECAFA; Wadhimini na Wafadhili wetu – kampuni, mashirikia ya umma na watu binafsi – wanaochangia maendeleo ya mpira wa miguu nchini kwa hali na mali.

• Kuwa karibu na jamii na kuisaidia jamii. Nia ni kutumia umaarufu wa mchezo wa mpira wa miguu nchini kuhamasisha maendeleo ya jamii, hasa katika masuala ya afya ya jamii – kampeni ya malaria, ukimwi, kupambana na madawa ya kulevya na kadhalika. Rais anayeondoka madarakani ni Balozi wa Malaria nchini na Rais wetu mpya ni mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Malaria, chini ya Uenyekiti wa Waziri wetu wa Afya, Mheshimiwa Hussein Mwinyi.

8.​Utekelezaji wa Dira tuliyojiwekea na malengo yetu ulifanyika kwa ushirikiano wa karibu na wanachama na wadau wetu. Yaliyofanyika yanajulikana. Itoshe kusema kuwa kazi hiyo ilifanyika kwa jitihada kubwa na uadilifu mkubwa na kwamba malengo tuliyojiwekea yalifikiwa.

9.​Katika hotuba niliyoitoa katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu uliopita – Jumamosi, tarehe 26 Oktoba 2013, niliainisha kwa kina nini kilifanyika katika kipindi cha uongozi uliopita pamoja na mafanikio ya kazi iliyofanyika. Napenda kuimbatanisha hotuba hiyo kama sehemu ya taarifa hii ya makabidhiano.

10.​Matarajio yetu ni kuwa, baada ya jitihada za kuweka msingi wa uongozi na wa maendeleo ya mpira wa miguu nchini, nguvu itaelekezwa katika kukuza kiwango cha mpira wa miguu nchini mwetu. Tulichokifanya ni kutayarisha Mpango wa Muda Mrefu wa Maendeleo ya Mpira Miguu Nchini – 2013 hadi 2016 (Long Term Technical Development Plan – 2013 to 2016), ambayo umeambatanishwa kama sehemu ya taarifa hii ya makabidhiano.

11.​Hivyo basi, uongozi mpya una kazi ya kusimamia na kufanikisha utekelezaji wa Mpango huo. Pia, ni matarajio yetu kuwa uongozi mpya utayadumisha mambo ya msingi tuliyojiwekea na kuufanyia kazi upungufu uliopo.

Shukurani kwa Wanachama na Wadau wa TFF

12. ​Pamoja na kuwa nimeshatoa shukurani mara kadhaa, napenda kwa mara nyingine tena kuwashukuru wote waliotusaidia kufika hapa tulipo. Nawashukuru sana wanachama wetu, wadau wetu wote – Serikali yetu na vyombo vyake vyote, wadhamini na wafadhili, waandishi na vyombo vya habari, wapenzi wa mpira na wananchi kwa ujumla kwa mchango wao wa hali na mali. Bila yao tusingefika hapa tulipofika.

13. ​Shukurani maalum zimwendee Mheshimiwa Rais wetu, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa mchango wake usiopimika. Alikuwa ni sehemu mabadiliko haya tangu mwanzo, hata kabla ya uongozi wetu kuingia madarakani. Ametusaidia kwa kiasi kikubwa kuzijenga timu zetu za taifa siyo tu kwa uamuzi wake wa kulipia mishahara ya walimu wa timu ya taifa, bali pia kwa kuwahamasisha vijana wetu kwa hali na mali wafanye vizuri. Sina hakika kuwa yupo Rais mwingine, popote pale duniani, aliye karibu na mapenzi ya dhati kwa vijana wa timu zake za taifa zaidi ya Rais wetu. Zaidi ya hayo, Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha utawala bora katika mpira wa miguu nchini na amefanya kila aliloliweza kuona kuwa kiwango cha mchezo kinapanda na timu zetu zinafanya vizuri. Napenda kutoa shukurani za dhati kwake kwa uongozi na msaada wake.

Wanachama, Katiba na Kanuni, Wafanyakazi, Mali na Mikataba ya TFF

14.​Wanachama

TFF ina jumla ya Wanachama 44 ambao wote ni wanachama hai kama ifuatavyo:

• Vyama vya Mikoa ​– 25
• Vyama Shiriki ​- 5
• Vilabu vya Ligi Kuu ​- 14

15.​Katiba na Kanuni

Hivi sasa TFF ina Katiba Mpya (ya Mwaka 2013) iliyofanyiwa marekebisho ya mwisho na Mkutano Mkuu Maalum wa TFF tarehe 13 Julai 2013.

Pamoja na Katiba TFF ina kanuni zifuatazo ambazo kwa mujibu wa Katiba ya TFF hupitishwa na kamati ya Utendaji:

• Kanuni za Fedha

• Kanuni za Mashindano kuanzia Ngazi ya Wilaya hadi Ligi Kuu

• Kanuni za Utii

• Kanuni za Nidhamu

• Kanuni za Maadili

• Kanuni za Uchaguzi za Uchaguzi za TFF na za Wanachama wa TFF

• Kanuni zinazosimamia Uendeshwaji wa Bodi ya Ligi Kuu

• Kanuni za Mashindano mengine, kama vile Copa Coca Cola, Uhai Cup, Super 8 na Taifa Cup. Ni vyema ikafahamika kuwa kila mashindano lazima yawe na Kanuni zinazosimamia uendeshwaji wake.

TFF inalazimika kuzifanyia marekebisho Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wake kufuatia marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi za TFF. Aidha, TFF inadeni la kutayarisha Kanuni za Chombo cha Usuluhishi (Arbitration Tribunal) kama ilivyoainishwa katika Katiba. Hivi karibuni, TFF imepokea Kanuni za Mfano kutoka FIFA ambayo ipo haja ya kazi hii kukamilishwa na uongozi mpya.

16.​Wafanyakazi wa TFF

Hivi sasa TFF ina jumla ya wafanyakazi 29. Kati yao yupo/wapo

• Katibu Mkuu​​​​​​- 1
• Wakurugenzi / Maofisa Mwandamizi​​- 5
• Wafanyakazi wengine ​​​​- 23​

Katibu Mkuu na Wakurugenzi wapo katika kipindi cha nyongeza cha miezi sita (6) cha mikataba yao, kinachoishia mwishoni mwa mwezi Desemba 2013. Wafanyakazi wengine wapo katika mikataba ya miaka minne yenye kipindi cha majaribio cha miezi sita kuanzia mwanzoni mwa mwezi Septemba 2013. Hivyo basi, uongozi mpya una nafasi ya kufanya tathmini ya mahitaji ya TFF kisha kufanya uamuzi juu ya ajira za Wafanyakazi waliopo kadiri utakavyoona inafaa.

TFF ilichukua hatua ya kuingia kufanya makubaliano ya hiari na wafanyakazi wake ili kuondokana na ajira za maisha (Permanent Employment) na kubaki na ajira za mikataba (Contract Empoyment) kwa wafanyakazi wake wote.

Wafanyakazi wa TFF wamekuwa wakifanya kazi ngumu na saa nyingi kuliko kawaida. Ajira ya TFF haina saa za ziada wala siku za mapumziko. Kutokana na dhana ya kujitolea na ukweli kwamba shughuli nyingi za TFF, kama vile michezo na mikutano hufanyika siku za mwisho wa wiki na sikukuu, ni dhahiri kuwa Wafanyakazi wa TFF wamekuwa wakilazimika kufanya kazi siku hizo, na mara nyingi bila malipo ya saa za ziada. Aidha, kutokana na kukosa uwezo, uongozi uliopita ulishindwa kupandisha mishahara yao ipasavyo.

Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru kwa kuihudumia TFF na mpira wa miguu katika mazingira magumu sana. Tunauomba uongozi mpya uliangalie suala hili kwa umakini, kama moja ya hatua za kuongeza ufanisi wa Sekretariati.

17.​Mali za TFF

​Hivi sasa TFF ina mali zifuatazo:

• Kiwanja cha Karume Stadium, chenye hati namba 27026 iliyotolewa tarehe 10 Novemba 1981. Kiwanja cha Karume kina ukubwa wa ekari 8.26. Ombi la kuingezea muda hati hiyo limeshapelekwa na linafuatiliwa.

• Ndani ya Kiwanja hicho, kuna Jengo la ofisi ya TFF, Jengo la Kituo cha Ufundi (Technical Centre) na Uwanja wa nyasi za bandia wa Karume.

• Kiwanja cha Tanga chenye ukubwa wa hekta 7.6 (ekari 19) kilichopo katika eneo zuri sana mjini Tanga. Kiwanja hiki tayari kimeshalipiwa na hivi sasa taratibu zinaendelea kukamilisha taratibu za kukiandikisha na kupata hati.

• Magari sita (6) na Trekta moja (la kusafishia uwanja wa nyasi bandia). Magari hayo ni: Bus kubwa aina ya Yutong, basi dogo aina ya Coaster, magari ya aina 4WD Ford Everest, Rav 4, Suzuki Escudo na Honda CVR. Mawili kati magari hayo – Suzuki Escudo na Honda CVR – yanatumika lakini hayapo katika hali nzuri. Ni vyema uongozi mpya ukayafanyia tathmini magari hayo na kufanya maamuzi muafaka kadiri utakavyoona inafaa.

• Fedha taslimu Shilingi 33,518,000 na US$ 1,390 zipo katika akaunti hivi sasa. Hii ni baada ya TFF kufanya malipo ya Shilingi 158,000,000 kwa ajili ya Mkutano Mkuu (uliofanyika wiki iliyopita) na malipo ya Shilingi 56,240,000 yaliyofanyika kwa ajili matayarisho ya Timu ya Taifa ya Wanawake U-20 na gharama za mchezo baina ya timu yetu ya Taifa na ile ya Msumbiji uliofanyika wiki iliyopita. Hata hivyo, leo hii US$ 415,000 (Shilingi 664,000,000) kimehamishwa kutoka kwenye Akaunti za TBL kwenda kwenye Akaunti za TFF. Fedha hizo zitakuwa tayari kwenye Akaunti ya TFF ifikapo Jumanne wiki ijayo. Malipo haya yalikuwa yafanyike karibu miezi miwili iliyopita lakini yalicheleweshwa ili kutoa nafasi kwa zoezi la ukaguzi wa fedha za udhamini wa TBL kufanyika. Zoezi limefanyika vyema na kufikia ukingoni, ndiyo maana malipo yamefanyika. Malipo mengine yanayofanana na hayo, ya US$ 420,000 (Shilingi 672,000,000) yanatarajiwa kufanyika wiki mbili kutoka sasa – katikati ya mwezi huu wa Novemba 2013.

Hivyo basi, uongozi unaoingia madarakani hautaanza kwa shida. Ni matarajio yetu kuwa hatua ya awali itakuwa kurejesha fedha kwenye akaunti zilikoazimwa kinachofikia US$ 166,509 – US$ 148,174 kutoka kwenya Akaunti za FAP na US$ 18,335 kutoka kwenye Akaunti ya TRA – kwa ajili ya kugharimia Mkutano Mkuu na matumizi ya Taifa Stars kwa ajili ya matayarisho na safari ya kwenda Gambia.

Ili kujiridhisha kuwa fedha za udhamini zinatumika kama ilivyokubalika katika mikataba, TFF imetoa nafasi kwa wadhamini kufanya ukaguzi wa fedha inazozitoa wakati wowote ule. Utamaduni huu tumekuwa nao katika kipindi chote cha utawala wa uongozi wetu, ili kutoa imani kwa wadhamini na kuhakikisha kuwa malengo ya udhamini husika yanafanikiwa. Huu ni utaratibu mzuri na ni matumaini yetu kuwa utadumishwa.

Jengo la Kituo cha Ufundi ndiyo kwa limekamilika kukarabatiwa na bado halijafunguliwa rasmi. Ukarabati huo umefanikisha kutengenezwa kwa mfumo wa maji machafu unaojitegemea. Hivyo, kutohitaji kutengemea mashimo ya Jengo la Ofisi za TFF. Hatuo ya mwisho ya kazi hiyo ni kukamilisha ukaguzi wa matumizi yaliyofanyika katika ukarabati huo na kuiwasilisha CAF mapema iwezekanavyo. Hayo ndiyo makubaliana kuhusiana na msaada uliotolewa na CAF – unaojulikana kama CAF FAP 2.

Ukarabati wa Kituo cha Ufundi umefanywa, pamoja na sababu nyingine, ili kutoa fursa kwa Mradi wa Ujenzi wa Karume kuendelea. Kama nilivyoeleza katika Mkutano Mkuu, dhamira ni kuwekeza katika Mradi wa Ujenzi wa jengo / majengo yenye hadhi kubwa kwa ajili ya kukodishwa kuzunguka uwanja huo. Jengo lililo karabatiwa na uwanja wa mpira vitabaki na kuendelea kutumiwa kama Kituo cha Mafunzo. Jambo la muhimu ni kuhakikisha kuwa uwekezaji katika mradi huo hauhitaji dhamana ya uwanja wetu na majengo yetu. Ni imani yetu kuwa njia muafaka inapatikana, ikiwa ni pamoja na utaratibu wa ‘Build, Operate and Transfer’ (BOT).

18.​Hesabu za TFF

Ripoti ya Ukaguzi wa hesabu za TFF hadi kufikia Desemba 2012 iliwasilishwa katika Mkutano Mkuu uliopita. TFF ilipata Hati Safi ya Ukaguzi wa hesabu zake na Mkutano Mkuu ukaikubali na kuipitisha ripoti hiyo hesabu za mwaka 2012. Aidha, taarifa ya hesabu za TFF kwa kipindi cha kuanzia tarehe 1 Januari hadi 30 Septemba 2013 kusambazwa kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu.

Ifahamike kuwa TFF imekuwa ikipata Hati Safi, kila mwaka katika kipindi cha miaka minane iliyopita. Hatuna shaka kuwa hali hii itaendelea.

19.​Mikataba ya Udhamini

​TFF inayo mikataba ifuatayo ya udhamini na Wadhamini wafuatayo:

• Vodacom – Udhamini wa Ligi Kuu
• TBL – Taifa Stars
• Coca Cola – Mashindano ya Copa Coca Cola
• SSB & Co – Mashindano ya Uhai
• Bank ABC – Super 8
• Azam Media – Haki za Matangazo ya Television kwa Ligi Kuu

Aidha, baadhi ya vilabu kama vile Yanga na Simba vinadhaminiwa na TBL, Coastal Union inafadhiliwa na Tanga Cement na Azam FC inadhaminiwa na Azam Cola.

Changamoto zinazoikabili TFF

20. ​Zipo changamoto nyingi zinazoikabili TFF lakini kubwa kwa maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu na ambazo uongozi mpya hauna budi kuzishughulikia ni ulazima wa:

• Kuendeleza sola la vijana na watoto kwa kutoa fursa kwa watoto/vijana wengi kupata malezi mazuri ya uchezaji wa mpira wa miguu ili kupanua wigo wa kupata wachezaji wenye vipaji. Katika jambo hili bado tuko nyuma sana. Tulididimia sana kutokana na kufutwa kwa michezo mashuleni. Ipo haja ya uongozi mpya kushirikiana na Serikali kuhamisha michezo shuleni, kama hatua ya wali ya kutatua tatizo la soka la vijana/watoto.

• Kuendeleza soka la wanawake. Matatizo ya soka la wanawake yanafanana na ya soka la vijana. Tofauti ni ndogo sana. Kama ilivyo kwa soka la vijana, hatua muhimu kufanyika kwa jitihada ya kuwahamasisha wasichana wacheze mpira wa miguu shuleni.

• Kuhakikisha ueledi unazingatiwa katika uongozi wa Vilabu na Vyama Wanachama wa TFF. Kinyume chake hatutaweza kushindana na wenzetu ambao walishapiga hatua katika taaluma ya uongozi wa michezo. Vilabu vyetu ni lazima vihakikishe kuwa vinatimiza masharti ya ‘Club Licencing’ kama yalivyotolewa na CAF, pamoja na marekebisho yake. Huu ni mtihani kwetu. Ni lazima tufaulu kutimiza masharti hayo, vinginevyo tutabaki nyuma. Ipo haja ya kuuangalia kwa mfumo wa uongozi wa Vilabu vyetu na Vyama Vyetu kwa azma ya kubuni mfumo utakaotuletea ufanisi zaidi wa kiungozi na uendeshaji kuliko ilivyo hivi sasa.

• Kuhamasisha uwekezaji katika maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu nchini. Tuna upungufu mkubwa wa vifaa na viwanja vya kuchezea. Ni vigumu kuundeleza mchezo wa mpira bila ya kuwa na viwanja vya kuchezea na vifaa. Aidha, zinahitajika raslimali watu na fedha katika kulea na kuwaendeleza wachezaji na wataalamu wetu. Licha ya hapo kiasi kikubwa cha fedha kinahitajika kwa ajili ya matumizi mengine ili timu ifanye vizuri. Kwa maneno mengine tunahitaji kufanya kila jitihada kuhamasisha watu binafsi, makampuni na Serikali iwekeze katika mpira, wadhamini zaidi wajitokeze na wapenzi wengi zaidi wachangie timu zao – kwa njia mbalimbali – ili kuongeza mapato ya vilabu na vyama husika. Vilabu vyetu na Vyama Wanachama wa TFF vinakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha za uendeshaji. Mawazo au fikra kuwa kuna fedha nyingi katika mpira wa miguu ni dhana isiyo na msingi na inayotokana na kutofahamu gharama za uendeshaji wa vilabu na vyama vyetu. Pamoja na ongezeko kubwa la mapato ya milangoni na mchango wa udhamini katika kipindi cha uongozi uliopita, bado kinachopatikana hakikidhi hata theluthi moja ya mahitaji muhimu. Haja ya kuongeza mapato ndiyo changamoto mama. Ikitatuliwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza makali ya changamoto nyingine.
• Ili kuvutia uwekezaji, udhamini na misaada kwenye mpira wa miguu, ni lazima tuhakikishe kuwa tunaendelea na jitihada za kujenga uaminifu wa utunzaji na matumizi ya fedha ndani ya TFF. Ipo haja ya kuhakikisha kuwa Kanuni za Fedha zinazingatiwa na hesabu zetu zinakaguliwa mara kwa mara. Mpango wa Tiketi za Elektroniki ni muhimu usimamiwe kwa nguvu zote kwa vile sio tu utatuongezea mapato bali pia utatoa picha ya uaminifu na ueledi.

Uhusiano na ZFA

21.​TFF haina budi kufanya kila linalowezekana kudumisha uhusino mzuri baina yake na ZFA. TFF inatambulika na FIFA kama msimamizi wa mchezo wa mpira wa miguu nchini Tanzania. Lakini ukweli ni kuwa mchezo wa mpira katika visiwa vya Unguja na Pemba unasimamiwa na ZFA. Hakuna matarajio ya hali hiyo kubadilika. Kwa sababu hiyo, upo ulazima wa kudumisha uhusiano uliopo na kuhakikisha kuwa ZFA inapata haki ya kupewa baadhi ya miradi inayotokana na fedha za FIFA – FAP. Kwa vile fedha hizo hatolewa kwa njia ya miradi, utaratibu tuliokubaliana ni kuhakikisha kuwa kila mwaka baadhi ya miradi / semina zinafanyika visiwani.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Uharibifu wa Mali na kukosa nidhamu kwa baadhi ya wapenzi wa Simba ni Aibu….

Arsenal mbele kwa mbele